JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHINI
Awamu ya Pili ya Operesheni Kimbunga imeweza
kukamata majambazi ya kutumia silaha 67 na wahamiaji haramu 134 katika kipindi cha wiki moja tangu kuanza kwake Septemba 21hadi Septemba 27 mwaka
huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
Silaha zilizokamatwa ni pamoja na bunduki
aina ya SMG Moja, Pisto Moja na Magobole 17 pamoja na risasi 115 zikiwemo za
bunduki aina ya SMG 102 na Risasi za Pisto 13. Aidha, Magazine mbili
zilikamatwa pamoja na Sare za Jeshi la Burundi.
Wahamiaji haramu waliokamatwa wengi wao ni
kutoka nchi za Burundi ambapo raia wake 114 walikamatwa wakiishi nchini kinyume
na sheria wakati raia wa Rwanda 20 walikamatwa katika kiindi hicho.
Aidha, watu Watatu walikamatwa kwa tuhuma za
kuhifadhi wahamiaji haramu nchini huku Lita 271 za gongo , ngozi ya Mbwea,
Bangi kilo Tatu na Makokoro 12 vilikamatwa wakati wa operesheni Kimbunga awamu
ya Pili ikiwa katika wiki yake ya kwanza.
Wakati huo huo, Wilaya ya Karagwe mkoani
Kagera imejipanga kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu ili kuhakikisha kuwa
tatizo hilo linafikia mwisho wake na kuwapa nafasi wananchi kufanya shughuli
zao za kijamii na kimaendeleo bila ya hofu ya kufanyiwa uhalifu na wahamiaji
haramu.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bi Dari Rwegasira
amewaambia Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata aliokutana nao katika
Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, mwishoni mwa wiki iiliyopita kuwa
kuanzia sasa kila kiongozi, kuanzia ngazi ya Kiijiji/Mtaa, Kata, Tarafa na
Wilaya, atawajibika kwa jinsi anavyoshughulikia kumaliza tatizo la wahamiaji
haramu katika eneo lake.
Wilaya ya Karagwe ni moja ya wilaya zenye
tatizo sugu la wahamiaji haramu ambao wanatuhumiwa kuwanyanyasa wananchi katika
baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo, kwa kuendesha vitendo vya wizi wa mifugo,
kuvamia maeneo ya kilimo, na pia kuchochea uhalifu wa unyang’anyi wa kutumia
silaha na kusababisha mauaji.
Wahamiaji hao haramu wanashutumiwa kufanya
baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Karagwe yasipitike kwa urahisi, mojawapo ikiwa ni
eneo la msitu wa Kimisi, ambapo eneo hili limekuwa na matukio mengi ya ujambazi
wa kutumia silaha na wananchi kuvamiwa na kuibiwa mali zao na hata wengine
wakipoteza maisha katika matukio hayo.
Maazimio kadhaa yalitolewa katika kikao hicho
kati ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe na Watendaji Wakuu wa Wilaya hiyo, ikiwa ni
pamoja na kuwa:
·Viongozi kuanzia ngazi ya Kijiji/Kitongoji,
Kata hadi Tarafa kutia saini mkataba wa kushughulikia wahamiaji haramu,
majambazi wa kutumia silaha na wafadhili wao, mifugo haramu inayoingia nchini
kutoka nchi jirani pamoja na vitendo vyote vya uhalifu katika maeneo
wanayoyaongoza.
· Kiongozi yoyote wa Kijiji, Kata au Tarafa
atakayeshindwa kushughulikia wahamiaji haramu walioko katika eneo lake
atawajibishwa.
· Wahamiaji wote haramu ambao bado wapo katika
maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo wasakwe na kurejeshwa kwao mara moja.
· Msako uanzishwe mara moja kuwasaka wahamiaji
haramu wote ambao wamejificha katika maeneo ya misitu na ranchi za mifugo
zilizoko katika wilaya hiyo kwa kuvishirikisha vyombo vyote vya Utawala na vya
Ulinzi na Usalama vilivyoko katika Wilaya hiyo.
· Kila kijiji kiwe na takwimu sahihi za wageni
waliopo katika maeneo yao.
· Wahamiaji haramu wote wanaorejeshwa kwao
wasipewe nafasi ya kurudi tena nchini na mwananchi yoyote atakayebainika
kuwapokea au kuwasaidia kurejea atolewe
taarifa haraka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
· Vibali vyote vya Ukazi vilivyotolewa kwa
wageni mbalimbali sasa vitakaguliwa upya ili kuhakiki uhalali wake.
Imeandaliwa na Timu ya Habari ya Operesheni
Kimbunga
Septemba30,2013
Post a Comment