MWANAMKE mkazi wa jijini Arusha, Farida Ismail (29) amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akiwa na kilo 7 za bangi. Inadaiwa mtuhumiwa alikuwa ameficha bangi hiyo kwenye begi lake kwa kushona mfuko wa ndani.
Alikamatwa jana saa 10.20 alfajiri baada ya mzigo wake kufanyiwa upekuzi na maofisa wa uwanja wa ndege.
Alitaka kusafiri kwa ndege TK673 aina ya Boeing 738 iliyokuwa ikienda Istanbul, Uturuki. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alikiri kuwepo kwa tukio hilo.
"Ni kweli tukio hilo lipo na limetokea muda huo huo uliosema yaani alfajiri, lakini sasa hivi nipo nyumbani lakini kesho (leo) nitatoa taarifa kamili,’’ alisema Kamanda.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka uwanjani hapo, maofisa wa ukaguzi wa KADCO walipopekua, awali hawakugundua kama kuna bangi katika begi la mama huyo hadi hapo walipojiridhisha kwa mara ya pili ndipo waligundua ilipokuwa imeshonewa kwenye begi.
“Tulimkamata majira ya saa 10.20 alfajiri ya leo (jana) na kilo saba ya bangi na alificha kwa ustadi mkubwa katika begi lake lakini tuligundua,’’ alisema mmoja wa wafanyakazi wa uwanja huo.
Post a Comment