Msanii
wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) akiweka sahihi yake kuashiria
amekubaliana na taratibu zote alizoelekezwa na Bodi ya Filamu wakati wa
ukaguzi wa filamu yake ya “Foolish Age”.Katibu
Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo akiwaonyesha wajumbe
pamoja na wahusika wa Kampuni ya Proin Promotions baadhi ya maeneo
muhimu ya kufanyiwa marekebisho wakati walipowasilisha filamu yao ya
“Foolish Age” katika Bodi ya Filamu kwa ajili ya ukaguzi. Msanii
wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) akieleza jambo mbele ya Katibu
Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo wakati kampuni ya
Proin Promotions ikiwasilisha filamu yake ya “Foolish Age” kwa ajili ya
ukaguzi.
……………………………………………………………
Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
KAMPUNI ya Proin Promotions imewasilisha
filamu yake iliyopewa jina la “Foolish Age” kwa Bodi ya Filamu Tanzania kwa
ajili ya ukaguzi ambapo baada ya kufanyiwa marekebisho filamu hiyo
inaweza kuruhusiwa katika uzinduzi wa Kampuni hiyo hivi karibuni.
Bodi
ilifikia hatua ya kuwaita wahusika yaani Proin Promotions na Elizabeth
Michael (Lulu) kwa ajili ya kufanya majadiliano kuhusu maudhui na
maadili katika filamu hiyo kabla ya kufanyia maamuzi.
Katika
majadiliano hayo Bodi ya Filamu iliwakumbusha wahusika hao kufanya
baadhi ya marekebisho katika filamu hiyo ili iweze kuwa kivutio kwa
umma, pia Bodi ya Filamu iliwakumbusha juu ya umuhimu wa kuzingatia
kifungu cha 14 cha Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ambacho
kinaipa Bodi mamlaka ya kukagua filamu, matangazo na maelezo yote na
kile cha 24 (1) (d, n na t)
cha Kanuni za sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza kinachofafanua
mambo yanayotakiwa na yale yasiyotakiwa katika filamu ambayo filamu hiyo
imekwenda kinyume.
Kwa
upande wake Mwanasheria wa Kampuni ya Proin Promotions Bi. Gift Msuya
alikubaliana na ushauri uliotolewa na Bodi ya Filamu na aliiomba Bodi
itoe muda kwao kwa ajili ya kufanyia marekebisho katika filamu hiyo.
Naye
msanii Elizabeth Michael (Lulu) aliieleza Bodi ya Filamu kuwa Filamu
hiyo aliitengeneza muda mrefu na kwa sasa atazingatia maelekezo ya
sheria, Kanuni na taratibu hususani katika eneo la maadili. Aidha
alikiri kuwa ni kweli maeneo yaliyobainishwa kweli yanahitaji
marekebisho.
Katibu
Mtendaji Bodi ya Filamu Bi Fissoo alimalizia kwa kuishauri Kampuni hiyo
kutotumia filamu hiyo katika uzinduzi wa kampuni yao hadi hapo
watakapofanyia marekebisho katika baadhi ya maeneo muhimu ndani ya
filamu hiyo.
Proin
Promotions ni Kampuni inayojikita katika kuandaa na kutengeneza filamu
za kitanzania na kuzisambaza nchini, pia ni kampuni inayotarajiwa kutoa
ushindani mkubwa katika tasnia ya filamu. Kampuni hiyo inatarajiwa
kuzinduliwa hivi karibuni baada ya maandalizi rasmi kukamilika.
Post a Comment