Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa onyo kwa
kikundi cha waasi nchini Kongo cha M23, kuwa kikiwachokoza lipo tayari kwa
vita.
Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa jeshi hilo, Kanali Kapambala
Mgawe, wakati akihojiwa na NIPASHE Jumamosi kutokana na tishio lililotolewa na
kikundi hicho kuvamia mji wa Goma endapo Serikali ya Kongo itajiondoa kwenye
mazungumzo ya amani.
Kanali Mgawe, alisema wanajeshi waliopiga kambi eneo
la Goma, wamejitayarisha kwa vita ya aina yoyote, na hawatasita kutoa kipigo
kikali baada ya kuona kikundi hicho cha M23 kinawashambulia.Wanajeshi wa Tanzania wapo nchini humo kuunda kikosi
maalum cha Umoja wa Mataifa ambacho kimepewa jukumu la kunyang'anya silaha waasi
pamoja na kulinda amani mashariki ya nchi hiyo.
Nchi zingine zilizopeleka
majeshi yao kuunda kikosi hicho ni Malawi na Afrika ya Kusini.
Hata
hivyo, kwa siku za hivi karibuni hali ya amani katika mji wa Goma imezidi
kuzorota, huku Mashirika ya habari ya Kimataifa yakieleza wanajeshi wa kikundi
hicho wapo karibu na mji huo na kuongeza hali ya wasiwasi kwa
wananchi.
"Jeshi lipo na hali nzuri, hatuna hofu na vitisho vya waasi
kwa sababu tumejiandaa kwa kila kitu, ni wazi waasi wakitushambulia watakuwa
wendawazimu, tutajibu kwa makali ya hali ya juu," alisema Kanali
Mgawe.
Alisema hawana sababu ya kuingilia vita hiyo kwa sasa kutokana na
utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuwapa kazi ya usuluhishi, kabla ya
kutumia nguvu kama wakiona haki ya kimsingi ya wananchi inakiukwa.
"Kuna
mambo kadhaa hatujakamilisha katika uundaji wa kikosi cha Umoja wa Mataifa,
lakini tumeanza kufanya kazi ya kuchunguza na kupata taarifa zinazoweza
kutusaidia tukianza kazi rasmi," aliongeza.
"Watanzania wasiwe na wasiwasi, vijana wetu wana mafunzo
na zana za kisasa za kuwafanya kuwakabili waasi ambao wengi wameokotwa mitaani
na hawana mbinu za kivita."
Alisema, hali ya mji huo ipo
tulivu, ingawa katika siku za hivi karibuni waasi wa kikundi cha Maimai
walivamia gereza moja na kuwatorosha wafungwa ili kuwalazimisha kujiunga na
kikundi hicho.
Read more: http://talkbongo.blogspot.com/2013/07/waasi-wa-m23-wakitaka-vita-sisi-tupo.html#ixzz2YIA0B4j8
Loading...
Post a Comment