Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
Jaji Joseph Warioba
******
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameionya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, kutoingilia maoni ya wananchi wanaojadili
rasimu ya Katiba hiyo.
Sumaye amesema tume ya Jaji Warioba haipaswi kuwa
na msimamo wake kuhusu maoni yaliyotolewa na wananchi maana wamekwisha yaweka
katika rasimu.
Mchakato wa kutungwa Katiba Mpya umefikia hatua ya
kujadiliwa na mabaraza katika ngazi za wilaya, kata na asasi za kijamii ambapo
maoni yanaendelea kutolewa.
Sumaye alitoa karipio hilo wakati akifunga mkutano
wa baraza la Katiba katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, kampasi ya Mbeya ulioandaliwa
na Chama cha Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahliso).
kumekuwapo na kauli kadhaa zinazotolewa na vyama
vya siasa, asasi za kiaraia na tume hiyo, zikitafsiriwa kama kuingilia mchakato
wa majadiliano ya umma kuhusu Katiba Mpya.
“Wao (tume), wamekwisha toa rasimu ya maoni, basi
wayaachie mabaraza ya Katiba wajadili rasimu hiyo, badala ya kuonekana tume nayo
ina msimamo wake ambao inataka upitishwe,” alisema.
Hata hivyo, Sumaye alisema tume hiyo haipaswi
kulaumiwa kutokana na maoni yaliyojitokeza kwenye rasimu inayojadiliwa sasa.
“Ili mradi kazi ya tume ilikuwa ni kuratibu maoni
ya wananchi, basi tume haipaswi kulaumiwa kwa maoni yaliyotolewa, isipokuwa kama
tume imetoa rasimu isiyowakilisha maoni na wananchi walivyoyatoa,” alisema.
Wakati wa kutoa maoni yao bila shaka wapo
Watanzania waliotaka serikali moja, wapo waliotaka serikali mbili, waliotaka
serikali tatu, waliotaka serikali nne labda wapo waliotaka serikali ya mkataba
na inawezekana labda wapo waliotaka tuachane na Muungano.
Kwa mujibu wa Sumaye, siyo sahihi mtu au kundi la
watu kukejeli au hata kutukana mtu au kundi lingine lililotoa maoni
yanayotofautiana na yake au ya kundi lake.
Alisema, Watanzania wanapaswa kujifunza
ustahimilivu na kuheshimu maoni au mawazo ya watu wengine, na kama hatukubaliani
nayo, wayapinge kwa nguvu ya hoja na siyo hoja ya nguvu.
Sumaye alimkariri mwanazuoni, marehemu Wole
Soyinka, aliyewahi kusema, the greatest threat to freedom is the absence of
criticism, akimaanisha tishio kubwa kwa demokrasia ni kutokuwapo kwa
ukosoaji.
Sumaye alisisitiza kuwa matatizo yaliyopo nchini,
mathalani maisha magumu na maendeleo duni, hayawezi kutatuliwa kutokana na
kuwapo kwa Katiba Mpya.
Kauli kama hiyo, iliwahi kutolewa na Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete,
kuizindua Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Sumaye alisema, anaamini kwamba hata Katiba
iliyopo sasa bado ni nzuri, akitumia kigezo cha kutumika kwake kwa kipindi cha
miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, kutokana na changamoto na mabadiliko
yanayojitokeza, Katiba hiyo ingehitaji marekebisho.
USHIRIKI WA TAHLISO
Sumaye alisema ushiriki wa TAHLISO katika baraza
la Katiba, una umuhimu wa pekee kutokana na sababu tofauti.
Alizitaja baadhi yake kuwa ni TAHLISO
kuwawakilisha vijana wasomi wenye uelewa, ambao mchango wao utatoa upeo wa hali
ya juu katika Katiba hiyo.
Pia alisema vijana wana umuhimu wa pekee katika
mchakato wa Katiba hiyo, kwa vile watapenda kuwa na chombo hicho (katiba)
kitakachoitengeneza Tanzania inayofaa.
“Kijana utakuwa mtu wa ajabu sana kama utataka
kuishi kwa miaka hamsini ijayo katika nchi ya shida isiyo na maendeleo, iliyojaa
rushwa, na isiyo na matumaini,” alisema.
Aliongeza, “vijana wa Tanzania wakiongozwa na
ninyi wasomi, lazima mshiriki kutengeneza Katiba itakayoweka, kwa miaka mingi
ijayo, mazingira ya nchi yetu ya salama na amani na pia ya maendeleo kwa wote
bila kujali rangi, dini, jinsia au ukundi wowote.”
RASIMU YA KATIBA MPYA
Sumaye alisema kuna vipengele vingi katika rasimu
hiyo, akiivita kuwa ‘vigumu’ na ‘vyepesi’.
Kuhusu ‘sakata la Muungano’, Sumaye alisema idadi
ya serikali zitakazoundwa si jambo kubwa kwake, bali hoja zinazowiana na muundo
huo.
Alizitaja hoja hizo kuwa ni sababu za kufikia
uamuzi huo, ikiwa serikali tatu itatoa jawabu la kuyatatua matatizo yaliyopo na
kuubaini muundo utakaoutikisa Muungano.
Alizitaja hoja nyingine zinazohitaji majawabu kuwa
ni uwezekano wa kugharamia serikali tatu na vyombo vyake.
“Ni dhahiri kuna maswali yanayotaka majibu au kama
majibu hayapatikani, basi tukae chini tuyatafakari kwa makini zaidi,”
alisema.
Alisema yapo matatizo makubwa manne ambayo
hayajatatuliwa chini ya mfumo wa serikali mbili, na kwamba serikali tatu
itayafanya kuwa magumu zaidi.
Aliyataja kuwa ni mvutano wa madaraka na wa
utaifa, mgawanyo wa rasilimali, gharama za uendeshaji na changamoto zinazotokana
na jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama.
AUZUNGUMZIA UADILIFU
Sumaye alisema Katiba Mpya pekee si mwarobaini wa
matatizo ya jamii, bali inahitaji kusimamiwa na serikali adilifu, inayojali
maslahi ya umma.
Pia alisema Rais wa nchi anapaswa kuwa mchapakazi
na anayejali maslahi ya umma mpana na siyo maslahi yake binafsi, ya watoto wake
au ya marafiki zake.
“Yeye mwenyewe (Rais) awe na uadilifu usiotiliwa
mashaka ya aina yoyote na apigane vita vya wazi dhidi ya rushwa, ufisadi, dawa
za kulevya na maovu mengineyo katika jamii,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment