MUUNGANO wa vyama vya siasa vya upinzani nchini, jana ulitinga ofisi za Msajili wa Vyama, Jaji Godfrey Mutungi, kwa nia ya kueleza dhamira yao ya kupinga Rais Jakaya Kikwete kuusaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Vyama hivyo vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, vinavyounda ushirikiano wa kisiasa wa kupinga Rais kusaini muswada huo, vilimfafanulia Msajili huyo kilichotokea bungeni hivi karibuni, kwa wabunge wa upinzani nje ya ukumbi wa Bunge, wakati wale wa CCM wakipitisha muswada huo pamoja na marekebisho yake.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viunga vya viwanja vya Ofisi ya Msajili, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ushirikiano huo, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema moja ya mapendekezo waliyompatia Msajili ni kutaka maridhiano ya kikatiba, hivyo Rais Jakaya Kikwete asisaini sheria hiyo.
“Tumefanya mazungumzo na Msajili, tulifika kumsabahi na kumweleza yaliyojiri bungeni kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mchakato ulianzia tume mpaka kura ya maoni ya katiba… Zanzibar haikushirikishwa, Serikali ilipeleka vipengele 6,” alisema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba alisema Oktoba 10 mwaka huu, ni siku ya kitaifa ya kupinga kusainiwa kwa Sheria hiyo na kwamba maandamano yatakayofanyika yatakuwa ya amani.
“Oktoba 10, wananchi wajiandae kukutana katika viwanja vya Jangwani, ni siku ya kitaifa, taratibu zote zitaelezwa, maandamano, mikutano na shughuli zote zitakuwa za amani. Hatusubiri Jeshi la Polisi kuzuia, Jeshi la Polisi linapokea taarifa na zitafuatwa kadiri iwezavyo,” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumza kwa niaba ya Chadema Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema ushirika wao utatumia njia za kidemokrasia kushinikiza Rais asisaini Sheria hiyo.
“Tutatumia njia za kidiplomasia kupinga na kuwaandaa wananchi kwa kutumia njia hizo, kwani jambo hili limekuja kwa muda muafaka kutokana na kauli zilizotolewa na viongozi wa masuala hayo, Jaji Joseph Warioba na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema kauli ya Jaji Warioba juu ya kuwepo kwa kasoro katika kipengele kinachomhusisha pamoja na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inasadifu uhalisia wa mapungufu yaliyomo kwenye sheria hiyo, na kumtaka kwenda mbali zaidi kwa kuainisha vipengele visivyokidhi upatikanaji wa Katiba mpya.
Alisema makundi mbalimbali pamoja na wananchi wa Zanzibar hawakushirikishwa wakati Kamati ya Bunge ya Sheria ikikusanya maoni.
Pia alisema kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Chikawe kuwa Katiba haipatikani Kibanda Mti wala Jangwani ni ulevi wa madaraka na wala haitarudisha nyuma juhudi za Muungano huo kwa maslahi ya wananchi.
Pia alisema Waziri Chikawe amewahi kukiri kuwa kuna vifungu vya katiba ambavyo havikushirikisha Wazanzibari na kwamba kigezo hicho kilipaswa kutumika kwa Waziri huyo kumshauri Rais Kikwete asisaini.
Hata hivyo, Jaji Mutungi hakuweza kupatikana kuzungumzia mwafaka uliopatikana na kama mapendekezo hayo ameyapokea, badala yake msemaji wake, Happiness Muyombo, alisema Msajili huyo ana kikao kirefu, hivyo atazungumza na vyombo vya habari wakati mwingine.
Vyama hivyo viliamua kuungana kwa pamoja kupinga kusainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 pamoja na kutangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
on Monday, September 30, 2013
Post a Comment