Bwana Harusi Fadhili Mahenge akiwa ndani ya Suti akisubiri kufungishwa ndoa |
Bi Harusi Naomi Ngoje akiwa amejilalia chumbani akisubiri hatima ya Wazazi ndipo ajiandae kwenda kanisani tayari kwa kufunga ndoa na mchumba wake waliodumu kwa miezi saba. |
Bwana harusi akiwa na mpambe wake kanisani wakimsubiri bibi Harusi |
Askofu Kenani Mpalala akiwa katika picha ya pomaja na Bwana Harusi na mpambe wake muda mfupi baada ya kuwasili kanisani |
Askofu Keenan Mpalala wa kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania akionesha tangazo la Ndoa |
Baadhi ya ndugu wa mwanamke wakiwa katika kikao na kuendelea na msimamo wao kuwa mahali lazima imalize ndipo wamtoe binti yao |
Jamaa wameshika vichwa hali haieleweki |
Baadhi ya akina mama wakiangalia ratiba ya harusi |
Kanisani |
Baadhi ya waumini na majirani wakisubiri kanisani |
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Familia
moja ya Makunguru Mtaa wa Ilolo Jijini Mbeya imesababisha sintofahamu
dhidi ya Familia nyingine baada ya kumkatalia binti yao kuolewa kwa madai ya
waoaji kutokamilisha Mahari waliyokuwa wamepangiwa.
Tukio hilo la aina yake limetokea leo
ambapo Bwana harusi aliyefahamika kwa jina la Fadhili Mahenge(28) Mkazi wa
Songea aliyekuwa amuoe Naomi Ngoje na harusi yao kufungwa katika kanisa la Free
Pentecoste Church Of Tanzania(FPCT) lililopo Makunguru Jijini hapa kushindwa
kufungwa baada ya wazazi wa Bibi harusi kuzuia ndoa hiyo hadi Mahari
itakapokamilika.
Wakizungumzia tukio hilo Nyumbani kwa
Familia ya Bibi Harusi, Mjomba wa Bibi Harusi Dickson Ngoje amesema tatizo la
wao kugomea ndoa hiyo ni kutaka waoaji kutimiza masharti waliokuwa
wamekubaliana awali ambayo hadi siku ya mwisho familia hiyo haijatekeleza.
Amesema siku ya kwanza waoaji walifika
Nyumbani kwa Mzee Ngoje na kujitambulisha ambapo walipangiwa taratibu za mahari
kwa mujibu wa Mila kuwa watatakiwa kutoa Blanket 2, Mashuka mawili,
Mkaja(200,000), mbuzi 4, Majembe 4, Ng’ombe Jike 2 na Ngo’mbe Dume 1 pamoja na
fedha taslimu Shilingi Laki 3.
Amesema baada ya Familia hiyo ya Waoaji
ambao ni Ukoo wa Mahenge kupangiwa vitu hivyo waliondoka na kuahidi kurudi siku
nyingine kwa ajili kukamilisha vitu walivyopangiwa ambapo walirudi Septemba 11,
Mwaka huu wakiongozwa na Mshenga aliyejulikana kwa jina moja la Mzee Katete
wakiwa na Blanketi 2, Mashuka mawili pamoja na Fedha shilingi 10,000/= ambazo
walizipokea na kuwaambia hawawezi kuzungumza chochote juu ya Ndoa.
Mjomba huyo anaongeza kuwa baada ya wiki
mbili familia hiyo ilirudi na kukuta Nyumbani kuna ukoo mzima wakiwa na
Shilingi 200,000/= ndipo walipoambiwa walipe kiingilio shilingi 100,000/= ndiyo
wanaweza kupokelewa nyumbani jambo ambalo walilitekeleza kisha kulipa fedha
walizokuwa nazo kama Mkaja na kuomba wapewe kibali cha kuandikisha ndoa na
taratibu za kumalizia vilivyobaki zikiendelea.
