KAMATI ya pamoja ya kushugulikia masuala ya
muungano wa Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ) imefanikiwa kutatua hoja 10 kati 19.
Hoja zilizotatuliwa ni suala la ongezeko la
gharama za umeme kwa asilimia 21.7 kwa wateja wa Tanzania Bara na Zanzibar
asilimia 168 ambalo kamati hiyo imeafikiana na Shirika la Umeme nchini (TANESCO)
kufanyiwa marekebisho ya viwango vya bei.
Msemaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Siglinda
Chipungaupi, alisema juzi kuwa pamoja na kufanyiwa marekebisho ya bei pia deni
la Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco) litapatiwa ufumbuzi.
Hoja nyingine zilizotatuliwa ni utekelezaji wa
sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Zanzibar, sasa imefanyiwa
marekebisho kupitia sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali ‘Written Laws
Miscellaneous Amendments’ namba 8 ya mwaka 2006 ambapo sasa inafanya kazi sehemu
zote mbili.
Chipungaupi alisema pia hoja ya ushiriki wa
Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo iliwasilisha miradi ya
maendeleo ya kiuchumi kwa ajili ya kuijumuisha katika miradi ya kikanda
inayotekelezwa katika jumuiya ya Afrika Mashariki nayo ilipita.
Hoja ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na msaada
kutoka nje, alisema mazungumzo yalifanyika baina ya SMT na SMZ yalifikia muafaka
kwamba fomula ya asilimia 4.5 itumike katika kuhakikisha kwamba SMZ inapata
fungu lake.
Pamoja na hizo, hoja nyingine zilizokubaliwa ni
za uvuvi katika ukanda wa uchumi na bahari kuu, Uwezo wa Zanzibar kukopa ndani
na nje ya nchi ambapo makubaliano yaliafikiwa kwamba wizara zinazoshughulikia
masuala ya fedha SMT na SMZ ziandae utaratibu na muongozo.
Hoja ambazo bado zipo katika mazungumzo ni
suala la kodi ya mapato na zuio, Utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili,
Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za Nje, ajira kwa watumishi wa Zanzibar
katika taasisi za muungano na mfuko wa maendeleo wa jimbo kwa SMZ.
Zingine ni malalamiko ya wafanyakazi kutozwa
kodi mara mbili, hisa za SMZ zilizokuwa kwenye bodi ya sarafu ya jumuiya ya
Afrika Mashariki, tume ya pamoja, usajili wa vyombo vya moto, kuimarika
ushirikiano kwa masuala yasiyo ya muungano na kujenga udugu miongoni mwa
Watanzania
Chanzo - Tanzania Daima
Post a Comment