PICHA NA MAKTABA |
IGP MWEMA, RPC ANDENGENYE WATIWA HATIANI
Na Josephat
Isango
HATIMAYE ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora, kuhusu vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na mauaji
yaliyotokea Arusha Januari 5, 2011 kwenye maandamano ya CHADEMA imevuja.
Licha ya ripoti hiyo kufichwa kwa kutosomwa
hadharani kwenye vyombo vya habari kutokana na kulishutumu moja kwa moja Jeshi
la Polisi, Tanzania Daima imefanikiwa kuinasa.
Maandamano hayo ya CHADEMA ya kupinga ukiukwaji
wa kanuni na sheria katika uchaguzi wa Meya ya Manispaa ya Arusha, Gaudence
Lyimo, licha ya kuruhusiwa na polisi awali baadaye yalipigwa marufuku na Mkuu wa
Jeshi hilo nchini, IGP Saidi Mwema.
Hata hivyo, CHADEMA walikataa kutii agizo hilo
kutokana na taarifa ya IGP kutowafikia kwa maandishi kama inavyoelekezwa kwa
mujibu wa taratibu za utendaji wa jeshi hilo.
Kufuatia vurugu hizo za polisi na wafuasi wa
CHADEMA, watu watatu waliuawa kwa kupigwa risasi, wengine zaidi yya 30
kujeruhiwa na wafuasi zaidi ya 70 wakiwemo viongozi waandamizi wa chama ambao
walifunguliwa mashtaka mahakamani.
Kutokana na tukio hilo Tume ya Haki za
Binadamu, iliunda tume iliyochunguza suala hilo Januari 10 hadi 13 mwaka 2011,
kwa kuwahoji viongozi wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Jeshi la Polisi, hospitalini
walipolazwa majeruhi na njiani walipoandamana wafuasi wa chama hicho.
Tume hiyo iliongozwa na Kamishna Joaquine
De-Mello akiandamana na ofisa uchunguzi, Philipo Sungu, kutoka idara ya elimu
kwa umma na mafunzo kufuatilia tukio hilo kwa muda wa siku tatu ili kupata picha
halisi.
Lengo kuu lilikuwa kubaini chanzo cha vurugu
hiyo, uvunjwaji wa haki za binadamu ambapo Januari 11, asubuhi tume hiyo ilianza
kuonana na madaktari na wagonjwa majeruhi waliolazwa katika hospitali mbili za
Mount Meru na Seliani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo gazeti hili
linayo nakala yake, taarifa zilizopatikana katika hospitali zilionyesha
kupokelewa kwa majeruhi 26 katika hospitali ya Mount Meru na wawili
Seliani.
Majeruhi watatu walipoteza maisha wakati
wakipatiwa matibabu ya awali hapo hospitali ya Mount Meru, 22 walilazwa katika
hospitali ya Mount Meru na watatu walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka
hospitalini.
Ripoti ya madaktari ilithibitisha kuwa vifo
hivyo vilitokana na majeraha ya risasi za moto huku majeruhi wengine
wakithibitisha kupigwa risasi za moto huku wakionyesha majeraha hayo kwenye
miili yao.
Licha ya ripoti kuonyesha vitendo hivyo vya
uvunjifu wa haki za binadamu uliofanywa na polisi, inasema kuwa maandamano ya
CHADEMA na mkutano yalikuwa halali na jeshi ndilo lilisababisha fujo hizo kwa
kutofuata sheria.
“Tanzania inajivunia Katiba inayoainisha
vipengele mbalimbali vinavyotambua na kulinda haki za msingi za binadamu, hivyo
kama nchi nyingine inawajibika kwa Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu la
mwaka 1948 (UDHR) ambalo ni mama wa matamko, makubaliano na mikataba ya vizazi
vyote vya haki,” inasema ripoti hiyo.
