Na Hassan Hamad
OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim
Seif Sharif Hamad amesema matarajio ya wananchi kuhusu mchakato wa mabadiliko ya
katiba ni kuona unaondoa vikwazo vya utafutaji na matumizi ya rasilimali asili
zikiwemo mafuta na gesi.
Makamu wa Kwanza
wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Naibu Waziri wa
Uingereza anayehusika na Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds,
alipofika nyumbani kwake Mbweni kwa mazungumzo
Maalim Seif ameeleza hayo nyumbani kwake mbweni
alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Uingereza ulioongozwa na Naibu Waziri
anayehusika na Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds ambapo pamoja na
mambo mengine walizungumzi juu mchakato wa katiba na maendeleo ya utafutaji na
uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Amesema wakati Zanzibar imeshaamua kuliondoa
suala hilo katika orodha ya mambo ya Muungano, bado inasubiri taratibu za
kisheria ambazo zinaweza kupatikana baada ya kukamilika kwa mchakato wa
katiba.
Amesema mara baada ya kukamilika kwa mchakato
huo na suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika mambo ya Muungano,
Zanzibar itatangaza zabuni za uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ambapo
makampuni mbali mbali yataruhusiwa kuomba zabuni hizo, na hatimaye kuanza rasmi
kwa kazi ya uchimbaji.
Makamu wa Kwanza
wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Naibu Waziri wa
Uingereza anayehusika na Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds,
nyumbani kwake Mbweni.
Amefahamisha kuwa mchakato wa katiba umefikia
hatua nzuri baada ya kuanza kwa mabaraza ya katiba tarehe 12/07/2013, ambayo
itafuatiwa na bunge la katiba na baadaye wananchi wataamua katiba hiyo kupitia
kura ya maoni.
Kuhusu nishati ya umeme ambapo Uingereza ni
mshirika wa karibu wa nishati hiyo nchini, Maalim Seif amesema Zanzibar imo
katika mchakato wa kutafuta nishati mbadala itokanayo na jua pamoja na upepo,
ambapo tayari imeonesha mwelekeo mzuri.
Amesema nishati hiyo itakapopatikana itaondosha
usumbufu unaojitokeza mara kwa mara na kupunguza utegemezi wa upatikanaji wa
umeme kutoka Tanzania Bara, sambamba na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Aidha Maalim Seif ameelezea mazingira ya
uwekezaji Zanzibar, na kuuomba ujumbe huo kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza
hasa katika sekta za utalii na uvuvi wa bahari kuu.
Amesema Zanzibar ambayo kwa sasa imetoa
kipaumbelele katika sekta ya utalii, inakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa
hoteli za nyota tano katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Ameongeza kuwa Zanzibar pia ina mpango wa
kujenga bandari ya kibiashara katika eneo la mpigaduni, pamoja kuvifanyia
matengenezo makubwa viwanja vya ndege, ili kuweka mazingira bora zaidi ya
uwekezaji.
Nae bw. Simmonds amesema Uingereza itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo nishati.
Ameahidi kuwasiliana na makampuni ya utalii,
uvuvi na ujenzi ili kuangalia uwezekeno wa kuja kuwekeza Zanzibar katika maeneo
mbali mbali nchini.
Chanzo - ZanziNews
Post a Comment