Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba
(pichani) amesema mchakato wa Katiba Mpya una vikwazo vingi na kwamba Katiba
haiwezi kupatikana mwaka 2014 kama Rais Kikwete alivyoahidi hivyo, kuna
haja ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Bara.
Hii ni mara ya pili kwa Lipumba kutoa kauli hiyo.
Mei mwaka huu, alitoa tamko kama hilo alipoonyesha wasiwasi wake kuhusu
upatikanaji wa Katiba Mpya akadai ni janja ya CCM kumwongezea muda Rais.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Lipumba
alisema kuwa amekuwa akiutafakari kwa kina mchakato wa Katiba Mpya kama
unaweza kukamilika mwaka 2014, lakini jibu linalomjia, hakuna.
Alitaja baadhi ya vikwazo ambavyo vinaweza
kukwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya kuwa ni Daftari la Kudumu la
Wapigakura kama halijaboreshwa na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho
vya utaifa ambavyo vitatumika kupigia kura hiyo.
Wakati Profesa Lipumba akisema hayo, tayari Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeeleza kuwa haina mpango kwa sasa wa
kuboresha Daftari la Kudumu Wapigakura kwa ajili ya kura za maoni kwa
sababu muda uliobaki ni mfupi.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva
alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, kuwa itakuwa vigumu
kuliboresha daftari hilo kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni
utakaofanyika mwanzoni mwa mwaka 2014 kwa sababu muda uliobaki ni mfupi
na hakuna fedha za kufanya hivyo.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge) William Lukuvi alipoulizwa bungeni mwisho mwa wiki
kuhusiana na kauli ya Jaji Lubuva alisema msimamo uliotolewa na Waziri
Mkuu kuhusiana na daftari hilo ndiyo msimamo hasa wa Serikali.
Desemba 5, mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
alivihakikishia vyama vya siasa na Watanzania kwamba Daftari la Kudumu
la Wapigakura litaboreshwa kabla ya upigaji kura ya maoni kuhusu Katiba
Mpya ya Tanzania.
Waziri Mkuu alisema hayo wakati akihitimisha
hotuba yake ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013, ambapo
suala la Daftari la Wapigakura liliibua mvutano mkali baina ya wabunge
na Serikali.
Profesa Lipumba alisema kuwa kutokana na hali
ilivyo sasa ni wazi kwamba Katiba Mpya haiwezi kupatikana kabla ya mwaka
2015, hivyo kuna haja ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili
kushughulikia mchakato wa Katiba na kuimarisha uwajibikaji wa vyombo vya
dola.
“Ni wazi kwamba hatuwezi kupata Katiba mpya
ifikapo Aprili 26, wakati tunasherehekea miaka 50 ya Muungano, kwani
bado mchakato huu ni mrefu na unahitaji muda wa kutosha,” alisema
Profesa Lipumba na kuongeza:
“Rasimu ya mwisho ya Tume ya Katiba itapatikana
mwezi huu, huku na Rais anawajibika kukamilisha undaji wa Bunge la
Katiba kwa kuteuwa wabunge 201 baada ya kupata mapendekezo, hivyo
itakuwa bahati Bunge la Katiba kuanza mwisho wa mwezi Januari kitu
ambacho kinarefusha mchakato huu.”
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment