Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania Bw.John Muya
akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu mikakati ya mfuko huo
inayolenga kuongeza mapato yake ikiwemo ujenzi wa jengo
litakalojulikana kama kakakuona,kushoto ni Kaimu Katibu Tawala wa mfuko
huo Bi Antonia Raphael.
1. UTANGLIZI
Mfuko
wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF) ulianzishwa mwaka 1978 baada
ya kufanya marekebisho (ammendmend) ya kifungu cha 69 cha Sheria ya
Kuhifadhi Wanyamapori (Wildlife Conservation Act) Na. 12 ya mwaka 1974.
Marekebisho hayo yalitangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 21 la tarehe
22 Mei, 1981.
Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya sasa Na.5 ya mwaka 2009 inabainisha uwepo wa Mfuko kisheria katika kifungu cha 91(1).
Mfuko
ulianzishwa kwa lengo la kuiongezea Idara ya Wanyamapori uwezo wa
kifedha wa kutekeleza majukumu yake ya ulinzi wa wanyamapori. Serikali
ilitambua kuwa ulinzi wa wanyamapori unahitaji fedha nyingi na fedha
kutoka Hazina hazikidhi mahitaji yaliyopo.
Mfuko
hugharamia majukumu mbalimbali ya Idara ya Wanyamapori ikiwa ni pamoja
na uzuiaji ujangili, uendelezaji wa mapori ya akiba, usimamizi wa
matumizi ya wanyamapori, utunzaji wa kanzidata na kuwezesha watumishi
kuhudhuria mafunzo mbalimbali.
2. UZUIAJI UJANGILI
Mfuko
hugharamia shughuli za doria ndani na nje ya Mapori ya Akiba na doria
za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni pamoja na
kukabiliana na tatizo la kunguru weusi katika mikoa mbalimbali nchini.
Mfuko
hufanya malipo ya kifuta machozi kwa wananchi ambao ndugu zao wameuawa
au kujeruhiwa na wanyamapori. Aidha, Mfuko hulipa kifuta jasho kwa
wananchi ambao mashamba yao yameharibiwa na wanyamapori. Wananchi ambao
mashamba yao yameharibiwa na wanyamapori wanatakiwa kutoa taarifa kwenye
ofisi ya kijiji iliyopo karibu ndani ya siku tatu tangu uharibifu
ulipotokea. Uongozi wa kijiji husika hutoa taarifa Wilayani ili wataalam
wa kilimo na wanyamapori wafanye tathmini ya uharibifu uliotokea.
Kwa
upande wa watu wanaojeruhiwa au kuuawa na wanyamapori ni lazima
uharibifu uthibitishwe na dakatari. Aidha, ni lazima awepo shahidi
kutoka katika eneo husika ambaye si ndugu wa familia iliyoathirika ili
kuepuka udanganyifu. Uongozi wa wilaya husika hutuma maombi ya fedha za
kifuta jasho/machozi kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori. Aidha,
Afisa kutoka Makao Makuu ya Idara ya Wanyamapori hutembelea eneo husika
ili kuhakiki uharibifu uliotokea kabla ya kufanya malipo endapo kuna
haja ya kufanya hivyo. Baada ya taratibu kukamilika fedha za kifuta
jasho/machozi hutumwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika ambapo
huwapatiwa waathirika au ndugu wa familia iliyoathirika.
Viwango vya malipo ya kifuta jasho/machozi ni kama ifuatavyo:-
Kupoteza maisha (kifo) – shilingi 1,000,000/=
Ulemavu wa kudumu – shilingi 500,000/=
Kujeruhiwa – shilingi 200,000/=
Uharibifu wa mazao (kuanzia ekari 1 – 5):
Umbali wa kilo mita 0.5 kutoka eneo la hifadhi – Hakuna malipo
Umbali kuanzia kilo mita 1 – 4 kutoka eneo la hifadhi – 25,000/=
Umbali kilo mita 4 – 5 kutoka eneo la hifadhi – 75,000/=
Umbali zaidi ya kilo mita 5 kutoka eneo la hifadhi – 100,000/=
Kifo cha ng’ombe – 50,000/=
Kifo cha kondoo, mbuzi, nguruwe, punda – 50,000/=
Vifo vya wanyama wengine – 10,000/=
3. UENDELEZAJI WANYAMAPORI
Mfuko
hugharimia shughuli mbalimbali za usimamizi wa wanyamapori ikiwa ni
pamoja na usimamizi wa maeneo ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori
(WMAs), kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii, usimamizi wa maeneo ya
ardhoevu na uendelezaji wa miundombinu (nyumba za watumishi, barabara,
mipaka na viwanja vya ndege) katika mapori ya akiba.
