Mfanyabiashara wa madirisha ya alluminium jijini Arusha, Japhet Minja
(30), amelazwa katika Hospitali ya Selian jijini hapa, baada ya
kumwagiwa kimiminika kinachodaiwa kuwa ni tindikali usoni na watu
wasiojulikana.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana
saa 12:15 alfajiri katika eneo la Shamsi, wakati mfanyabiashara huyo
akitoka nyumbani kwake kwenda kazini.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa ndugu
zake ambaye hakutaja jina lake, alisema kuwa Minja alikumbwa na mkasa
huo wakati akienda kwenye shughuli zake za kila siku.
Alisema baada ya kufika eneo la Shamsi, Minja alikutana na vijana wanne
wakiwa wamesimama barabarani kisha walimsimamisha kama vile walikuwa
wakitaka kumuomba msaada.
“Baada ya ndugu yangu kusimama,
alishusha kioo cha gari upande wake na hapo wale vijana wakafungua
mlango kwa nguvu na kumchomoa ndani ya gari na kumtoa nje, kisha
kumshambulia kwa kumpiga na baadaye kumwagia tindikali usoni,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kumwagia tindikali wakati watu
waliokuwa karibu na eneo hilo wakikusanyika vijana hao walikimbia na
kutokomea kusikojulikana.
Alisema watu hao walimchukua Minja
na kumkimbiza hospitalini hapo kwa matibabu waandishi wa habari
walipofika hospitalini hapo kufuatilia tukio hilo, walizuiwa na uongozi
kutokana na majeruhi huyo kulazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalum (ICU)Mganga wa Hospitali hiyo, Dk. Godbless Massawe,
aliyempokea Minja hospitalini hapo kwa matibabu, alithibitisha kuwa
alimwagiwa kitu ambacho mpaka sasa hawajaweza kukibaini kwa kuwa vipimo
vya kubaini tindikali kwa nchini, vinapatikana Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH).
Dk. Massawe alisema kitu alichomwagiwa
Minja kilikuwa kinamsababishia macho yake kukosa nguvu ya kuona, kadri
muda ulivyokuwa ukienda huku kikimsababishia apate maumivu makali kwenye
ngozi ya uso.
Alisema wakati akiendelea kupatia huduma ya
kwanza, alilalamika kuwa anapata shida kuhema, wakamwekea hewa ya
oksijeni na baada yamuda alishindwa kuzungumza, lakini alianza kupata
nafuu baada ya kuendelea kumhudumia.
Dk. Massawe alisema
baada ya kupata nafuu aliweza kusema kuna wateja walikwenda nyumbani
kwake na kumuomba awauzie madirisha kwa Sh. milioni 4, lakini walimpatia
Sh. milioni 3.
Alisema baada ya kumapatia fedha hizo
waliongozana hadi barabarani na wakiwa njiani kuna watu wakazuia gari la
wateja wake na alipoamua kushuka, ndipo alipovamiwa na baadhi yao
wakaingia kwenye gari lake na kuchukua fedha zake kisha kummwagia
‘spray’ kwenye macho.
Alisema Minja aliendesha gari mwenyewe
hadi duka moja la dawa nao wakamshauri anawe uso na aliponawa aliambiwa
aende hospitalini.
Alisema alikwenda zahanati moja ambayo
hakuitaja na kushauriwa kwenda hospitali kubwa na alipofika Selian,
akaanza kujisikia vibaya na kupoteza fahamu.
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo
na kusisitiza kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kitu
alichomwagiwa mfanyabiashara huyo.
“Kitu kinachotupa mashaka
ni kimoja kuwa yule mtu aliendesha gari mwenyewe, sasa kama tindikali
utaweza kuendesha gari kweli, hivyo vitakuwa visa tu,” alisema Sabas.
Matukio ya watu kumwagiwa tindikali yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka nchini.
Masoud Mohamed Shambi, mkazi wa kisiwa cha Pemba, alikumbwa na mkasa huo mwaka 2000.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Rashid Ali Juma
(45) naye, alimwagiwa tindikali Februari 18, 2011, saa 2:30 usiku, nje
ya msikiti wa Amaan.
Novemba 5, 2012, Katibu wa Mufti wa
Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, alimwagiwa tindikali na mtu
asiyefahamika wakati akifanya mazoezi ya viungo kwenye Uwanja wa
Mwanakwerekwe.
Mwaka 2012 mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia mjini Zanzibar, Chandurali Chunilai Asawala alimwagiwa tindikali.
Mei 23, 2013, Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini
Magharibi, Mohamed Said Omar maarufu kwa jina la Kidevu, pia alimwagiwa
tindikali.
Agosti 7, 2013, saa 1:15 usiku, watu
wawili waliokuwa katika pikipiki kwenye eneo la Mji Mkongwe, Mtaa wa
Shangani, waliwamwagia tindikali mabinti wawili, raia wa Uingereza,
Katie Gee (18) na Kirstie Trup (18) waliokuwa Zanzibar wakifanya kazi ya
ualimu kwa kujitolea.
Septemba 14, 2013, Padri Ancelmo
Mwang'amba wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Cheju, alimwagiwa tindikali na
mtu asiyejulikana katika maeneo ya Mlandege.
Mwaka
1995, aliyewahi kuwa Mbunge wa Mwanza Mjini, Said Shomari alimwagiwa
tindikali na kujeruhiwa vibaya mwilini, hasa sehemu za shingoni.
Usiku wa kuamkia Julai 13, Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Said Juma
Makamba alimwagiwa tindikali wakati akiwa nyumbani kwake eneo la
Kwamrombo, Arusha.
Mwingine ni mmiliki wa maduka ya Home
Shopping Centre, Said Mohamed Saad aliyemwagiwa tindikali Julai 19,
2013, usiku wakati akiwa kwenye jengo kubwa la biashara la Msasani City
Mall.
Mwingine ni Saeed Kubenea, Mkurugenzi wa Hali Halisi
Publishers ambao huchapisha gazeti lililofungiwa la Mwanahalisi
aliyepatwa na mkasa huo Januari 7, 2008.
SOURCE: NIPASHE
on Saturday, October 12, 2013
Post a Comment