Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Uchaguzi wa Madiwani: Hofu yazidi kutanda jijini Arusha


 

uchaguzi_chadema_ccmHofu ya vurugu imetanda mkoani Arusha, .
Tayari wazee wa kimila kutoka maeneo tofauti ya Arusha, wamekutana na kutoa wito wa kuwapo amani na pande husika kutokuwa chanzo cha vurugu.
Baraza Kuu la viongozi wa mila wa Kimasai (Marya), limetoa maazimio 10, likisema limechoshwa na kusikitishwa na vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu jijini humo.
Katibu wa Marya, Amani Lekisalie Lukumay, akisoma tamko hilo jana mbele ya viongozi wa mila (malaigwanani) kutoka mikoa ya Arusha na Manyara, alisema hakuna haja ya kuwapo umwagaji damu mkoani humo.
“Hatuhitaji kuona damu ikimwagika tena katika maeneo yote ya watu wa maa (wenyeji wa kabila la Wamasai), wakiendelea itatulazimu kuchukua njia muafaka ya kurejesha amani na utulivu na kutomwagika damu tena,” alisema.


Alisema wanatoa wito kwa mahakama kuharakisha kusikiliza na kuamua kesi za watuhumiwa wa uvunjifu wa amani, kutokana na maandamano na mikutano iliyofanyika kati ya mwaka 2010 hadi 2013.
Mkutano huo wa malaigwanani kutoka mikoa ya Arusha na Manyara uliofanyika kwenye ‘makazi’ yao ya kimila yaliyopo katika Chuo cha Ufundi Arusha, ambapo pia ulimjumuisha pia Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye.
Kabla ya kusoma tamko hilo, baadhi ya malaigwanani walikuwa wakizungumzia masuala mbalimbali yanayowahusu, hususan, ya kisiasa, uongozi, amani na utulivu katika jiji la Arusha.
Hata hivyo, baadhi yao wakizungumza baada ya mkutano huo, walipingana na wazee hao kuhusu suala la wageni wanaoishi jijini hapa wakidaiwa kuwa ndio wanaosababisha vurugu.
Walidai kuwa mazungumzo ya viongozi hao na maazimio waliyoyatoa yalikuwa na mwelekeo wa kisiasa na ukabila, jambo ambalo ni hatari.
Walisema kwa mfano, madai kuwa baadhi vurugu zinazotokea jijini hapa zinachangiwa na maandamano yanayofanywa na vyama vya siasa, ni mwelekeo wa kuingilia shughuli za upigaji kura zinazotarajiwa kufanyika kesho.
“Tunatoa tamko kwa viongozi wote wa vyama vya siasa, asasi za kiraia na taasisi zote za jamii au kundi lolote lenye nia ya kuvuruga amani katika jiji letu la Arusha waache kufanya hivyo kabisa,” alisema Lukumay.
Alisema wanaunga mkono jitihada na hatua zote zinazochukuliwa na serikali kukomesha vitendo vya hujuma kwa maendeleo na ustawi wa taifa na wataendelea kushirikiana na viongozi na watendaji kukomesha vitendo hivyo.
Alisema wao kama viongozi wa mila wana wajibu wa kulinda usalama na utulivu katika jiji la Arusha kama ambavyo katiba ya nchi inavyoelekeza.
“Wageni, wakazi na washirika wote kwa ujumla wao katika jiji letu waonyeshe ushirikiano na watusaidie kulinda na kuendeleza umoja, upendo, mshikamano, amani na siyo kuwa chanzo cha matatizo kwani hatutakubali kabisa.”
“Tunatoa tamko kwa viongozi wote wa vyama vya siasa, asasi za kiraia na taasisi zote za jamii au kundi lolote lenye nia ya kuvuruga amani katika jiji letu la Arusha waache kufanya hivyo kabisa,” alisema.
Waliiomba serikali kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana jamii ili kuepusha hasara ya uhai wa watu na mali inayotokana na vitendo viovu vya watu wenye hila na ustawi na maendeleo ya jiji la Arusha na Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kusomwa kwa tamko hilo, Mwenyekiti wa Maarya, Langidare ole Menavi, alisema wamefanya mkutano huo kutokana na damu inayomwagika jijini hapa.
Alisema tangu kupata Uhuru hapakuwepo na hali kama hiyo, lakini imeanza kuibuka miaka miwili au mitatu iliyopita. Kikao kingine cha Marya kinatarajiwa kufanyika Julai 18, mwaka huu.
Wakati hali ikiwa hivyo, polisi mefanya msako wa nyumba hadi nyumba na kumkamata mgombea udiwani kupitia wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Rayson Ngowi.
Ngowi, anasadikiwa kuwekewa ulinzi na kikundi cha ulinzi cha Red Brigade kinachomilikiwa na Chadema.
Kesho, uchaguzi huo utafanyika katika kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi, ikiwa ni baada ya (uchaguzi huo) kuahirishwa Juni, 16 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na mabomu yaliyopigwa siku moja kabla ya siku ya uchaguzi iliyopangwa.
Liana, alisema maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika na taratibu za kuwatangaza wasimamizi, wasimamizi wasaidizi na makarani zimekamilika.
Mafunzo kwa ajili ya wasimamizi hao yameanza juzi na yanatarajia kukamilika leo.

