*Rasimu kutumika kuwaondolea sifa ya kugombea urais
*Yumo pia Membe, Magufuli, Sitta, Zitto na Wassira
MKAKATI wa kuwaengua vigogo wanaotajwa kung’ang’ania kugombea nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 sasa umebainika, MTANZANIA Jumapili linaripoti.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili, mkakati huo ambao umelenga kuwang’oa viongozi hao, unadaiwa kutekelezwa na baadhi ya wanasiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Rasimu ya Katiba Mpya, iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Imeelezwa kuwa kupitia Rasimu hiyo ya Katiba Mpya, kuna vipengele vilivyopenyezwa kwa nia ya kuwabana watu fulani fulani ndani na nje ya CCM ambao wanatajwa kuusaka ukuu wa dola mwaka 2015 na chama hicho hakitaki kuona wanakuwa kikwazo dhidi yake.
Mtoa habari wetu ndani ya CCM alilidokeza gazeti hili kuwa vipengele hivyo ambavyo vimewekwa kama mtego, ni vile vinavyotaja sifa za mgombea Urais na mgombea Ubunge.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, kutokana na hilo, baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM kwa makusudi wameamua kuufanya mjadala kuhusu serikali tatu kuwa mkali, ili kuzuia mjadala mpana katika masuala mengine.
Kipengele ambacho kama kikiachwa bila kufanyiwa marekebisho kinaweza kuwabana wanasiasa wengi ndani na nje ya CCM wanaotajwa kuwania Urais 2015 ni pamoja na kile cha Sura ya Saba, ambacho kinazungumzia Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu Serikali, Rais na Makamu wa Rais, katika sehemu ya kwanza C kwenye kipengele cha 75 (E) kinachozungumzia sifa za Rais kimeeleza kuwa mtu atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kushika nafasi ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa: anazo sifa za kumwezesha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba hiyo.
Wakati ikiwa hivyo katika sifa za kuwania nafasi ya Rais, kwenye Rasimu hiyohiyo kipengele cha sifa za kuwania nafasi ya Ubunge kilichopo katika sura ya tisa, sehemu ya pili (A) inayozungumzia kuhusu uchaguzi wa wabunge, katika kipengele cha (2a) kimeeleza kuwa mtu hatakuwa na sifa za kugombea/ kuchaguliwa kuwa Mbunge ikiwa mtu huyo aliwahi kuwa Mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano.
Kutokana na hilo, ni wazi kuwa viongozi au vigogo waliowahi kuwa wabunge kwa vipindi zaidi ya vitatu vya miaka mitano hawatakuwa na sifa za kugombea Urais kwa sababu tayari kipengele cha sifa za kuwania Urais kimetaja kuzingatia sifa za mgombea ubunge.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa vigogo karibu wote ndani na nje ya CCM wanaotajwa kutaka kuwania nafasi ya Urais watakuwa wamepoteza sifa za kuwania nafasi hiyo endapo kipengele hicho kitaachwa bila kufanyiwa mabadiliko.
Vigogo hao wanaotajwa kutoka CCM ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, wakati kutoka Chadema ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbroad Slaa na Zitto Kabwe.
MTANZANIA JUMAPILI
Loading...
Post a Comment