Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SERIKALI IMEKASIMU MADARAKA KWA WAKUU WA SHULE, VYUO NA WALIMU WAKUU KUHUSU USIMAMIZI WA UTUMISHI WA WALIMU ILI KUONGEZA UFANISI


IMG_5671
Naibu Katibu, Tume ya Utumishi wa Umma Bw.Edwin Mikongoti akieleza kwa waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mpango wa serikali wa  kukasimu madaraka kwa wakuu wa shule,  vyuo  na walimu wakuu kuhusu usimamizi wa utumishi wa walimu ili kuongeza ufanisi,wakati wa Mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO). IMG_5680
Katibu Msaidizi, Idara ya Utumishi wa Walimu,Tume ya Utumishi wa Umma(kulia) akiwaeleza waandishi wa habari faida za mfumo wa ugatuaji madaraka ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi sehemu za kazi.wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).kushoto ni Katibu Msaidizi, Idara ya Utumishi wa Walimu,Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Evelyne Omari. Picha na Georgina Misama-Maelezo

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TUME YA UTUMISHI WA UMMA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
Tume ya Utumishi wa Umma imepewa dhamana ya kuhakikisha kuwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu zinatekeleza mamlaka waliopewa ya usimamizi na uendeshaji wa Rasilimali watu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma ili kuimarisha Utawala bora na Uwajibikaji.
Idara ya Utumishi wa Walimu ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya 2002 Kifungu 6(4), Kanuni Na. 6(h) na Na. 35(2)(b) za Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 imepewa Mamlaka ya Kushughulikia Masuala ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu wote walio katika Utumishi wa Umma.

Kwa Mujibu wa Kifungu 21(2) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.18 ya Mwaka 2007 na kwa Kanuni Na.118 ya Kanuni za Utumishi wa Umma ya mwaka 2003, Tume ya Utumishi wa Umma imepewa uwezo wa kukasimisha madaraka yake kwa Wakuu wa Shule, Vyuo na Walimu Wakuu.  Masuala yanayokasimishwa ni yale ya kiutumishi na ushughulikiaji wa makosa madogo madogo ya kinidhamu kwa Walimu na Wakufunzi walio vyuoni, Walimu wa Shule za Sekondari na Shule za Msingi.
Ili kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa masuala ya kiutumishi Wakuu wa Vyuo vya Ualimu/ Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wanatakiwa kuwajibika katika kuwaelimisha Walimu taratibu za masuala ya ajira katika maeneo ya:- Ajira na Usajili; Kuthibitisha kazini Walimu; Kubadilisha kazi/cheo Walimu; Kupandisha vyeo Walimu.
Aidha watashughulikia pia makosa madogo madogo ya kinidhamu na kutoa adhabu. Madaraka yamekasimiwa kwa makosa ambayo kama yakithibitika adhabu zake kwa mujibu wa Kanuni Na. 118 ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003 zitakuwa ni:- Onyo; Kusimamisha nyongeza ya mshahara; Kufidia hasara au sehemu ya hasara ambayo mtumishi ataisababishia serikali kutokana na kukosea au uzembe wake; na Karipio.
Utaratibu wa namna ya Utekelezaji wenye ufanisi wa masuala yote yaliyokasimiwa ni kama ifuatavyo;-
i)             Wakuu wa Shule / Vyuo na Walimu Wakuu watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo na itakayokuwa inatolewa.
ii)           Mkuu wa Chuo, Shule au Mwalimu Mkuu atawajibika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu yaliyokasimiwa kwake.
iii)          Masuala yote yatakayoshughulikiwa katika mchakato ulioelezwa, ikiwa ni pamoja na vielelezo na kumbukumbu zote za vikao zitatakiwa kutunzwa vizuri kwa matumizi ya baadaye.
iv)         Katibu wa TSD Mkoa atakuwa na wajibu wa kushauri Wakuu wa Shule, Vyuo na Walimu Wakuu juu ya uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika kutekeleza majukumu waliyokasimishwa.
v)           Mawasiliano kati ya Mkuu wa Chuo/Shule, Mwalimu Mkuu na Mamlaka nyingine yatakuwa ni kwa njia ya maandishi.
vi)         Iwapo Mkuu wa Shule/Chuo au Mwalimu Mkuu atatenda kosa la kinidhamu (miongoni mwa makosa madogo madogo) au hatatoa taarifa/atakataa kutoa taarifa au ataficha baadhi ya taarifa, Katibu TSD Wilaya (Mamlaka yake ya Nidhamu) ataweza kuchukua hatua kwa kuzingatia Kanuni 43 Sehemu B ya Jedwali la kwanza la Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003.
vii)        Mafunzo/ Maelekezo kwa Wakuu wa Shule au Vyuo na Walimu Wakuu kwa kushirikiana na Waajiri yatolewe na pia kuwepo na mafunzo ya mara kwa mara.
Matarajio ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa kukasimu madaraka kwa Wakuu wa Shule, Wakuu wa Vyuo vya Ualimu / Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Walimu Wakuu ni kwamba;- Mfumo huu utasaidia kushughulikia masuala ya kiutumishi ya Walimu kwa haraka zaidi na kwa ufanisi; Badala ya kila Mwalimu kuacha kufundisha darasani kwa lengo la kufuatilia masuala yake ya kiutumishi Wilayani, sasa kutakuwa na utaratibu wa Mkuu wa Shule/Chuo au Mwalimu Mkuu kuona kuwa ni wajibu wake na kwamba atawajibika iwapo Walimu walio chini yake watakosa kupata huduma za kiutumishi.
Taarifa sahihi za Walimu zitapatikana kutokana   na Tange itakayoandaliwa katika ngazi ya Chuo/Shule. Kudhibiti udanganyifu wowote utakaofanywa na Walimu kama vile vyeti vya kughushi, viwango vya elimu, vyeo walivyonavyo. Kuhakikisha Walimu wanapata ajira rasmi na kusajiliwa ndani ya miezi mitatu tangu kuajiriwa.
Kusimamia vema zoezi la kuthibitishwa kazini na kupandishwa vyeo; Kuchukua hatua mapema kwa wanaotenda makosa ya kinidhamu; Kuamsha ari ya kazi na usimamizi wa maadili ya kazi ya ualimu kwa karibu zaidi.
Imetolewa na: 
Edwin P. Mikongoti
Naibu Katibu
 Tume ya Utumishi wa Umma
Idara ya Utumishi wa Walimu
01 Oktoba, 2013
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top