Kwamba Tanzania kama miongoni mwa nchi
wanachama zilizoweka sahihi na kuridhia mikataba hiyo zinawajibika moja kwa moja
“kuheshimu, kulinda, kutetea na kutekeleza” haki zilizoainishwa kwenye mikataba
husika.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa “kanuni za jumla za
jeshi la polisi namba 403 kifungu cha kwanza inasema; Mtu yeyote ambaye anataka
kuitisha, kukusanya, kuandaa na mkutano wowote au maandamano katika eneo lolote
hadharani atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi si chini ya saa 48 kabla ya
wakati mkutano au maandamano kufanyika kwa ofisa wa polisi wa wilaya
husika.
Na pindi anapopelekea taarifa kwa maandishi kwa
mkuu wa polisi wa wilaya anaruhusiwa kuendelea kuandaa, kuitisha, kukusanya,
kuunda, au kuandaa mkutano au maandamano kama ilivyopangwa.
Ila mpaka atakapopata taarifa ya maandishi
kutoka kwa Afisa Polisi wa Wilaya husika kueleza sababu za kusitisha maandamano
hayo.”
Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mujibu wa sheria
hiyo, polisi “Officer in charge” wa eneo katika eneo hilo la Arusha mjini ni OCD
wa Arusha Mjini – ndiye aliyepaswa kutoa maelekezo ya kuzuia maandamano na si
Kamanda wa Polisi wa Mkoa au Inspekta Jenerali wa Polisi.
“Kwa mantiki hii, taarifa ya CHADEMA kwa polisi
ilitosha kwa wao kuendelea na mipango yao ya maandamano na mkutano kama
inavyoelezwa kisheria,” anasomeka taarifa hiyo.
Pia inaonyesha kuwa Sheria Na. tano (5) ya
mwaka 1992 ya vyama vya siasa kifungu cha 11 vifungu vidogo vya (4) na (6) na
sheria Na. 1 ya 1939 ya polisi na huduma za mgambo kifungu 43.-(1), (2),
zilikidhi pia hitaji la CHADEMA kuendelea na mipango yao ya maandamano na
mkutano wa hadhara kama ilivyopangwa.
Kwamba Sheria Na.5, 1992 ya vyama vya siasa
kifungu 11. — (8) inasema: kama jeshi la polisi linasitisha maandamano au
mkutano taarifa hizo hutolewa kwa maandishi kueleza sababu, wala si kutumia
televisheni, kama ilivyojitokeza kwa tukio la Arusha.
“Hivyo CHADEMA walikuwa sahihi kwa kuwa
hawakupata taarifa ya kimaandishi licha ya polisi kudai kutoa barua hiyo lakini
walishindwa kuthibitisha madai yao mbele ya tume.
Ripoti hiyo pia inaongeza kuwa askari walifanya
vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya viongozi na waandamanaji hasa
wanawake bila kujali hali zao.
Kwa mfano wanatajwa mbunge wa viti maalum Lucy
Owenya na mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Josephine Mushumbusi, kuwa walipigwa na
kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao.
Kwamba viongozi wa CHADEMA na wananchi wengi
walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi kati mjini
Arusha.
“Askari waliwapiga waandishi wa habari,
waliwanyang’anya vifaa vyao vya kazi na kufuta picha na kazi walizokuwa
wanazifanya kwenye maandamano. Askari na waandamanaji walisababisha uharibifu wa
magari na mali za umma na wananchi.
“Aidha walisababisha upotevu wa mali za
wananchi zikiwemo simu mbili za mkononi za Owenya na fedha tasilimu sh 2,700,000
za majeruhi Ally Ogaga walizodai kunyang’anywa na askari, wakati Ofisi ya CCM
Mkoa wa Arusha ilivunjwa vioo kwa mawe na waandamanaji na nyumba ya mwananchi
Salum Ally iliungua kwa moto uliosababishwa na mlipuko wa bomu lililoruka kutoka
kwenye gari la polisi,” ilisomeka.
Chanzo Tanzania
Daima
Post a Comment