Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akielezea jinsi
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyosikitishwa na Kitendo cha raia
wawili wa Uingereza Katie Gee na Kisty Trup cha kumwagiwa tindikali
(Acid) na watu wasiojuilikana katika maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar. Kushoto
ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said
Ali Mbarouk, Kulia yake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed wakiambatana na Bamalozi wa
heshima wa Uingereza, Ujerumani an Marekani waliopo hapa Zanzibar.
Kikao
hicho cha dharura kilifanyika Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar
na kushuhudia pia na baadhi ya Viongozi wa Jumuia za utembezaji watalii
za hapa Zanzibar ZATO na ZATI. Picha na Hassan Issa wa – OMPR -- ZNZ.
****************************************
Othman Khamis Ame
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na kitendo kibaya na kiovu
walichofanyiwa raia wawili wa kike wa Uingereza Katie Gee na Kisty Trup
cha kumwagiwa Tindi kali { Acid } mapema jana usiku katika maeneo ya
Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Raia
hao wawili wa Uingereza ambao wamekuja Nchini Tanzania kwa kazi za
kujitolea wakiwa hapa Zanzibar kwa matembezi ya wiki wamejeruhiwa katika
sehemu zao za uso na vifua na watu ambao mpaka sasa bado
hawajajuilikana.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo hapo
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Mabalozi wadogo
wa Heshima wa Uingereza, Ujerumani na Marekani waliopo hapa Zanzibar
walioambatana na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni Utalii na
Michezo pamoja na Jumuia zinazojihusisha na utembezaji watalii za ZATO
NA ZATI.
Balozi
Seif alisema kwa kuwa hilo sio tukio la bahati mbaya kufanya hivyo
amewaomba wananchi popote pale walipo kujaribu kusaidia kutoa taarifa
kwa vyombo vya ulinzi mara tuu watakapoona dalili za watu waliohusika na
vitendo hivyo.
Alifahamisha
kwamba Zanzibar ni moja ya Nchi inayosemwa vizuri katika Nyanja za
Kimataifa, lakini kwa mfumo huu uliojichomoza unaofanywa na baadhi ya
watu wachache wasioeleweka malengo yao unaweza kukatisha tamaa kwa wale
wageni waliojipangia kutaka kutemebelea Zanzibar.
“
Ipo kumbu kumbu hapo nyuma na nyengine si ya muda mrefu ya matukio ya
baadhi ya watu kumwagiwa tindi kali { Acid } lakini hichi cha wageni
hawa waliokuwa kujitolea hapa Nchini kimewafanya kupewa adhabu
wasiyostahiki “. Alielezea Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewahakikishia Mabalozi hao
wadogo wa Heshima hapa Zanzibar wa Uingereza, Ujerumani na Marekani
kwamba Serikali kwa kushirikiana na Vyombo vya ulinzi kwa msaada wa
Wananchi itafanya uchunguzi na kuhakikisha wahusika wa kitendo hicho
wanatiwa nguvuni ili kupelekwa katika vyombo vya sheria.
Mapema
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema
Vijana hao wa kujitolea kutoka Uingereza Katie Gee na Kisty Trup
walipatia huduma ya kwanza katika Hoteli ya Tembo iliyopo Forodhani
chini ya usimamizi wa Dr. Saleh Mohammed Jidawi Katibu Mkuu Wizara ya
Afya.
Alisema
tukio hilo la tindikali linaloonekana kutumiwa na baadhi ya wakorofi
kama sialaha kwa kuwaathiri watu wasio na hatia limeleta athari kubwa na
kutia doa katika sekta ya Uchumi.
Waziri
Mbarouk alimpongeza Balozi wa Heshima wa Uingereza hapa
Zanzibar Balozi Carll Salisbury kwa hatua zake za kutoa usafiri wa
Ndege ili kusafirishwa kwa vijana hao ili kuendelea kupatiwa matibabu
zaidi Mjini Dar es salaam na baadae Nchini mwao.
Wakichangia
katika kikao hicho Ofisa wa Ubalozi wa Marekani hapa
Zanzibar Jefferson Smith na Balozi wa Heshima wa Uingereza hapa
Zanzibar Carll Salisburg walisema Serikali ni vyema ikawa na utaratibu
wa kufanya uchunguzi wakati yanapotokea matukio yasio ya kawaida ndani
ya Jamii.
Nao
wawakilishi wa jumuiya za watembezaji watalii hapa Zanzibar wameiomba
Serikali kutenga fungu maalum kwa ajili ya kuviunga mkono vyombo vya
ulinzi katika kukabiliana na matukio yanayoashiria kutaka kuvunja amani
na kuhatarisha maisha ya Jamii.
Kwa
upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mohammed Aboud Mohammed ameiasa jamii kujenga tabia ya kuchukia jambo
lolote baya lionaloonekana kujichomoza miongoni mwao katika maeneo
wanayoishi.
Waziri
Aboud alieleza kwamba mazingira yaliyopo mitaani hivi sasa
yamejidhihirisha wazi kuwa wapo baadhi ya watu wanaoshabikia matendo
maovu yanayofanyika katika sehemu zao ambayo wanaelewa wazi kuwa hatma
ya matendo hayo hufikia hatua ya kuwaathiri hata wao wenyewe.
Post a Comment