Na Irene
Mark
MATUKIO ya uporaji na utoroshaji madini
yanazidi kushika kasi ambapo wafanyabishara wawili wa madini ya Tanzanite jijini
Arusha wamejeruhiwa kwa risasi na kuporwa kiasi kikubwa cha madini yenye thamani
ya zaidi ya sh mil. 60 fedha taslimu huku Ofisa Usalama wa Uwanja wa ndege
mkoani Kigoma naye akitiwa mbaroni kwa kutaka kutorosha madini.
Matukio hayo mawili yalitokea juzi na jana
zikiwa ni siku chache tangu kuuawa kwa mfanyabiashara bilionea wa jijini Arusha
Erasto Msuya aliyepigwa risasi zaidi ya 20 wilayani Hai mkoani
Kilimanajaro.
Wakati hali ikiwa hivyo, wakala wa Ukaguzi wa
Madini Tanzania (TMAA) umetangaza kukamata shehena ya madini yenye thamani ya
zaidi ya sh bilioni 13 katika kipindi cha miezi 10 yaliyokuwa yakitoroshwa
nchini kinyume cha utaratibu.
Katika tukio la jijini Arusha lililotokea jana
saa 9:30 alasiri eneo la Pangani, wafanyabiashara Steven Alex na Abel Mutta
walipigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakati wakiwa kwenye gari
kando ya barabara walikokuwa wamekuja kununua madini hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus
Sabas, alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini akadai asingeweza kulizungumzia kwa
vile hakuwa na taarifa kamili.
Hata hivyo mashuhuda wa tukio hilo, walidai
kuwa wafanyabiashara hao walikuwa ndani ya gari aina ya Range rangi ya Silva
ambapo Alex alikuwa upande wa dereva na Abel alikuwa upande wa pili wakiwa na
mtu mwingine nyuma ambaye hakufahamika jina lake mara moja.
Wakati wafanyabiashara hao wakiwa wameegesha
gari kando ya barabara kusubiri kuwalipa watu waliowauzia madini, zilikuja
pikipiki tatu zikasimama kando ya gari lile na vijana watatu walishuka na
bastola kisha kumsogelea Alex wakimtaka afungue mlango.
“Vijana hao walikuwa wakidai afungue awape hela
zao lakini hakufanya hivyo, ndipo wakampiga risasi tumboni na kwenye paja huku
Mutta akipigwa ya mguuni na kisha walifungua mlango wa gari baada ya kuwajeruhi
wakachukua madini na fedha,” alisema shuhuda mmoja.
Aliongeza kuwa baada ya kufanikisha mpango wao,
vijana hao waliondoka na pikipiki zao ambazo zilifichwa sehemu ya namba za
usajili huku kila mmoja akielekea barabara yake.
Ofisa Kigoma
Mkoani Kigoma, mmoja wa maofisa usalama wa
uwanja wa ndege, Clephace Lukindo, alikamatwa na maofisa wenzake uwanjani hapo
akitaka kuvusha madini ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu tisa sawa na thamani
ya sh milioni 400.
Hata hivyo tukio hilo limekuwa likifichwa na
uongozi wa uwanja pamoja na jeshi la polisi mkoani humo kwa kile kinachodaiwa
kuwa ofisa huyo amekuwa akitoa vitisho kwa wafanyakazi wenzake.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, ofisa
huyo ambaye anadaiwa kuwekewa mtego na maofisa wenzake wawili baada ya kubaini
mpango wake huo wa kutaka kuvusha mzigo huo kwa kutumia leseni ya kusafirishia
madini ya mtu mwingine.
Taarifa zilidokeza kuwa ofisa huyo licha ya
kuwa na leseni hiyo isiyokuwa ya kwake, hakuwa na nyaraka zingine za kuonyesha
alikopata mzigo, anaupeleka wapi na kiasi chake.
Chanzo hicho kilidai kuwa baada ya kufika eneo
la ukaguzi, ofisa mwenzake, Yusuf Mpame, na polisi Koplo Theophil walimtaka
aonyeshe vibali na nyaraka hizo ili wathibitishe kuwa mzigo huo unasafirishwa
kihalali.
Hata hivyo Lukindo baada ya kuona wenzake
wamemshtukia na kutaka kumkamata alitumia nguvu kumkaba ofisa mwenzake Mpame
ambaye alimnyonga shingo na kisha kung’ata lakini akanusuriwa na wenzake Koplo
Theophil na Jeremiah.
