Kamati
ya Hesabu za Serikali imekutana na Wizara ya Ardhi kwa madhumuni ya
kupitia Hesabu za Wizara kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2012.
Changamoto za Wizara ni nyingi sana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) amehoji mambo mengi sana na mengi ni wizi,
upotevu wa mapato ya Serikali na malalamiko ya wananchi kuhusu ardhi.
CAG alitoa hoja za ukaguzi maeneo ya mapato kutokusanywa, kulimbikizwa
na hata kukusanywa bila kuyawasilisha Wizarani.
Katika
Mwaka wa Fedha 2011/12 Wizara ilipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi
bilioni tisini na tisa (99 bilioni) lakini ilikusanya shilingi bilioni
ishirini tu (20 bilioni) sawa na asilimia 21 ya makadirio.
CAG
pia alihoji masuala ya viwanja vilivyopimwa, kugawiwa watu lakini watu
hawakupewa hati ambapo zaidi ya viwanja 7, 342 vilikutwa ni viwanja
vyenye shaka. Pia viwanja 160 jijini Dar es Salaam vyenye thamani ya
zaidi ya shilingi 555.8 milioni viligundulika ni viwanja ambavyo
walijigawiwa maafisa wa Ardhi maana haoakuwa na ushahidi wowote wa mauzo
ya viwanja hivyo. Hoja nyingine ni pamoja na ukiukaji wa sheria kwa
kujengwa kwenye fukwe nk.
Katika
Ripoti ya Hesabu za Serikali Kuu 2011/12 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali alipendekeza kuanzishwa kwa haraka mfumo fungamanifu
wa Taarifa za Ardhi, kutunza kumbukumbu kielektroniki na kuunganisha
kuanzisha utaratibu wa kwamba wakati wa kusajili hati ya ardhi
anayesajili kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN).
Baada
ya mjadala wa kina na kushauriana na wakaguzi na wataalamu Kamati ya
Hesabu za Serikali iliona kuwa kuna haja kubwa sana ya kufanya
mabadiliko makubwa kwenye mfumo mzima wa kutoa hati za kumiliki Ardhi.
Hivyo Uamuzi mkubwa
tuliochukua ni kuagiza kuwa hati zote za kumiliki ardhi zitolewe upya,
ziwe za dijitali na hati ziendane na namba ya Mlipa kodi (TIN).
Kamati
imeagiza kuwa Wizara kutoa majibu ya utekelezaji wa agizo hilo ifikapo
Mwezi Januari mwaka 2014. Tunaamini kuwa iwapo hati zote za ardhi
zitakuwa za dijitali, tutaondoa kabisa tatizo la hati mbili kwenye
kiwanja au shamba moja, itakuwa ni rahisi kwa usimamizi wa ardhi na
itaondoa mgogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Pia tunadhani pia itakuwa
rahisi kujua nani anamiliki ardhi kiasi gani, wapi nk.
Tunaamini
kuwa mfumo wa dijitali katika hati za ardhi utaongeza usalama zaidi kwa
wamiliki wadogo wa ardhi na kuondokana kabisa au kwa kiasi kikubwa na
hati za bandia ambazo zinaumiza zaidi wananchi masikini wanaotapeliwa
kila wakati. Ardhi yenye hati za kidijitali na zinazotunzwa
kielektroniki zitakuwa na thamani zaidi na zitawezesha mahitaji zaidi ya
hati hizo kwa shughuli mbalimbali za wananchi.
Mapato
yatokanayo na umiliki yatakusanywa kirahisi sana na kwa kuwa kila hati
itakuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) itakuwa ni njia
rahisi ya kuzuia ukwepaji kodi ya ardhi. Kwa kuwa kamati imeagiza
kuanza kutumika kwa risiti za elektroniki kwa malipo ya serikali,
tutaweza kupandisha mapato ya Serikali na hasa kwenye halmashauri za
wilaya na kuepukana na kodi sumbufu kwa wananchi.
Changamoto
kubwa ni kama matajiri wenye ardhi kubwa watakubali mageuzi haya kwani
hawapendi ijulikane kiwango cha ardhi wanachomiliki na pia itazuia
ukwepaji kodi na kupunguza rushwa kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi.
Mfumo
huu hata hivyo uwezeshe watu kuweza kutafuta kwenye mtandao hati, iwe
rahisi kutafanya utafutaji. Pia mfumo huu unaweza kusaidia sana suala la
fidia kwa wananchi wanaohamishwa kupisha uwekezaji mkubwa kama kwenye
sekta za madini na gesi asilia. Kwa mfano mwekezaji atapaswa kuhakikisha
hati za kijiditali zinapatikana kwa wananchi wanaohamishwa kupisha
mradi baada ya maridhiano ya wananchi hao kuhusu kupisha mradi na mahala
watakapohamia.
Kuna
haja pia hata hati za madini (mining rights) na leseni mbalimbali ziwe
za dijitali na kuhusishwa na TIN. Huko ndipo tunapaswa kuelekea.
Zitto Kabwe
MwenyeKiti PAC
Post a Comment