4. UTAFITI, TAKWIMU NA MAFUNZO
Mfuko
hugharamia mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi wa Idara ya Wanyamapori
wanaosoma katika vyuo vya Mweka na Pasiansi. Pia hugharamia mafunzo ya
muda mfupi kwa watumishi wa Idara katika vyuo mbalimbali ndani ya nchi.
Aidha, Mfuko huchangia uendeshaji wa vyuo vilivyo chini ya Idara ambavyo
ni Pasiansi na Likuyu-Sekamaganga.
Pia Mfuko huchangia gharama za utafiti na kuidadi wanyamapori kupitia taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
5. MATUMIZI YA WANYAMAPORI
Mfuko
hugharamia usimamizi wa matumizi ya wanyamapori ambazo ni: ukusanyaji
wa maduhuli, usimamizi wa uwindaji wa kitalii na wa wenyeji, utalii wa
picha, biashara ya wanyamapori hai na mazao yatokanayo na wanyamapori,
mashamba na bustani za ufugaji wa wanyamapori.
6. MIRADI YA MAENDELEO YA JAMII
Mfuko
huchangia utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo kwenye jamii
zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa. Miradi hiyo ni ile ya maji, afya,
elimu na miradi ya vikundi vya wajasiriamali. Mfuko huchangia kwenye
miradi hiyo ili kuwezesha wananchi kuona faida za kuhifadhi wanyamapori.
Miradi
hiyo ni pamoja na: ujenzi wa uzio wa shule ya walemavu- Ilembula
(Njombe), ujenzi wa vyoo, mabafu na ununuzi wa vitanda- shule ya
sekondari ya Namanga (Longido), ukarabati wa bwawa katika kijiji cha
Mwakiloba- Wilaya ya Magu, ujenzi wa zahanati katika kata ya Kwadelo-
Kondoa, kuchangia ununuzi wa sare na vifaa vya shule kwa ajili ya watoto
yatima 168 katika Wilaya za Nachingwea, Kilwa, Lindi vijijini na
Liwale, ujenzi wa madarasa katika shule ya Sekondari ya Luduga- Njombe,
ununuzi wa mashine ya kusaga ya kikundi cha Enaboishu kijiji cha
Kitendeni- Wilaya ya Longido na Ujenzi wa bweni katika Shule ya
Sekondari Wiliam Lukuvi- Iringa.
7. CHANGAMOTO
Katika
kutekeleza majukumu yake Mfuko unakabiliwa na changamoto mbalimbali
kubwa ikiwa ni ufinyu wa bajeti ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo.
8. MIKAKATI
Katika
kukabiliana na changamoto hizo Mfuko unaendelea kutafuta vyanzo vipya
vya mapato zaidi ya biashara ya uwindaji wa kitalii ambao ndicho chanzo
kikuu cha mapato kwa sasa. Miradi ya maendeleo ya Mfuko imebuniwa ili
kuiendeleza kwa ajili ya kuongeza mapato ya Mfuko. Miradi hiyo ni Ujenzi
wa Jengo la Kakakuona, Pori la Akiba Pande, Bustani ya Wanyamapori ya
Tabora, Bustani ya Wanyamapori ya Ruhila (Songea) na Kambi ya Utalii
katika Pori la Akiba Selous. Miradi hiyo iko katika hatua mbalimbali za
kuiendeleza.
9. HITIMISHO
Utekelezaji
wa majukumu ya Mfuko hauwezi kufanikiwa bila nguvu ya pamoja na
ushirikiano kutoka kwa wananchi husasan katika kupambana na ujangili.
Hivyo, wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa
wanyamapori na mazingira yao kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi
kijacho cha watanzania.
Post a Comment