THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Mifuko ya
Hifadhi nchini itaendelea kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa kugharimia miradi
mbali mbali nchini lakini kwa namna ya kuilinda ili Serikali isije kuua bata wa
dhahabu anayetaga mayai ya dhahabu.
Rais pia amesema kuwa
Mifuko ya Hifadhi yote katika Tanzania ni salama kabisa na hatairajiwi kukumbwa
na changamoto za ukwasi hadi mwaka 2040 ikitokea kunakuwepo na hitilafu katika
uendeshaji wa Mifuko hiyo ama baadhi yake.
Rais pia amesema kuwa
misaada inayotolewa na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC)
ni ya aina yake duniani kwa sababu wanufaika wakubwa wa misaada hiyo wanapewa
uhuru wa kuamua ni miradi gani ndani ya nchi igharimiwa na misaada ya MCC.
Vile vile, Rais
amezitaja sekta kubwa ambako wawekezaji kutoka Marekani wanaweza kuweza mitaji
yao kama njia ya kuongeza uwekezaji wao katika Tanzania na hivyo kusaidia
kukuza kwa kasi zaidi uchumi wake.
Rais Kikwete alikuwa
akizungumza leo, Alhamisi, Septemba 26, 2013, kwenye Hoteli ya Hyatt, mjini New
York, Marekani katika Mkutano wa Uwekezaji wa nchi chache za Afrika na
wafanyabiashara wa Marekani ulioandaliwa na MCC
yenyewe na kufanyika chini ya uenyekiti wa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Bwana
Daniel W. Yohannes.
Mkutano huo ambao
kaulimbiu yake ilikuwa, “Africa’s Economic Transformation”
umehudhuriwa na viongozi wa nchi nne
ambazo zilizonufaika na awamu ya kwanza ya miradi mikubwa ya MCC, Tanzania ikiwa ndiyo nchi iliyopewa
fedha zaidi za Shirika hilo duniani za kiasi cha dola za Marekani 698 ambazo
zimeingizwa katika miradi ya miundombinu ya barabara, usambazaji umeme vijiji,
ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na usambazaji wa huduma ya maji katika Jiji
la Dar Es Salaam na Manispaa ya Morogoro.
Tanzania sasa imeanza
majadiliano na MCC kuhusu awamu ya
pili ya msaada wa Shirika hilo.
Mbali na Rais Kikwete,
viongozi wengine ambao wamehudhuria Mkutano huo ni Rais Armando E.Guebuza wa
Mozambique, Waziri Mkuu wa Lesotho Mheshimiwa Tom Thabane na Waziri Mkuu wa
Morocco Mheshimiwa Abdalleh Benkiane.
Akijibu maswali katika
Mkutano huo baada ya kuwa ametoa hotuba yake, Rais Kikwete amesema kuwa hakuna
shaka kuwa Mifuko ya Hifadhi nchini imeanza kuchangia kwa kiasi kikubwa miradi
ya maendeleo na itaendelea kufanya hivyo kwa namna ya kuifanya mifuko yenyewe
endelevu.
“Hakuna shaka kuwa
Mifuko ya Hifadhi Tanzania sasa imeanza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya
nchi yetu. Kwa kiasi kikubwa ilikuwa fedha ya Mifuko hiyo iliyosaidia kujenga
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na inachangia miradi mingine mingi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Isitoshe, mifuko yetu
yote ni salama na ina afya nzuri. Haitarajiwi kuwa inaweza kupata matatizo kwa
miaka mingi ijayo hadi mwaka 2040 na matatizo yatatokea tu kama tukiendesha
mambo yetu vibaya. Tunaitumia mifuko yetu vizuri na kwa manufaa ya maendeleo ya
nchi yetu. Tutaitumia vile vile kwa namna endelevu yaani tusije tukaua bata wa
dhahabu ambaye anataga mayai ya dhahabu.”
Kuhusu misaada ya MCC, Rais Kikwete amesema kuwa “misaada
hiyo ni ya aina yake duniani kwa sababu ina uhuru. Nchi inayopewa msaada
inapewa uhuru wa kuamua yenyewe ni miradi gani igharimiwe na msaada unaotolewa
na MCC. Ni modeli nzuri na aina yake duniani.”
Amesisitiza Rais
Kikwete: “Nani angekubali kugharimia barabara za Namtumbo hadi Songea? Nani
angegharimia barabara ya kutoka Tunduma hadi Sumbawanga? MCC imekubali kutupa
fedha ya kugharimia miradi hiyo baada ya kuwa sisi wenyewe tumefanya uamuzi”.
Rais Kikwete ameongeza: “Isitoshe,
MCC inachukua muda mfupi kufanya maamuzi. Hata pale ambako sisi tunaopewa pesa
tunalazimika kupata kibali cha matumizi ama kufanya mabadiliko kwenye maamuzi
kuhusiana na miradi inayogharimiwa na MCC, uamuzi unachukuliwa kwa haraka bila
ucheleweshaji ambao tunakumbana nao katika mahusiano yetu na baadhi ya
mashirika ya kimataifa.”
Kuhusu nafasi za uwekezaji katika Tanzania, Rais
Kikwete amewaambia wawekezaji hao kuwa nafasi ziko katika sekta za ujenzi wa
miundombinu ya barabara, reli, bandari za Mtwara na Tanga, na umeme; sekta ya
utafutaji na uchimbaji wa gesi na utoaji wa huduma kwa sekta hiyo mpya katika
Tanzania; uwekezaji katika sekta ya uvuvi; uwekezaji katika sekta ya kilimo na
viwanda vinavyotegemea kilimo; uwekezaji katika utalii iwe Tanzania ama
Tanzania Visiwani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
26 Septemba, 2013
Post a Comment