HOSPITALI ya Millpark ya Johannesburg, Afrika Kusini, imesema
madaktari waliokuwa wakimtibu aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi walibaini kuharibika kwa ubongo wake
kutokana na kumwagika kwa maji yanayoutunza ambayo kitaalamu yanaitwa
‘cerebrospinal fluids’ au CCF.
Msemaji wa Hospitali hiyo, Tebogo Nyembezi alisema
Dk Mvungi alicheleweshewa tiba baada ya kupata tatizo la maji hayo
yanayotunza ubongo kumwagika mara baada ya kujeruhiwa.
Dk Mvungi (61), alipata majeraha makubwa baada ya
kujeruhiwa na watu waliovamia nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya
Kinondoni, Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu. Alifariki dunia jana
mchana.
“Maji hayo ambayo ni miligramu 50 tu katika ubongo
wa mwanadamu ambayo huufanya ubongo uelee yakimwagika nusu tu, basi
mgonjwa yupo hatarini, lakini akiwahishwa na kupata tiba sahihi anaweza
kupona,” alisema Nyembezi.
Alisema iwapo mgonjwa atapewa tiba sahihi ndani ya
saa 48, ubongo wake unaweza kurudi katika hali ya kawaida, lakini saa
hizo zikizidi hawezi kupona kabisa kwa sababu maji hayo yanapomwagika
ubongo hujigonga kwenye mifupa ya sakafu yake na kuharibika kabisa.
Mtaalamu wa mishipa na neva za fahamu
(neurosurgeon) katika Hospitali ya Regency, Dar es Salaam, Dk Hariff
Najin alisema kazi kubwa ya maji hayo ni kuulinda ubongo pindi
inapotokea ajali ili usidhurike lakini endapo maji hayo yatamwagika nao
huharibika.
“Haya maji yanaufanya ubongo uelee na usielemee
kichwa. Hivyo inapotokea maji haya yakaisha au kupungua, ubongo
hujigonga na kukosa ukinzani na kuharibika,” alisema.
Alisema maji hayo ambayo hufika hadi kwenye uti wa
mgongo yakikosekana katika ubongo, husababisha damu isitembee kwenye
eneo hilo jambo ambalo pia linaweza kusababisha mishipa katika sehemu ya
nyuma ya ubongo kuharibiwa.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu Muhimbili
(Moi), Profesa Lawrence Museru alisema anachofahamu ni kuwa Dk Mvungi
alipelekwa Afrika Kusini kwa kuwa alipata madhara makubwa kwenye ubongo
na wala si kwa sababu ya kumwagika kwa maji kama ilivyoelezwa Afrika
Kusini.
“Majeraha hayo yalisababisha damu kuvilia katika
ubongo na kusababisha uvimbe ambao kwa kitaalamu unaitwa ‘traumatic
brain injury’ na sisi tulithibitisha vipimo hivyo vya awali na
kumsindikiza mpaka huko,” alisema Profesa Maseru.
Profesa Museru alisema Dk Mvungi alipata majeraha
makubwa kichwani na sehemu nyingine mwilini ambayo yanaonekana
yalisababishwa na kupigwa kwa vitu vyenye ncha kali au magongo na hivyo
kuleta madhara katika ubongo.
Alisema hawezi kuthibitisha chanzo hasa cha kifo
hicho kwani kinaweza kuwa ni kuharibika kwa ubongo au sababu nyingine
zilizotokana na tatizo hilo (secondary causes). MWANANCHI
Post a Comment