Wekundu wa Msimbazi Simba “Taifa kubwa” wanatarajia kufanya mkutano mkuu wa wanachama Agosti 20 mwaka huu jijini Dar es salaam ili kujadili mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo ya klabu hiyo.
Mwenyekiti wa klabu ya Simba ambaye ni mbunge wa Tabora mjini, Alhaji Ismail Aden Rage amesema kwa kawaida mkutano huo ulitakiwa kufanyika Agosti 5 kwani mwaka jana ulifanyika tarehe hiyo, lakini wamelazimika kusogeza mpaka tarehe tajwa ili kuepukana na mwezi mtukufu wa Ramadhan.
“Tumeamua kusogeza mbele mkutano mkuu wa wanachama wa klabu ya Simba, lengo letu ni kuepukana na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, lakini pia kufika muda huo uongozi utakuwa umekamilisha baadhi ya mambo”. Alisema Rage.
Rage alisema katika mkutano wa mwaka huu kutakuwa na ajenda mbalimbali ambazo zitajadiliwa na wanachama halali wa klabu hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema ajenda ya kwanza itakuwa ni kujadili taarifa ya ukaguzi wa fedha za klabu, na baada ya kujadiliwa kwa ajenda hiyo, watajadili ya pili ambayo ni mipango endelevu ya klabu hiyo.
Rage aliendelea kueleza kuwa ajenda ya tatu ni Taarifa ya klabu itakayosomwa na katibu mkuu Evodius Mtawala, baada ya hapo wanachama watachangia, huku hotuba ya mwenyekiti ikifuatia na hatimaye kufungwa kwa mkutano huo.
“Cha msingi ni kuwa wanachama watakaohusika katika mkutano huo ni wale hai tu waliolipa ada ya uanachama kupitia benki. Kama mtu anafikiri ni utani basi ajitokeze siku hiyo wakati si mwanachama hai”. Alisema Rage.
Rage aliwataka wanachama wa Simba kujiandaa na mkutano huo ambao utakuwa chachu ya mafanikio ya klabu yao ikiwemo kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao.
“Sisi Simba tumejipanga sana, tunataka kuiboresha timu yetu katika Nyanja zote, Agosti 20 wanachama wote wanatakiwa kufika katika mkutano ili kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya kuijenga timu yao kwa kuchangia mawazo yao”. Alisema Rage.
Ili kufanikisha mkutano huo, leo hii wadhamini wakuu wa klabu hiyo, Kampuni ya bia ya TBL kupitia kinywaji chake cha bia ya Kilimanjaro, wamekabidhi shilingi milioni 20 kwa uongozi wa Simba ikiwa ni sehemu ya udhamini wao.
Akiongea wakati wa makabidhiano hayo, meneja wa TBL, George Kavishe alisema wao wanajipanga kuendeleza klabu ya Simba chini ya mwavuli wa udhamini wao, hivyo wanawatakia mkutano mwema wekundu hao wa Msimbazi Simba wenye makazi yao mitaa ya Msimbazi Kariakoo jijini Dar es salaam
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Post a Comment