Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala juzi
aliwekwa kitimoto na baadhi ya wakulima wilayani Mvomero mbele ya
mawaziri wengine wanne katika mkutano ulioitishwa kutafuta suluhu ya
mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Mkindo.Makala ambaye
pia ni Mbunge wa Mvomero ulipo mgogoro huo, alilalamikiwa na wakulima
hao wakidai kwamba amekuwa akiwasikiliza zaidi wafugaji na
kutoonyesha jitihada za kumaliza tatizo hilo.Mawaziri wengine
waliohudhuria mkutano huo kwa agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza, Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Gudluck Ole-Medeye.
Akijibu
shutuma zilizoelekezwa kwake, Makala alisema: “Msiseme tu mwangalie na
juhudi zangu. Namshukuru Dk Nchimbi kwa kusoma barua ya Waziri Mkuu,
uongo umejitenga na ukweli umedhihirika. Mimi nikiwa mbunge ni
mwakilishi wa wananchi, nimewaita mawaziri hapa, nimekuwa kama mshenga
ili wasikie malalamiko yenu,” alisema Makala.
Malalamiko ya wananchi
Katika
malalamiko yao, wakulima hao walisema licha ya uonevu wanaoupata kutoka
kwa wafugaji na Jeshi la Polisi, mbunge wao amekuwa kimya.
“Mbunge
wetu hatusaidii kitu kila tunapopata matatizo. Yalipotokea machafuko
Kijiji cha Hembeti hakuonekana. Kuna taarifa zisizo rasmi kuwa amekuwa
akifanya mapatano na wafugaji kwa siri,” alisema mmoja wa wanakijiji wa
Mkindo, Shomari Msumi na kuongeza:
“Watoto
wetu wamelazwa Hospitali ya Bwagala, Polisi wamekuja kuwafunga pingu na
kuondoka nao, wafugaji hawaguswi kwa sababu ya nguvu ya fedha. Vyombo
vya Dola hasa Mahakama nayo inatukwamisha. Mazao yameliwa lakini kesi
haziamuliwi, hadi leo kesi iko wilayani.”
Mkulima
mwingine, Aziz Dendego alisema: “Tunaumizwa mno na viongozi wa wilaya.
Mimi nimefika hapa mwaka 1975. Kero zimeanza miaka 20 iliyopita na
Serikali ndiyo inayosababisha. Mkuu wa Mkoa anaagiza tu lakini hatuoni
vitendo. Mkuu wa wilaya alikuwa mzuri lakini sasa amebadilika kabisa.
Bunduki za kijeshi zimetumika kwenye mapigano, wakulima wamezipataje?”
Mmoja wa
wakulima hao, Shaaban Khamis alisema wameamua kuunda vikundi vya ulinzi
shirikishi baada ya kulalamika kwa muda mrefu bila kusikilizwa.
Wakulima
hao pia wamemlalamikia Mwenyekiti wa Kijiji cha Wafugaji cha Kambala
waliyemtaja kwa jina moja la Kashu wakidai kuwa amekuwa akiongoza
mapigano dhidi ya wakulima.
Hata hivyo, Kashu hakuhudhuria mkutano huo ambao wafugaji waliwakilishwa na mfugaji mmoja tu, Majuka Koila.
“Watu
wameuawa, nyumba 380 zimechomwa moto na wafugaji katika Kijiji cha Kwa
Mbogo, hadi leo hakuna aliyekamatwa,” alisema Hassan Said.
Mawaziri wamtetea
Licha ya
Dk Mathayo kuahidi kujenga majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo,
alimtetea Makala kuwa amekuwa akimsumbua kuhusu matatizo ya wakulima.
“Makala anakaa nyuma yangu pale bungeni, amekuwa akinisumbua sana. Mbunge wenu anawapenda,” alisema na kuongeza:
“Lazima
wafugaji wafuate sheria na utaratibu. Matatizo haya yanatokana na
ukosefu wa miundombinu hasa malambo na majosho. Tutayajenga ili wafugaji
wasiingie kwa wakulima.”
Huku akimtetea Makala, Naibu Waziri, Ole-Medeye alitaja mikakati mitatu ya Serikali.
“Mnyonge
mnyongeni lakini haki yake mpeni. Shetani kazi yake ni kusababisha vita
na ugomvi kati ya ndugu na ndugu. Makala amenisumbua sana. Migogoro
mingi imekuwapo kabla hata hajaingia madarakani. Kwa mfano, mgogoro huu
wa Bonde la Mgongola umeanza mwaka 2005, Makala alikuwepo?”
Kuhusu
utatuzi wa mgogoro huo, Ole Medeye alisema amemwagiza Katibu Mkuu wa
wizara hiyo kumaliza suala hilo nje ya mahakama ili kuleta suluhu.
Mkuu wa
Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka alipojaribu kumtetea kwa kuwauliza
wananchi kama Waziri Makala ameshawatembelea mara ngapi, Mwenyekiti wa
Kijiji cha Mkindo, Ally Shamte alisema amefika mara moja tu tangu
achaguliwe.
Waziri
Chizza alikiri kuwa kero za wakulima zinatokana na kutopewa majibu
haraka... “Lipo tatizo la kutotoa majibu haraka. Tunao mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN), tunapaswa kutoa majibu sasa siyo kusubiri matukio.
Tusingependa kuja hapa baada ya watu kufa, maana hatuwezi kuwafufua,”
alisema Chizza.
Makala ajitetea
Baada ya mawaziri hao kujieleza, Chizza alimpa nafasi Makala ambaye alieleza kwa kina jinsi alivyoshughulikia migogoro hiyo.
“Ulipotokea
mgogoro wa Kijiji cha Lukenge, nilikaa na wafugaji wa Kijiji cha
wafugaji cha Sokoine na siku hiyohiyo nilikaa na wakulima wa Kijiji cha
Sigaju. Siku walipofunga barabara nilikuwa mkoani Iringa kwenye sherehe
za kuzima Mwenge. Watu wanafanya siasa, wengine wananipigia simu na
kuniuliza niko kijijini, hayo ni mambo ya siasa tu,” alisema na
kuongeza:
“Mgogoro
wa Bonde la Mgongola tumekuja pale wakatoa tamko, shamba la Kijiji cha
Begi hakuna mwanasiasa yeyote aliyeshughulikia zaidi yangu. Nimekaa pale
hadi saa mbili usiku. Hata wale vijana waliosingiziwa kesi nimetoa
fedha yangu mfukoni kuwatoa.”
Dk Nchimbi awajia juu polisi
Licha ya
kumtetea Makala, Dk Nchimbi alishangazwa na Jeshi la Polisi mkoani humo
kutowakamata wafugaji waliohusika katika mapigano hayo.
“Binafsi
sijaridhishwa na idadi ya wafugaji waliokamatwa. Haiwezekani wauawe watu
sita, wakulima wanne na wafugaji wawili halafu wakamatwe wakulima 32 na
wafugaji wawili. Hakikisha unafanya operesheni ya kuwakamata
waliohusika,” alisema Dk Nchimbi.
Awali,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alikanusha
kuwa bunduki zilizotumika kwenye mapigano hayo zilikuwa za kijeshi.
“Baada
ya tukio, maganda yaliyookotwa yalikuwa ya bunduki za aina ya ‘shot gun
na rifle’. Hata yule mfugaji aliyeuawa bunduki yake imesalimishwa siyo
ya kijeshi,” alisema.
Post a Comment