Anasema tangu hapo Ndoa ilianza
kutangazwa Disemba 8 na kuisha Disemba 22, Mwaka huu baada ya kutangazwa mara
tatu huku tangazo likiashiria ndoa kufungwa tarehe 28/12/2013 ambapo wazazi
wakiahidi kumalizia Mahari iliyobaki kabla ya siku ya kufunga ndoa.
Akizungumzia kwa kirefu kashishe hiyo,
Mjomba huyo anasema baada ya wazazi wa Mwanaume kusisitiza kumaliza kila kitu
hadi ifikapo Disemba 23, Mwaka huu na wao walijikusanya na kupanga taratibu za
sherehe hususani ya kumwaga binti yao(Send Off) ambayo ilifanyika Disemba 24,
Mwaka huu.
Aidha baadhi ya ndugu wameongeza kuwa
familia hiyo haioneshi uaminifu wa kumalizia Mahari hiyo kutokana na ahadi
zisizotekelezeka walizotoa tangu kipindi cha nyuma na kuongeza kuwa hata kwenye
sherehe ya kumwaga binti yao walifika baadhi ya ndugu wakiwa na Zawadi tofauti
na taratibu zinavyotaka.
Wamesema kwa mujibu wa taratibu za
Sherehe za SendOff upande wa Mwanaume unatakiwa kuleta zawadi ambazo ni
nguo za Bibi Harusi za kuvaa siku ya Ndoa Pamoja n Harusi lakini wao
hawakufanya hivyo ingawa walikuwa na Nguo ambazo tayari zilikuwa zimetumika.
Kwa upande wa Mchungaji aliyekuwa
anataka kufingisha Ndoa hiyo ambaye pia ni Askofu wa Kanisa hilo, Mchungaji
Kenan Mpalala alipoulizwa kuhusu hali hiyo amesema kwa mujibu wa taratibu za
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 8 pingamizi litolewe ndani ya siku 21.
Amesema upande wa Wazazi wa Mwanamke
ulishindwa kuwasilisha pingamizi lao kanisani kabla ya Siku 21 badala yake
walifika kutoa malalamiko kuhusu kutomaliziwa kwa mahali jambo ambalo alisema
yeye kama Mwandikisha Ndoa halimhusu bali pande mbili wanatakiwa kulimaliza
kabla ya Ndoa.
Naye Bwana Harusi Mtarajiwa Fadhili
Mahenge(28) alipoulizwa kuhusiana na suala hilo huku akiwa tayari Kanisani kwa
ajili ya Kufungishwa Ndoa alisema anachosubiri ni hatma ya Wazazi wa Mwanamke
kama wanaweza kumwachia Mkewe iliwanachodai awe anamalizia taratibu.
Amesema yeye kama yeye kwa sasa hana
fedha zozote za kuweza kumalizia anachodaiwa zaidi ya kuomba busara za wazazi
wa Mwanamke kumruhusu Ndoa ifungwe ndipo aweze kulipa Mahari anayodaiwa kwa
awamu kutokana na hali yake ya kiuchumi kuwa Mbaya.
Ameenda mbali zaidi kwa kusema kama
Wazazi wa Mwanamke wataendelea kuwa na Msimamo huo basi hata yeye ataomba
arudishiwe kile alichokitoa awali ili ajipange upya kwa ajili ya ndoa baada ya
kukamilisha madai yao.
Hadi tunaingia mtamboni Mbeyayetu ambayo
ilikuwepo sehemu ya tukio timu ya usuluhishi ilikuwa ikiendelea na kazi yake
ikiongozwa na Mchungaji, Mwenyekiti wa Mtaa na Mzee Maarufu ambaye ni Katibu wa
Chama cha Wakulima (TASO) kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ramadhani Kiboko, huku
muafaka ukiwa haujapatikana.
Na Mbeya yetu
Na Mbeya yetu
Post a Comment