Serikali
itachunguza orodha ya vitu vilivyolipwa fidia wakati wa uthamini wa
mali za wakazi wa kijiji cha Mloganzila jijini Dar es Salaam , baada ya
wananchi kudai wamepunjwa na majalada ya mali kutoweka kinyemela.
Hatua hiyo ilitangazwa na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, baada ya kulalamikiwa na wanavijiji kuwa wathamini wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walichakachuua fidia ya
mali zao.
Eneo la Mloganzila limekuwa na mgogoro
wa ardhi karibu miaka 10 baada ya serikali kulichukua kwa wananchi ili
kujenga Chuo Kikuu kipya cha Afya na Tiba pamoja na hospitali ya
kisasa.
Hata hivyo ilijimilikisha bila kuwalipa
wananchi fidia ya ardhi kwa maelezo kuwa lilikuwa ardhi ya kampuni ya
umma ya kusindika nyama hivyo bado ni mali yake ikiwalipa fidia ya
majengo na mazao lakini si ya ardhi.
Wakazi hao walimweleza Waziri Mkuu Ijumaa
wiki hii alipozuru eneo hilo kuwa baadhi ya taarifa za mali zao
zimenyofolewa na kuchakachuliwa kwenye majalada na kuambulia Sh 50,000.
Aliwaambia kuwa ipo sheria ya viwango kwa
kila uthamani inayotaja kiwango cha fidia kwa kila kinachothaminiwa
hivyo lilikuwa jukumu la wananchi kuijua na kufuatilia.
Pia aliwaambia kuwa serikali itaangalia orodha ya kilichothaminiwa katika maeneo yao ili kubaini kasoro na kuzirekebisha.
Mwanakijiji mmoja wa Mloganzila alimweleza
Waziri Mkuu licha ya kumiliki nyumba ya kisasa ya vyumba sita pamoja
na mazao mengi aliambulia fidia ya milioni tano.
Alipolalamikia kupunjwa fidia alikwenda
kuangalia jalada lake na kubaini kuwa taarifa za mali zake zilinyofolewa
na kudai kuwa amepunjwa.
Wananchi wengi walilalamika kuwa licha ya
eneo hilo kuwa mali ya umma wao ni Watanzania wanaostahili fidia kama
ambavyo Wanabagamoyo watakavyofidiwa na kujengewa nyumba na mradi wa
bandari ya Bagamoyo.
Walihoji sababu za kuwafidia ardhi na mali
wakazi wa Chasimba waliovamia eneo la Wazo Hill mali ya kiwanda cha
sementi cha Heidelberg, kulipwa fidia ya maendelezo na ya ardhi.
Pia walipinga serikali kuwapa viwanja
Mabwe Pande watu waliojitumbukiza na kuishi mabondeni Jangwani na
Msimbazi tena kwa ujeuri lakini inawapunja fidia, kuwanyima viwanja na
kuchukua ardhi ya wanavijiaaji wa Mloganzila.
Wananchi karibu 3,000 wa kijiji cha
Mloganzila wameondolewa eneo hilo na kulipwa fidia ya kuendeleza ardhi
hiyo waliyodai ni ndogo kupindukia ikiwa ni Sh.6,000.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment