Jeshi la Polisi nchini limemtia mbaroni mtu mmoja mjini Mbeya anayedaiwa
kuhusika na vitendo vya ugaidi akiwa na hati mbili za kusafiria, na mwingine
Mtanzania adakwa akidaiwa kusaidiana naye.
Mtu huyo aliyekamatwa wilayani Kyela, pia
anatuhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi nchini Uingereza.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar
es Salaam, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, alisema
mtuhumiwa huyo alikuwa anatumia majina mawili tofauti kwenye hati za kusafiria
na alikuwa akijaribu kuvuka mpaka wa Tanzania kuelekea Malawi.
Alisema mtuhumiwa huyo alitumia hati ya Tanzania
yenye namba AB 651926 yenye jina la Adil Ally Patel na hati ya Uingereza
yenye namba NO 51555382 yenye jina la Iqbal Hassan Ally.
Manumba alisema hati ya Tanzania aliyokamatwa nayo
ni kati ya hati 26 zilizoibiwa kwenye Ofisi za Uhamiaji mwaka mmoja
uliopita.
Alisema
mshukiwa wa ugaidi alikuwa akisaidiwa na Mtanzania mmoja ambaye hakumtaja jina
na baada ya kukaguliwa kompyuta mpakato (laptop) yake ilikuwa na maneno ya
uchochezi ya kidini kuhusu imani tofauti.
Manumba alisema aliwasiliana na Serikali ya
Uingereza kuhusu hati ya mtuhumiwa huyo na kuelezwa kuwa ni halali na
kufahamishwa kuwa mtu huyo wanamtafuta kwa tukio la ugaidi nchini
Uingereza.
Alisema kuna Mtanzania
mwingine ambaye hakumtaja jina, alikamatwa kwa kuhisiwa kujihusisha na mtuhumiwa
huyo wa ugaidi ambaye baada ya kukaguliwa pia alikutwa na kompyuta yenye maneno
ya uchochezi dhidi ya dini isiyomhusu.
Alisema mtuhumiwa huyo alijitambulisa kuwa ni
mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kimoja kilichopo nchini Sudan.
Manumba aliwataka wazazi kuwa waangalifu na
vijana wao wanaokwenda kusoma nje ya nchi kwa kuwa baadhi yao hurubuniwa na
kujiingiza katika mambo yanayohusiana na ugaidi.
Aliongeza kuwa polisi wana uhakika kwamba kuna
baadhi ya vikundi vya kigaidi ndani ya nchi ambavyo vina mipango ya siri ya
kutekeleza ugadi nchini.
Aliwataka
Watanzania kuwa waangalifu wakati polisi ikifanya kazi yake ya uchunguzi na
kuonyesha kuwa hali ya usalama si nzuri nchini kutokana na matukio ya kihalifu
yanayoendelea.
Aidha, alisema polisi
inaendelea na uchunguzi dhidi ya matukio ya mlipuko miwili ya mabomu iliyotokea
mkoani Arusha na lile la kuuawa kwa Padri Evarist Mushi, Zanzibar.
Alisema
matukio hayo yameonyesha sura mbaya kwa Tanzania ya kuwepo kwa tishio la
ugaidi.
Alisema uchunguzi
utakapokamilika washitakiwa watafikishwa kwemnye mikono ya sheria kuhukumiwa kwa
makosa ya jinai.
Aliongeza kuwa
taarifa zitakazokuwa zikitolewa na raia wema zitasaidia polisi kurahisisha
uchunguzi na kuwakamata wahusika kwa wakati.
Manumba ametahadharisha kuwa ongezeko la uhalifu
nchini limekuwa likihusisha baadhi ya wananchi kutumika vibaya na wavunjifu wa
amani.
Alisema kufuatia matukio hayo,
baadhi ya watuhumiwa wanashikiliwa na baada ya uchunguzi kukamilika hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao.
“Hii ni sifa
mbaya Watanzania wanapaswa kujiepusha na vishawishi vya aina yoyote
vitakavyopelekea kuvunjika kwa amani iliyopo tangu kupatikana kwa uhuru wa
Tanzania,” alisema.
Katika matukio ya
kigaidi yaliyotokea siku za hivi karibuni watu watatu walikufa na zaidi ya 70
kujeruhiwa baada ya kurushwa bomu kanisani na mtu asiyefahamika katika kanisa la
Katoliki Jimbo Kuu la Arusha wakiwa wamejumuika katika uzinduzi wa Kanisa la
Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti.
Katika tukio jingine jijini humo, bomu lilipuka
kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) eneo la Soweto
kata ya Kaloleni mkoani Arusha.
Katika tukio hilo watu watatu walifariki
dunia kutokana na mlipuko wa bomu wakati chama hicho kikiwa kwenye mkutano wa
kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani.
Wakati huo huo Manumba alisema polisi jijini Dar es
Salaam limekamata meno ya tembo 347 katika eneo la Kimara ambayo yanaamika
yamepatikana kwa njia za kijangili katika mbuga za Tanzania.
Alisema mbali na nyara hizo, kuna meno mengine ya
tembo 788 yalikamatwa nchini Malawi katika mji wa Mzuzu na kwamba inaamika kuwa
yalisafirishwa kutoka Tanzania kama mzigo wa saruji kutoka katika kiwanda cha
Saruji Mbeya.
Manumba alisema polisi
nchini wanafanyakazi kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa kuhakikisha kuwa
ukweli wa matukio yanakuwa wazi na uchunguzi ukikamilika wahusika watafikishwa
katika vyombo vya sheria.
Loading...
Post a Comment