Aliwataja wanachama walioteuliwa kugombea nafasi za udiwani katika kata ya Elerah kuwa ni Emmanuel Laizer (CCM),Gilbert Bayo (CUF), Seif Shimba (CCK), Jeremiah Mpiga (Chadema), Boidafi Shirima (TLP).
Wagombea katika kata Kaloleni ni Emmanuel Miliari (CCM), Darwesh Ramathani (CUF), Kessy Lewi (Chadema) na Ngilisho Pauli (Demokrasia Makini).
Kata ya Themi ni Victoro Mkolwe (CCM), Kinabo Edmound (Chadema) na Lobora Ndaproi (CUF) .

Aliwataja wagombea kutoka kata ya Kimandoku kuwa ni Edna Saul (CCM) na Rayson Ngowi (Chadema).
Alisema vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kupigia kura ni 136 ambapo Kaloleni ina vituo 27, Elerahi (55), Kimandolu (39) na kata ya Themi (15).
Liana, alisema kuwa jumla ya wapiga kura 60,123 wamejiandikisha katika zoezi hilo.

Aliwataka wananchi kutimiza wajibu wao wa kupiga kura, kwani zoezi hilo ni muhimu huku akiwahakikishia kuwa usalama utakuwa imara wakati wa kupiga kura.
Aliwataka wananchi watakaosumbuliwa katika eneo la kupigia kura, watoe taarifa kwa askari ili achukuliwe hatua za kisheria.
MGOMBEA UDIWANI CHADEMA AKAMATWA
Katibu Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema kuwa wameshangazwa kuona polisi wanamkamata mgombea wao, Rayson
Ngowi saa saba usiku, akiwa nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa Golugwa, mgombea huyo alikuwa amelala, akilindwa na walinzi wa red brigade ambao walishindwa kumlinda baada ya polisi kuvamia na kumkamata, kisha kumpeleka kituo kikuu cha polisi.
“Lakini hawa polisi walipogundua wamekamata mgombea, waliamua kumwachia asubuhi jana (juzi), ili kukwepa lawama, ila mgombea alipotaka kuondoka na walinzi wake, polisi walikataa kuwaachia na kumruhusu aondoke peke yake,”alisema Golugwa.
Kwa mujibu wa Nipashe ilipowasiliana na Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, kuzungumzia tukio hilo, aliomba atafutwe baadaye na alipopigiwa kwa mara ya pili alijibu kuwa hawezi kuzungumzia chochote kwa sababu yuko katika harakati za kumpokea Rais Jakaya Kikwete.
*Habari hii imeandikwa na Woinde Shizza, Cynthia Mwilolezi na John Ngunge, Arusha
CHANZO: NIPASHE
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top