Harare. Siku moja baada ya kutangazwa rasmi kwamba aliyekuwa
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amestaafu kwa mujibu wa
sheria, amejitokeza na kueleza yaliyo moyoni mwake.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini
Harare jana, Tendwa alisema amepokea kwa mikono miwili kustaafu kutoka
katika nafasi hiyo nyeti katika siasa za Tanzania, huku akisema anajiona
mwenye bahati kufanya kazi na marais wawili katika nafasi yake.
Tendwa amefanya kazi chini ya uongozi wa Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa na baadaye Rais Jakaya Kikwete. Nafasi ya Tendwa,
imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi ambaye alikuwa jaji wa Mahakama
Kuu Kanda ya Dodoma.
Akizungumzia kuhusu viongozi wa vyama vya upinzani
kupokea kwa nderemo kustaafu kwake, Tendwa alisema wala hashangai
kuyasikia hayo kwani inaonyesha kwamba kazi yake alikuwa akiifanya vyema
na mujibu wa sheria.
“Unajua unapokuwa msajili na ukaona wadau wote
wanakushangilia hapo ujue kuna tatizo kubwa, nimekuwa ninafanya kazi
yangu vizuri sana kwa kuzingatia misingi ya sheria ambayo imewekwa kwa
mujibu wa sheria na kanuni,”alisema Tendwa.
Alisema kwamba, “Unajua kuvilea vyama ni kazi
kubwa sana ndugu yangu, maana kuna wakati hata Chama Cha Mapinduzi (CCM)
walikuwa wanasema ninaegemea na kuvipendelea sana vyama vya upinzani.
Leo nimestaafu nasikia vyama vya upinzani vinasema kwamba nilikuwa
nawapendelea CCM, hiyo inaonyesha kwamba nilikuwa ninafanya kazi yangu
sawa sawa.”
Kitu gani ambacho Tendwa hatakisahau?
Alisema kwamba katika miaka yake 13 ambayo amekuwa msajili hatomsahau waziri mmoja wa CCM.
Hata hivyo, Mwananchi lilimbana kumtaja waziri
huyo, lakini agoma kwa madai kwamba hapendi kuendeleza malumbano naye
baada ya kustafu kwake utumishi wa umma.
Tendwa alisema katika utumishi wake, waziri huyo alikuwa akimpatia wakati mgumu sana kwa kumpakazia kwamba yeye ni mpinzani.
“Katika miaka yangu 13 ofisini sitaweza kumsahau
huyo waziri maana alikuwa ananipakazia kwamba mimi ni mfuasi wa vyama
vya upinzani. Ninamshukuru Mungu kwamba baadaye alikuja kuniomba
msamaha, lakini ilikuwa imenisumbua sana katika kazi zangu,” alisema
huku akionyesha masikitiko MWANANCHI
Post a Comment