Na Hassan Abbas
Mpango
wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) umemuomboleza Rais wa
kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela kwa kumtaja kuwa
ni kiongozi wa mfano. Mandela (95) alifariki usiku wa Alhamisi iliyopita
baada ya kupambana na maradhi na umri mkubwa.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na makao makuu ya APRM yaliyoko mjini
Midrand, Afrika Kusini, kifo cha Mandela ingawa kimeliachia Bara la
Afrika huzuni kuu lakini Mzee Mandela anapaswa kushukuriwa kwa mambo
makubwa aliyoyafanya kwa ajili ya binadamu.
“APRM
ingependa kuwasilisha salamu zake za rambirambi kwa watu wa Afrika
Kusini, familia, marafiki, wenzetu wengine katika Bara la Afrika na
dunia kwa ujumla, kufuatia kifo cha Nelson Rholihlahla Mandela, Rais wa
zamani wa Jamhuri ya Afrika Kusini,” ilisema taarifa hiyo.
APRM
katika taarifa yake hiyo pia imesisitiza kuwa wakati Bara la Afrika na
dunia vikiwa katika huzuni, Mpango huo unaungana na dunia katika
kuomboleza na kuzikumbuka siku za maisha yake.
“Taasisi
hii ya Afrika inaungana na dunia kuzitafakari harakati za Mandela na
hasa uongozi wake madhubuti na usioyumba na kujitoa kwake katika
kupigania maendeleo ya mwanadamu,” iliongeza taarifa hiyo.
APRM
imetumia rambirambi hizo kusisitiza na kutambua mchango usio na kifani
wa Mandela katika ukombozi wa Afrika Kusini. Taarifa inasema:
“Tunamshukuru kwa harakati zake zisizo za ubinafsi za kuhakikisha Afrika
Kusini na dunia kwa ujumla inakuwa huru.”
Enzi
za uhai wake Mzee Mandela atakumbukwa kwa kupigania uhuru, kupiga vita
ukandamizaji na ubaguzi wa rangi hadi alipofanikiwa kuushinda mfumo
dhalimu wa kikaburu.
Pamoja
na kwamba katika sehemu kubwa maisha yake tangu alipostaafu siasa Mzee
Mandela alilazimika kupumzika zaidi kutokana na umri na maradhi bado
mara kadha alishiriki katika jitihada mbalimbali za kuimarisha utawala
bora Afrika ikiwemo kushiriki shughuli za APRM.
Mzee
Mandela atakumbukwa mwaka 2007 kwa uamuzi wake wa kuambatana na mkewe,
Graca Machel, kwenda nchini Kenya wakati wa tathmini ya APRM kuhusu
utawala bora nchini humo.
Wakati
Mama Graca alikuwa ndiye kiongozi wa jopo la wataalamu waliokwenda
kuitahmini Kenya inavyotekeleza misingi ya APRM, Mzee Mandela aliona
kuwa hiyo ni miongoni mwa fursa adimu na za kipekee kwake kushuhudia
Afrika inavyopambana na changamoto zake za maendeleo.
Akiwa
nchini Kenya katika ziara hiyo ya APRM, Mzee Mandela alinukuliwa
akisisitiza kuwa angependa kabla ya kifo chake kuliona Bara imara zaidi
la Afrika na linaloheshimu misingi adhimu ya utawala bora.
Post a Comment