Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

DKT. SHEIN NA KARUME NDANI YA BIFU JIPYAAA

 


http://zanzibardaima.files.wordpress.com/2013/03/shein.jpgKATIKA kauli inayoekelea kumlenga mtangulizi wake katika Ikulu ya Zanzibar, Rais Ali Mohamed Shein, amesema hawezi kumzunguka Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete kwa kupigia debe Muungano wa mkataba kama wanavyotaka baadhi ya Wazanzibari.
Vile vile, Dk. Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, alisema kamati ya maridhiano inayopinga muundo wa muungano wa serikali mbili, ilikusudia kumgombanisha, kumzulia na kumdhalilisha kwa wananchi na wanachama wa CCM kwa kumhusisha na harakati zao.

Ingawa hakutaja jina la kiongozi yeyote wa Zanzibar mbali tu ya kusema ni Wazanzibari, miongoni mwa viongozi waandamizi wa Zanzibar ambao wanatajwa kuupigia chapua Muungano wa Mkataba ni pamoja na Rais Mst
aafu, Amani Karume ambaye anadaiwa kushirikiana vilivyo na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, kushikiza Muungano wa Mkataba.
Dk. Shein aliyasema hayo kwenye mkutano mkubwa wa hadhara wa CCM uliofanyika jana kwenye viwanja vya Kibandamaiti Mkoa wa Magharibi Kisiwani Unguja.

Alisema kamati hiyo imepotosha ukweli  kwa kutaka kuuaminisha umma kwamba Wazanzibari wengi wanataka Muungano wa Mkataba hali ambayo ingeweza kusababisha mgongano baina ya wananchi, wanachama wa CCM na serikali yao.

“Nilisikia kwa mara ya kwanza kuwapo kwa kamati ya  maridhiano na hasa baada ya kusikia Dk. Amani Karume na Maalim Seif wamekutana Ikulu, sikuwa na hofu kwa kuwa natambua umuhimu wa maridhiano, sikujua kama kulikuwa na kamati ya maridhiano ya kudai Muungano wa Mkataba,”alisema Dk. Shein.

Aidha, alisema wakati fulani mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar mwaka 2010, aliombwa na mtu mmoja akutane naye na alipomkubalia mtu huyo alikwenda Ikulu akiwa na watu wengine watano kati yao wakiwamo mawaziri wake wawili.

Alisema walipokutana naye walimweleza kuwa walikwenda kumpongeza kwa ushindi alioupata na kumjulisha kuwa wao ndiyo walioshiriki kuleta maridhiano ya kisiasa na kumkutanisha Dk. Karume na Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 5 mwaka 2009 katika mazungumzo ya faragha kwenye Ikulu ya Zanzibar.

Akifafanua zaidi, alisema kwa mara ya pili walimwendea na kumpa pole kwa ajali ya kuzama meli ya MV Spice Islander, lakini mara ya tatu walikwenda wakiwa na ajenda ya kutaka serikali ya Muungano wa Mkataba na kumweleza kuwa wanamtegemea awasaidie katika madai hayo.

“Niliwaambia wasubiri kuyatoa mawazo waliyonayo kwenye tume ya mabadiliko ya katiba mpya,  niliwaambia kwamba mawazo hayo si yangu ila ni yenu na msinitegemee katika hilo, mimi ni Rais wa Zanzibar, nina chama changu na serikali haina mawazo kama mliyo nayo nyinyi hivyo msinichonganishe,”alisema na kushangiliwa.

Dk. Shein ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais katika serikali ya awamu ya tatu, alisema baadaye watu hao walimpa kitabu chenye maoni yao na utetezi wa ajenda wanayoikusudia, lakini aliwaambia kuwa mawazo hayo ni yao na wanapaswa kwenda kuyasema wenyewe.

Akizungumza huku akionyesha kuchukizwa na kamati hiyo, Dk. Shein alisema serikali ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), haina mawazo wala msimamo bali inachokingoja ni mawazo ya wananchi wenyewe kwa vile katiba ni chombo cha umma ndiyo wenye maamuzi kuhusu Muungano wanaoutaka.

Alisema kwa bahati mbaya kamati hiyo ilianza kubeba jukumu la kuwasemea Wazanzibari kuhusu msimamo katika Muungano na kuwataka wakubali mfumo wanaoutaka wao na kusababisha mgawanyiko miongoni mwa wananchi.

“ Wasiniingize mimi katika mpango wao wala wasitake kufika waendako kwa kutumia mabega yangu, wamelipika sasa waacheni walinywe wenyewe,”alisema Dk Shein huku akishangiliwa na wanaCCM.

Alisema yeye amewahi kufanya kazi na kushika nyadhifa za juu katika serikali ya Mungano akimsaidia Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na awamu ya nne, Jakaya Kikwete, hivyo hawezi kuwasaliti na kuwazunguka viongozi wenzake.

 “Sitamuogopa mtu yeyote atakaechezea amani ya nchi yetu, hakuna utani katika uongozi wa nchi na amani ya watu wake, tunafanya maamuzi ya pamoja kupitia Baraza la Mapinduzi, asiyeweza aninong’oneze kuwa ameshindwa kunisaidia, mwenye mushkel asisite kuniambia,”alisisitiza Dk. Shein.

Mkutano huo wa vunja jungu kabla ya kuingia kwa mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani pia ulihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Rais mstaafu wa awamu ya tano Zanzibar Dk. Salmin Amour, Mke wa rais wa kwanza Fatma Karume, mwanasiasa mkongwe  Abdulrazaq Simai Kwacha na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Ameir Mohamed, ambaye aliposimama kusalimia wananchi alikumbusha haja ya kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Kamati ya maridhainao inayoongozwa na Waziri wa zamani wa  SMZ, Mzee Hassan Nassor Moyo, inalenga kutetea Zanzibar kupata mamlaka kamili na kiti Umoja wa Mataifa na kuungwa mkono harakati za Jumuiya  ya Uamsho na mihadhara ya Kiislam wanaotetea Zanzibar ijitenge katika Muungano.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakari, Waziri wa zamani wa Kilimo na Maliasili, Masour Yussuf Himid, Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, Mkurugenzi wa Uenezi na Mwalisilianio ya Umma wa CUF, Salum Biman na mjasiriamali, Eddy Riyami.

CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top