Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

WAZIRI MKUU AFUNGUA MAFUNZO YA MAAFISA CHINA

               


PINDA_8414e.jpg
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama vifaru na silaha nyingine za kivita wakati alipotembelea banda la kunadi silaha mbalimbali za kivita zinazotengenezwa na kampuni ya NORINCO nje kidogo ya Beijing akiwa katika ziara ya kikazi nchini China Oktoba 18, 2013.
222_99aad.jpg
Waziri Mkuu, Mizengo pinda akizungumza baada ya kutembelea kampuni ya Aluminium Corporation of China , Beijing akiwa katika ziara ya kikazi nchini China Oktoba 18, 2013. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 
......................................................................................
*Ataka viongozi wabadili mitazamo yao kuhusu sekta binafsi
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kuna haja ya taasisi za mafunzo ya uongozi za China na Tanzania kuandaa kozi zenye kuwafaa makundi fulani ya viongozi ambazo zitasaidia kubadili mwelekeo wao na utendaji wao wa kazi hasa katika masuala yanayohusu sekta binafsi.
Amesema taasisi hizo zinapaswa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP), zinapaswa kujua faida za ushirikiano huo na zinapaswa kubainisha ni sekta zipi zinapaswa kutekeleza mpango huo wa ushirikiano.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Oktoba 18, 2013) wakati akifungua mafunzo ya siku 14 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali ya Tanzania yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha utendaji wa Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ) yameanza leo kwenye Chuo cha Uongozi cha China (China Governance Academy), jijini Beijing, China.
Alisema Tanzania imefanya maamuzi ya kutumia ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP) kama njia ya kukuza na kuendeleza miundombinu, kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na ujenzi wa viwanda.
"Ni muhimu taasisi zetu hizi mbili zikatambua jambo hili na kuchangia kwa juhudi zote ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa," alisema.
Alisema kozi kama hizo zinapaswa kuwalenga watumishi kutoka taasisi za serikali pamoja na sekta binafsi na akazitaka taasisi hizo kuhakikisha zinaisaidia kuwepo kwa ufanisi wa hali ya juu kwenye ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma. "Muwasaidie watu hawa waweze kutambua ni wakati gani ushirikiano wa aina hii unakuwa wa manufaa zaidi kwa wahusika, ni wakati gani wahusika wanafaidika na PPP, je wanakabiliwa na changamoto zipi, na wanafanyaje ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza," aliongeza.
Alisema jambo lililo wazi kuwa ushirkiano baina ya wajasiriamali wa Kichina na wa Kitanzania utasaidia kuongeza fursa za kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na kuendeleza miundombinu. "Natambua kwamba kuna wafanyabiashara zaidi ya 500 wa kutoka China ambao wako nchini Tanzania, hawa wanachangia maendeleo ya kiuchumi Tanzania kwa kuingiza teknolojia mpya na kutoa fursa za ajira," aliongeza.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, alitembelea kiwanda cha aluminium cha China CHINALCO) na kiwanda cha kutengeneza zana za kijeshi ambako alionyeshwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda hivyo.Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.
Pia amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top