CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimekataa kuhudhuria mkutano wa siku mbili wa kujadili amani ya nchi,
ulioitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa madai kuwa hauna tija kwa
taifa.
Chama hicho kimetaka fedha zitakazotumika
katika mkutano huo unaofanyika katika Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam
zielekezwe katika shughuli za kimaendeleo, ambazo zitakuwa na tija kwa wananchi
wengi.
Msimamo huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam
na Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benson Kigaila, wakati akizungumza na
waandishi wa habari, ambapo alisema wamesusia mkutano huo kwa sababu waandaaji
wamewaalika wanasiasa pekee, wakati suala la amani halishikiliwi na wanasiasa
pekee.
Kigaila alisema CHADEMA inaamini jukumu la
kulinda amani linashikiliwa na makundi mbalimbali ya kijamii, hivyo wanapaswa
kushirikishwa katika mkutano huo.
“Kikubwa ni kwamba Mwenyekiti wa TCD, James
Mbatia, amekiuka maazimio ya kikao ya kuteua muwezeshaji wa mkutano huo na
badala yake akafungamana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuteua watu wanaowataka.
Pili, amani haijadiliwi… amani inatengenezwa na kuwapo mazingira ya haki na
usawa,” alisema Kigaila.
Alisema licha ya serikali inayoongozwa na CCM
kulalamikiwa kuwa nyuma ya mikakati ya kuvuruga amani na kutolea mfano kauli ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ya hivi karibuni kuwa wanaokaidi amri za vyombo vya
dola wapigwe bila kujali kuwa wanatetea haki zao za msingi.
“Tunafahamu amani si ya wanasiasa peke yake, ni
ya wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, taasisi za kiraia na zile zisizo
za kiserikali, hao hawakushirikishwa, sasa tunakwenda kujadili suala hili na
nani au wale wanaoamrisha wananchi wapigwe?” aliongeza.
Alisema kuwa mchakato huo hauendani na hali
halisi iliyopo sasa, ambapo serikali ndiyo inayolalamikiwa kutesa na kuwadhuru
baadhi ya watu huku ikishindwa kuunda tume huru ya kimahakama kufuatilia
mchakato huo.
Kigaila alisema kama CHADEMA ingekubali
kuhudhuria ni sawa na kufanya sherehe juu ya makaburi ya watu waliokufa katika
mikono ya serikali ya CCM, jambo ambalo CHADEMA haiwezi kulikubali.
Alisema kwa sasa kuna matukio ya kutatanisha
yakiwahusisha maofisa wa polisi, ikiwamo kuuawa kwa aliyekuwa mtangazaji wa
kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, mlipuko wa bomu Arusha,
kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.
Kigaila alisema matukio hayo yote licha ya
kuvihusisha vyombo vya dola mpaka sasa serikali imekaa kimya na inaendelea
kujificha katika mgongo wa vyama vya siasa.
Alibainisha kuwa wakati leo mkutano huo ukianza
jijini Da esSalaam, mkoani Mtwara kuna malalamiko ya wananchi kupigwa, kubakwa
na kuteswa na baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) bila
kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Matukio yote haya yanatuonyesha serikali haina
dhamira ya kutaka amani iendelee, imeamua kubagua watu wa kuhudhuria mkutano
huo…sisi hatukubaliani nayo,” alisema.
Kigaila alisema wana taarifa kuwa serikali
imefadhili mkutano huo utakaotumia sh milioni 400 kwa siku mbili na idadi ya
wajumbe watakaohudhuria ni watu 70.
TCD waijibu
Tanzania Daima, liliwasiliana na Mwenyekiti wa
TCD, James Mbatia, juu ya mkutano huo kufadhiliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
ambapo alikanusha mkutano huo kuandaliwa na serikali kwa mgongo wa TCD.
Mbatia alisema mkutano huo unafanyika kutokana
na maazimio ya vyama vyote vilivyokutana mjini Dodoma Februari 7, mwaka huu na
kukubaliana wafanye mkutano wa kuzungumzia masuala ya amani inayoonekana
kulegalega kwenye baadhi ya maeneo.
Aliongeza kuwa si kweli kuwa wameyatenga
makundi mengine, bali vikao hivyo vitakuwa vya mwendelezo wa makundi mbalimbali
na hivi sasa wameanza na wanasiasa.
Alisema mkutano huo unaoanza leo kutakuwa na
mada nne tofauti, ambazo ni amani na demokrasia, amani na usalama
itakayowasilishwa na IGP Mwema, nafasi ya vyombo vya habari katika kuenzi amani
itakayowasilishwa na Dk. Ayoub Ryoba, pamoja na uzoefu wa serikali ya umoja wa
kitaifa Zanzibar.
Chanzo - Tanzaia
Daima
Post a Comment