MBUNGE wa Jimbo la Bukombe, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa
Geita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Profesa Kulikoyela
Kanalwanda Kahigi (pichani) amemsifu na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuendesha nchi vizuri na
kuhangaika sana kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, Profesa Kahigi amemsifu Rais Kikwete kwa kuendesha nchi kwa
makini na kwa kusikiliza pande zote na kuwa mwenye moyo wa kusaidia
wananchi. Profesa Kahigi ametoa sifa na pongezi hizo jioni, Novemba 9,
2013 wakati alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye eneo la Stendi ya Mabasi mjini Ushirombo, Wilaya ya
Bukombe. Katika mkutano huo uliohutubiwa na Rais Kikwete akiwa kwenye
siku yake ya pili ya ziara ya Mkoa wa Geita, Profesa Kahigi amewaambia
mamia kwa mamia ya wananchi:
“Namfahamu Rais Kikwete tokea tulipokuwa pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ni mtu mwenye moyo na roho ya kibinadamu sana. Na pia napenda kumpongeza sana kwa kufanya kazi akisikiliza watu wengine na pande zote za kisiasa za nchi yetu,” amesema Profesa Kahigi na kuongeza:
“Nawaomba viongozi ambao anawateua wawe na moyo kama wa kwake. Ni jambo la furaha vile vile kwamba Serikali ya Rais Kikwete inatuletea umeme katika wilaya yetu ambayo miaka na miaka hatuna umeme. Hili halina mjadala ni jambo la pongezi sana kwako Mheshimiwa Rais kutoka kwa wana-Bukombe.”
“Ni kweli zipo changamoto na kwa kweli tutaendelea kuzisema lakini jambo jingine zuri ni kwamba hata leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga kwa kiwango cha lami. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Rais wetu amefanya kazi nzuri sana kuwalete wananchi wetu maendeleo.”
Mapema leo, Rais Kikwete amezindua Shule ya Msingi ya Nga’nzo iliyoko Ushirombo, shule ambayo imedhaminiwa na ushirika wa wachimbaji wadogo wa dhahabu wa eneo hilo la Nga’nzo na kujengwa na mwekezaji wa ndani, Ndugu Emmanuel Gungu Silanga ambaye pia ni mwana-ushirika huo.
Shule hiyo imejengwa baada ya shule ya zamani katika eneo hilo kuwa imetishiwa na wachimbaji dhahabu wadogo ambao walikuwa wanachimba katika eneo la shule ambako kwanza walikuwa wanachimba usiku lakini baadaye wakapat ujasiri wa kuchimba hata nyakati za mchana.
Shule hiyo imejengwa kwa gharama ya Sh. Milioni 460 na Rais Kikwete amewachangia wanaushirika wa wachimbaji wadogo katika eneo hilo Sh. Milioni mbili.
Pia Rais Kikwete pia amezindua Wodi ya Wazazi katika kituo cha afya cha Kijiji cha Iboya, Kata ya Mbogwe. Mradi huo umegharimu Sh. Milioni 57 na ujenzi wa wodi hiyo ni maandalizi ya kukifanya kituo hicho cha afya hospitali mpya ya wilaya mpya ya Mbogwe
Post a Comment