Meneja wa uwanja huo aliyefahamika kwa jina
moja la Tesha, alipotafutwa na gazeti hili alipokea simu lakini alipoulizwa juu
ya sakata hilo alikatika ghafla hewani na alipopigiwa tena hakupokea.
Mmoja wa wafanyakazi wa uwanja huo alilidokeza
gazeti hili kuwa Lukindo alikuwa ayasafirishe madini hayo kwenda jijini Dar es
Salaam kwa ndege ya Shirika la ndege la Tanzania lakini baada ya sakata hilo
alikamatwa na kupelekwa polisi alikoshikiliwa hadi jana.
Majeruhi aliyeumizwa na mtuhumiwa huyo
alifikishwa hospitali na kupatiwa matibabu ya shingo ingawa Kamanda wa Polisi
mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, licha ya kupigiwa simu mara mbili alikwepa
kulizungumzi tukio hilo akisema anaendelea kulifuatilia.
“Sina taarifa kuhusu tukio hilo unaloliuliza
hadi sasa,” alijibu kamanda lakini alipobanwa aeleze hali ya ofisa aliyejeruhiwa
inaendeleaje alisema hilo bado walikuwa bado wanalichunguza na likikamilika
watalitolea taarifa.
Wakati tunakwenda mitamboni, taarifa
zilizotufikia zilisema kuwa ofisa huyo alipewa dhamana na jeshi hilo.
TMAA na utoroshaji
Madini hayo yalikamatwa kwenye viwanja
mbalimbali vya ndege nchini ambapo wakaguzi wa TMAA walishirikiana na Idara ya
Uhamiaji, Usalama wa Taifa, watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Jeshi la
Polisi na wafanyakazi wa viwanja vya ndege (TAA).
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi
za wakala huyo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa
TMAA, Bruno Mteta, alisema madini hayo yalikamatwa kati ya Septemba mwaka 2012
na Julai mwaka huu katika matukio 23 tofauti.
Alisema kwa mwezi huu tayari wakala huyo
amewakamata raia wawili wa kigeni wakiwa na shehena ya madini wakitaka kutoroka
nayo huku akisisitiza kwamba watapandishwa kizimbani wakati wowote.
“Agosti 20, mwaka huu, tumewakamata raia wawili
wa kigeni mmoja aliyekuwa anasafiri amekamatiwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) akiwa na madini ya vito yenye thamani ya sh milioni
25.32.
“Wa pili amekamatwa akiwa kwenye makazi yake
Jangwani Beach hapa jijini kwa kweli thamani ya madini ya mtuhumiwa huyu
haijafahamika,” alisema na kuongeza kuwa serikali imeyataifisha madini
hayo.
Kwa mujibu wa Mteta wafanyabiashara wa kigeni
na wazawa wanaruhusiwa kusafirisha madini hayo kwa kuzingatia utaratibu ili
serikali ipate mgao wake.
Awali, mkurugenzi huyo alisema tangu mwaka 2009
hadi mwishoni mwa mwaka jana, serikali ilipokea sh bilioni 317.74 ambazo ni
mrabaha uliolipwa na kampuni 10 kubwa za madini hapa nchni.
Alisema hivi sasa wizi wa madini kwenye migodi
mikubwa haupo kutokana na uwepo wa watumishi wa TMAA wanaotoa ripoti ya
uzalishaji kila siku na kwamba wafanyabiashara wa madini wanaoongoza kwa kukwepa
kodi ni wazawa.
Mteta alieleza changamoto zinazowakabili kuwa
ni kushindwa kuifikia mipaka yote inayounganisha nchi jirani (njia za panya)
ambazo hutumiwa na wafanyabiashara wengi kutorosha madini hayo.
Alisema watoroshaji wengi wa madini hayo ni
wageni kutoka nchi mbalimbali ambao wanauziwa madini na Watanzania na kufafanua
kwamba kati ya matukio 23 Watanzania ni wawili.
Alisema tayari kesi tatu kati ya 23
zimesikilizwa na kutolewa hukumu na kutoa mfano wa kesi ya mgeni aliyekamatwa na
madini yenye thamani ya zaidi ya dola 6,200 za Marekani kwamba alitozwa faini ya
sh milioni 1.5 na madini yake kutaifishwa na serikali.
Chanzo - Tanzania Daima
Post a Comment