Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
akipokea ua kutoka kwa Binti Witness Mwalongo anayesoma Kidato cha
Kwanza katika Shule ya Sekondari ya Mpechi iliyopo Mjini Njombe mara tu
baada ya kuwasili Rest House mjini hapo tarehe 17.10.2013. Mama Salma
yupo Mkoani Njombe akifuatana na Rais Kikwete aliye katika ziara ya
kuutembelea mkoa wa Njombe kuanzia tarehe 17.10 hadi 23.10.2013. Chanzo:
John Lukuwi (HM)
******
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) imeahidi kukipatia kituo cha afya Lupembe na Hospitali ya
Makambako iliyopo wilayani Njombe vitanda vya kujifungulia kina mama
wajawazito viwili ili kupunguza tatizo la vifo vyao na watoto wachanga
vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alitoa ahadi hiyo jana mara baada ya
kupokea ombi la Mbunge wa jimbo la Njombe Kaskazini Deo Sanga kwa
taasisi ya WAMA ili iweze kuwasaidia kina mama wanaopata huduma katika
hospitali hizo vitanda viwili vya kujifungulia.
Akiongea kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika katika kijiji cha Wanginyi kata ya Lupembe wilaya ya Njombe
katika mkoa mpya wa Njombe Mama Kikwete alisema jitihada za pamoja
zinahitajika ili kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na
watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua vinapungua hapa
nchini.
"Nimekubali ombi la Mbunge wenu na
ninawaahidi nitawapatia vitanda viwili vya kujifungulia kina mama
wajawazito kama alivyoniomba, mimi ninataka kina mama hawa wajifungue
katika mazingira salama ili vifo vyao na vya watoto wachanga vipungue",
alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema
takwimu zinaonyesha kuwa miaka mitatu iliyopita tatizo la vifo vya
watoto chini ya umri wa miaka mitano lilikuwa juu kwani walikuwa
wanakufa watoto 578 kwa kila vizazi hai 100000 lakini hivi sasa tatizo
limepungua na kufikia vifo 454 kwa kila vizazi hai 100000
hii ni kuonyesha kuwa uongozi wa Serikali ya awamu ya nne unafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa tatizo hili linapungua.
hii ni kuonyesha kuwa uongozi wa Serikali ya awamu ya nne unafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa tatizo hili linapungua.
Mama Kikwete pia aliwataka wakazi wa
mkoa huo kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi kwani maambukizi yako juu kwa
asilimia 14.8 ukilinganisha na maambukizi ya kitaifa ambayo ni asilimia
5.1 na kusisitiza kuwa hali hiyo haikubaliki hivyo basi kila mtu achukue
hatua kwani Tanzania bila Ukimwi inawezekana.
Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya
Serikali katika mkoa huo inaonyesha kuna jumla ya Hospitali 11, vituo
vya afya 21 na zahanati 190 zinazomilikiwa na Serikali, Taasisi za dini
na watu binafsi huku idadi ya wakazi ikiwa ni 702,097 kati ya hao
wanaume ni 329,359 na wanawake ni 372,728.
Mama Kikwete ameambatana na mmewe Rais
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika ziara ya kikazi ya siku saba mkoani
humo ambapo jana Rais Kikwete amezindua mkoa mpya wa Njombe, amezindua
kiwanda cha chai cha Ikanga na kuongea na wananchi wa wilaya ya Njombe.
Chanzo: Anna Nkinda, Maelezo
Post a Comment