Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Goodluck Ole-Medeye
(katikati), akiongoza wahitimu wa Mahafali ya 15 ya Chuo cha Uhasibu
Arusha (AII) kuelekea kwenye viwanja vya chuo hicho, muda mfupi kabla ya
kuwatunuku vyeti kwenye fani mbalimbali mkoani humo mwishoni mwa wiki,
wa kwanza ( kushoto) ni Mkuu wa Chuo hicho Prof Johannes Monyo, na
Mwenyekiti wa Bodi ya uongozi wa (AII), Mwanaidi Mtanda.
Wahitimu
wa Chuo cha Uhasibu Arusha (AII), wakivaa kofia zao muda mfupi baada ya
kutunukiwa vyeti vya fani mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo, kwenye
sherehe za mahafali ya 15 zilizofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho
mwishoni mwa wiki.
Kukithiri
kwa vitendo vya rushwa na ubinafsi ndani ya idara na taasisi za
serikali nchini kumeelezwa kuwa ni chanzo na ‘mwiba’ unaorudisha nyuma
juhudi na mipango madhubuti inayofanywa kila siku na serikali dhidi ya
wimbi la umasikini
Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Goodluck Ole-Medeye,
ameyasema hayo mkoani hapa, mwishoni mwa wiki, wakati akihutubia kwenye
sherehe za mahafali ya 15 ya Chuo cha Uhasibu Arusha
“Sehemu
ya fedha za walipakodi huishia kwenye midomo ya walafi wachache ambao
baadhi yao ni viongozi wasio waadilifu wenye dhamana ya kusimamia
miradi ya maendeleo ya taifa letu ,” alisema Medeye na kuongeza:
“Nawaomba
wale watakaobahatika kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
wasimame imara na kusema kwa sauti moja kuwa rushwa itamkwe na Katiba
kuwa adui wa Taifa na hivyo katiba iweke adhabu kali kwa
watakaojihusisha nayo.”
Aliwataka
wahitimu na wadau wengine kushirikiana kutoa elimu juu ya ubaya wa
rushwa kwa mustakabali mzuri wa amani ya taifa ili kufikia maendeleo ya
kijamii, kiuchumi na upevu wa kisiasa wanaoutarajia
Katika
hatua nyingine Dk Medeye aliwaasa wanafunzi wote nchini hususan wale
wanaotoka vyuoni kutumia fursa ya teknolojia ya habari na mawasiliano
(Tehama) katika ushindani wa soko la ajira la Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kimataifa kwa kusoma na kujua mambo mengi ya kiweledi.
“Tumieni
simu na kompyuta zenu kutafuta taarifa za kiushindani kitaifa na
kimataifa na hasa ushindani wa soko la ajira msiitumie mitandao hiyo
vibaya..tumieni kwa kupata vitabu, majarida na taarifa za utafiti zenye
manufaa kwenu kimasomo,” alisema
Alisikitishwa
na vitendo vya wanafunzi walio wengi kutumia vibaya fursa ya Tehama,
kwa kutafuta taarifa zilizo kinyume na maadili ya taifa au kupiga gumzo
‘kuchat’ hususan wanapokuwa wakiperuzi mitandao ya kijamii ikiwemo
Twitter, Google na Facebook
Naye
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa (IAA), Mwanaidi Mtanda, alisema chuo
hicho kina mpango wa kufungua kampasi nyingine mkoani Mwanza, na pia kwa
sasa kipo kwenye maandalizi ya kufungua kampasi mjini Babati-Manyara,
lengo ni kutoa fursa kwa watanzania katika muktadha wa ongezeko la ubora
wa elimu na idadi ya wanafunzi.
Aliongeza
kuwa Chuo hicho cha Uhasibu kwa mwaka huu kimeanzisha Stashahada za
Uzamili za Uhasibu, na Ugavi na Manunuzi. Pia kwa kushirikiana na Chuo
Kikuu cha Conventry cha Uingereza, na kile cha Galgotias nchini India
tayari wameanza kutoa kozi mbalimbali zikiwemo Stashahada na Shahada za
Uzamili kwa masomo ya kutwa na jioni
Aidha
katika hali ya kusisitiza, Mtanda aliomba serikali kuongeza kasi katika
kusaidia kutatua changamoto za uhaba wa mabweni na vyumba vya madarasa.
“Kama
tunavyosikia kwenye vyombo vya habari usalama wa wanachuo katika vyuo
vikuu mbalimbali nchini upo hatarini, majambazi yanawavamia wanavyuo,
yanawapora, kuwaibia, kuwajeruhi au wakati mwingine kuwaua,” alisema.
Awali,
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Johannes Monyo, alisema jumla ya wanafunzi
1,510 wamehitimu na kutunukiwa vyeti katika fani mbalimbali zaidi ya 29,
zikiwemo za Benki, Ugavi na Manunuzi, Uhasibu, Kodi, Usimamizi wa
Fedha, Sayansi ya Komputa na Teknolojia ya Habari.
Post a Comment