18/0/2013
Tanzania inatarajia kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa chuma barani
Afrika kwa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka pindi uzalishaji wa
madini hayo utakapoanza mwaka 2018/19 katika eneo la Liganga wilayani
Ludewa.
Hayo
yamebainishwa na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Shirika la Taifa la
Maendeleo (NDC) Abel Ngapemba wakati akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam leo.
Alisema
mradi huo wa uzalishaji chuma utakaotekelezwa chini ya kampuni ya
Tanzania China Mineral Resources Limited (TCIMRL), ambayo ni kampuni ya
ubia kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Shirika la Sichuan
Hongda Group (SHG) ya China utaenda sambamba na uzalishaji wa madini ya
Titanium na Vanadium.
“Mradi
huo ukikamilika tutaweza kuzalisha tani milioni 219 za chuma ambazo
zitadumu kwa zaidi ya miaka 70, na madini mengine yatakayotokana na
mgodi huo ni Titanium tani 175,400 kwa mwaka na Vanadium tani 5,000 kwa
mwaka”. Alisema Ngapemba.
Aidha
Ngapemba alisema kuwa uzalishaji huo utaiwezesha Tanzania kushika
nafasi ya nne ikizifuatia nchi za Afrika Kusini inayozalisha bidhaa za
chuma tani milioni 8.5 kwa mwaka, Misri tani milioni 8.0 na Libya tani
milioni 2.0 kwa mwaka.
Mradi
huu ni moja ya miradi miwili iliyopo katika mkataba kati ya NDC na SHG
uliotiwa saini Septemba 21, 2011 ya uanzishwaji wa mgodi wa makaa ya
mawe na ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa megawati 600 katika eneo la
Mchuchuma.
Miradi
mingine ni pamoja na ujenzi wa msongo wa umeme wa kilovoti 220 kati ya
Mchumchuma na Liganga, na uanzishwaji wa mgodi wa chuma pamoja na
ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua chuma , kiwanda cha kuzalisha bidhaa za
chuma na ujenzi wa barabara kati ya Mchuchuma na Liganga.
Chuma
kinachozalishwa duniani ni takribani tani bilioni 1.55 kwa mwaka,
mzalishaji mkubwa ikiwa ni China inayotoa tani milioni 711 kwa mwaka
ambayo ni sawa na asilimia 46 ya chuma chote kinachozalishwa duniani.
Miradi
hii itakayogharimu Dola za Kimarekani bilioni 3 inatarajiwa kuliingizia
Taifa mapato ya Dola bilioni 1.7 kwa mwaka itakapoanza uzalishaji
wake.
Post a Comment