Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansoor Yussuf Himid |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimemeguka
baada ya Kamati Maalumu kumvua uanachama Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansoor
Yussuf Himid, akidaiwa kukiuka maadili ya chama hicho. Uamuzi huo umekuja baada
ya Mansoor kudaiwa kupingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010,
inayoamini katika muundo wa Serikali mbili.
Chanzo cha kuaminika kutoka katika kamati hiyo,
kiliiambia MTANZANIA jana kuwa uamuzi wa kumvua uanachama Mansoor uliwasilishwa
katika kikao kilichofanyika CCM Kisiwandui chini ya Makamu Mwenyekiti wake
ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansoor
zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi
Agosti 16, 2013 katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambapo wajumbe wa kamati hiyo kwa
kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama mwakilishi huyo.
Dk. Shein ndiye aliyeongoza kikao cha Kamati ya
Maadili, huku wajumbe wakiwa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali
Vuai, Mohamed Hija, Mbaruk Rashid Omari na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif
Ali Idd.
Chanzo hicho kutoka ndani ya CCM Zanzibar,
kilisema tuhuma za Mansoor zilizowasilishwa zilikuwa tatu, huku ya kwanza ikiwa
ni kushindwa kusimamia malengo, madhumuni na masharti ya chama.
Aidha, Mansoor anadaiwa kutokusimamia wajibu wa
mwanachama kwa kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM, kwa kukiuka Ilani ya chama
hicho ya mwaka 2010.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa suala la kufukuzwa
uanachama kwa mwakilishi huyo lilizua mjadala mzito katika kikao cha jana,
lakini baadaye wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kufukuzwa kwake.
Mansoor amekuwa miongoni mwa Wazanzibari walio
katika safu ya mbele kutetea muundo wa Muungano utakaoipa Zanzibar mamlaka
kamili ya dola.
Chanzo hicho kilizidi kusema kuwa suala la
mwakilishi huyo kutakiwa kuwasilisha utetezi dhidi ya tuhuma zake, lilianzia
katika kikao cha CCM Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo alisema kama kufungwa
afungwe lakini atasimamia Muungano wa mkataba pamoja na mamlaka kamili.
“Katika kikao cha mkoa alitoa utetezi wake na
kusema kama kufungwa afungwe, kama kunyongwa anyongwe na kama kufukuzwa
afukuzwe, lakini anataka Serikali ya mkataba.
“Wakati anatoa utetezi wake, Mansoor, alikuwa
anatumia nakala moja ya gazeti la wiki la Julai 26, mwaka huu na kumtuhumu
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, kuwa naye anavunja Katiba ya
CCM,” kilisema chanzo hicho.
Kutokana na misimamo yake, Mansoor, anaaminika
zaidi kwa Wazanzibari hususani wale wanaoamini katika Muungano wa mkataba pamoja
na madaraka kamili ya dola ya Zanzibar.
MTANZANIA ilipomtafuta Msemaji wa CCM upande wa
Zanzibar, Waride Bakari Jabu, atoe ufafanuzi wa suala hilo, alisema yupo katika
kikao.
“Kwa sasa siwezi kusema jambo lolote mwanangu,
nafikiri unasikia sauti za wajumbe wakizungumza, nipo katika kikao na siwezi
kusema jambo lolote kwa sasa,” alijibu kwa kifupi Waride.
Historia yake
Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Mansoor,
alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki kupitia CCM, nafasi ambayo amedumu
nayo hadi sasa.
Pia ni mwanachama wa CCM aliyewahi kuwa mjumbe
wa Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na Mweka Hazina wa CCM upande wa
Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2012.
Nje ya CCM, ameshika nyadhifa mbalimbali za
uwaziri katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ).
Mwaka 2000 hadi mwaka 2004, alikuwa Naibu
Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, na kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2010
alikuwa waziri kamili katika wizara hiyo na baadaye mwaka 2010 hadi mwaka 2012,
alikuwa Waziri wa Kilimo na Rasilimali.
Aidha, alihudumu kama mjumbe wa Baraza la
Biashara la Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi 2012.
Kutokana na misimamo yake ndani na nje ya chama
na Serikali, Oktoba 15, 2012, Dk. Shein ilimlazimu kufuta uteuzi wake kwa
Mansoor kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Mansoor ni mwanasiasa na mfanyabiashara
aliyezaliwa Novemba 3, 1967 kisiwani Unguja. Alisoma masomo yake ya msingi na
sekondari nchini India kati ya mwaka 1976 na 1987.
Kabla ya kuingia rasmi katika siasa mwaka 2000,
aliteuliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Wawakilishi na alijihusisha katika
biashara ya hoteli.
Mwanasiasa huyo ni mtoto wa Mkuu wa Kwanza wa
Jeshi la Zanzibar baada ya Mapinduzi, Brigedia Jenerali Yussuf Himid.
Amekuwa akisimamia maridhiano ya Wazanzibari na
Umoja wa Kitaifa akiwa mmoja wa wajumbe sita wa Kamati ya Maridhiano
aliyoshiriki kikamilifu kuyaanzisha mwaka 2009.
Pia ni miongoni mwa Wazanzibari walio mstari wa
mbele kutetea muundo wa Muungano, utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya
dola.
Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Mwenyekiti
Hassan Nassor Moyo (CCM), Eddie Riyami (CCM), Abubakar Khamis Bakari (CUF),
Ismail Jussa Ladhu (CUF) na Salim Bimani (CUF).
Chanzo - mtanzania.co.tz
Post a Comment