Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt.Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hatua ya kuwavua madaraka
Maafisa wanne wa Jeshi la polisi nchini na kumsimamisha kazi mmoja
kutokana na kukiuka maadili na taratibu za Jeshi la Polisi.
……………………………………………………………….
Na Lydia Churi, MAELEZO
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewavua madaraka Maafisa wanne wa Jeshi la Polisi nchini na kumsimamisha kazi mmoja ambaye atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka maadili na taratibu za jeshi hilo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewavua madaraka Maafisa wanne wa Jeshi la Polisi nchini na kumsimamisha kazi mmoja ambaye atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka maadili na taratibu za jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es salaam leo, Waziri Nchimbi amesema hatua hiyo ni
katika kuendeleza vita ya kuhakikisha kuwa jeshi la polisi linakuwa na
nidhamu, linatekeleza wajibu wake wa kutenda haki na kuwalinda raia na
mali zao.
Alisema amewachukulia hatua
Maafisa hao baada ya kuridhia maoni ya kamati aliyoiunda kufanya
uchunguzi wa matukio yaliyolalamikiwa dhidi ya askari polisi katika
mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Kigoma kati ya Desemba 2012 na
Mei, 2013.
Waziri Nchimbi aliwataja
waliovuliwa madaraka kuwa ni Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani
Arusha Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro, Mkuu wa Upelelezi wilaya ya
Mvomero mkoani Morogoro Inspekta Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha
Polisi cha Dumila Inspekta Juma Mpamba na mkuu wa upelelezi wa wilaya ya
Kasulu ASP Daniel Bendarugaho na kumsimamisha kazi Inspekta Isaack
Manoni.
Alifafanua kuwa Mrakibu wa
Polisi Ramadhan Giro alivuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia
kikamilifu askari na maafisa walio chini yake ambao walikamatwa
wakisafirisha bangi yenye uzito wa kilogramu 540 kwa kutumia gari la
polisi.
Alisema askari hao wawili
waliokamatwa wakisafirisha bangi, walikuwa wakifanya kazi kwenye kituo
cha Ngarananyuki na baada ya kukiri kosa walifukuzwa kazi mwezi Mei
mwaka huu.
Alisema kwa upande wa Inspekta Jamal Ramadhan amevuliwa madaraka yake kwa kutochukua hatua stahiki baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara wa Mvomero Samson Mwita kubambikiwa fuvu la kichwa cha binadamu na askari polisi watatu wakishirikiana na matapeli wawili.
“Katika tukio hilo Inspekta Isaack Manoni amesimamishwa kazi na atashtakiwa kijeshi kutokana na tuhuma za kumtorosha mtuhumiwa, Cpl. Edward aliyekuwa dereva wa gari la Polisi lililokamatwa na bangi kitendo ambacho kimelifedhehesha jeshi la polisi” alisema Waziri Nchimbi.
Alibainisha kuwa Inspekta Juma Mpamba amevuliwa madaraka hayo kwa kuonesha udhaifu katika utendaji wake wa kazi kwa kutosimamia kikamilifu askari walio chini yake kitendo kilichosababisha askari kujipangia kazi nje ya utaratibu na kumbambikiza mfanyabiasha huyo kesi kwa lengo la kujinufaisha kinyume na maadili ya kazi. Aliongeza kuwa askari waliohusika na tukio hilo wamefukuzwa kazi na kushtakiwa.
Waziri Nchimbi alisema ASP Daniel
Bendarugaho amevuliwa madaraka kwa kutokuwa makini katika kufanya na
kusimamia upelelezi wa kesi ya mauaji ya marehemu Gasper Mussa
Sigwavumba aliyeuawa baada ya kupigwa na askari polisi wawili Desemba
mwaka jana.
Alisema upelelezi mbovu
uliofanywa chini ya usimamizi wa Mkuu huyo wa upelelezi ulisababisha
kesi hiyo kuondolewa mahakamani. Aliongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo
utaanza upya ili haki itendeke.
Post a Comment