Loading...
Home »
Unlabelled »
JIKO LA MAFUTA LAUA WATU WANNE WA FAMILIA MOJA HUKO ILEMELA JIJINI MWANZA...!!
WATU wanne wa familia moja, wamefariki dunia na mmoja
kujeruhiwa baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi, kuteketea kwa moto alfajiri ya
jana. Ajali hiyo ilitokea eneo la Lumala Mashariki wilayani Ilemela na ilitokana
na jiko la mafuta, ambalo halikuzimwa baada ya wanafamilia hao kula daku usiku;
matokeo yake, lililipuka alfajiri.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest
Mangu, ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na pikipiki iliyokuwa na mafuta ya petroli,
ambayo ilishika moto na kuungua na kuteketeza watu waliokuwa ndani pamoja na
nyumba.
Waliokufa ndani ya nyumba hiyo, mali ya Fadhil Nuru, ni
Amina Musa (75) na Mariam Musa (72) ambao ni mtu na dada
yake.
Wengine ni Busharat Bashir (23) na Janat Abdul mwenye
umri wa miezi sita, ambao ni mtu na mwanawe. Majeruhi, Dotto Twaa mwenye umri wa
kati ya miaka 17 na 18, amejeruhiwa vibaya usoni, mkononi na kifuani na amelazwa
katika Hospitali ya Rufaa Bugando.
Taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu hao, zinasema
Mariam alikwenda kumtembelea dada yake huyo, Amina, aliyekuwa akiishi kwa
mwanawe. Busharati na mwanawe, Janat, waliokuwa wakikaa Kirumba, walikwenda
nyumbani hapo eneo la Lumala, kumtembelea baba yao mdogo na kuwaona bibi zao
hao, ambao pia ni marehemu.
“Baba ambaye ni mkuu wa
familia, amenusurika. Yeye alikuwa amelala nyumba ya mbele. Hawa waliokufa na
huyo majeruhi, walikuwa wamelala nyumba ya nyuma,” alisema mmoja wa
wanafamilia, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini. Kamanda
alisema,
“Timu ya polisi bado ipo eneo la tukio wakiendelea
kufuatilia ili kujua kama kuna majeruhi wowote waliokimbizwa kwenye zahanati na
vituo vya afya ili tuweze kuwatambua”.
Mangu alisema atatoa taarifa zaidi leo timu
itakapomaliza kazi. Mangu alisema miili ya marehemu, ilihifadhiwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Hata hivyo, maziko yalifanyika
jana.
Akizungumza katika eneo la tukio, mmiliki wa nyumba
hiyo, Fadhil Nuru alisema moto ulioteketeza familia yake, ulizimwa na wananchi
waliojitokeza kuwasaidia.
Alisema walipiga simu mapema Zimamoto, lakini
walichelewa kufika na kukuta tayari majirani wamezima.
“Kama Zimamoto wangewahi
kufika kusingekuwa na madhara makubwa ya kupoteza wanafamilia wengi namna hii,
hata hivyo nawashukuru wananchi kwa kunisaidia,”
alisema.
SOURCE: HABARI LEO
on Friday, July 12, 2013
Post a Comment