********
Wakati Serikali ikisema Daftari la Kudumu la Wapigakura
litaboreshwa kwa ajili ya kura za maoni ya Katiba Mpya, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) imesema haina mpango huo kwa sababu muda uliobaki ni
mfupi.
Badala yake Nec imesema inajiandaa kuboresha
daftari hilo kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili kuingiza wale wote waliotimiza miaka 18
baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva
alisema jana kwamba itakuwa vigumu kuliboresha daftari hilo kwa ajili ya
upigaji wa kura za maoni utakaofanyika mwanzoni mwa mwaka 2014 kwa
sababu muda uliobaki ni mfupi na hakuna fedha za kufanya hivyo.
“Muda uliobaki kwa ajili ya upigaji wa kura za
maoni ni mfupi, itakuwa vigumu kwa tume kuliboresha daftari la
wapigakura nchi nzima ila tunajiandaa kuliboresha kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema nchi ni kubwa kijiografia kiasi kwamba
unahitajika muda mrefu kwa ajili ya kuliboresha daftari hilo na kwa vile
zoezi la upigaji kura za maoni litafanyika mwanzoni mwa 2014, tume
itakuwa imechelewa kufanya hivyo.
Kauli ya Serikali
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi alipoulizwa jana mjini Dodoma kuhusu tamko la
Jaji Lubuva, alisema msimamo uliotolewa na Waziri Mkuu wiki iliyopita
ndio msimamo wa Serikali.
“Serikali tunajiandaa, na wao (NEC) wanajua fedha
za mwanzo tumeshapeleka na mchakato umeanza. Wameshakagua mashine
zitakazotumika….process (mchakato) hii yote inalenga kura ya maoni,”
alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Lukuvi alisema inawezekana kauli ya
Rais Jakaya Kikwete kwamba Katiba Mpya itapatikana Aprili 26, mwaka huu
ndiyo inayowachanganya, wanaona muda uliopo ni mfupi lakini hilo ni la
Serikali na siyo tume.
Desemba 5, mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
alivihakikishia vyama vya siasa na Watanzania kwamba Daftari la Kudumu
la Wapigakura litaboreshwa kabla ya upigaji kura ya maoni juu ya Katiba
Mpya. Hali kadhalika Pinda alisema Serikali itatumia daftari hilo la Nec
katika upigaji kura ya maoni ya katiba kwa pande zote za Muungano.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati akihitimisha hotuba
yake ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 ambapo suala
la daftari la wapiga kura lilibua mvutano mkali. Wabunge wa Tanzania
Bara walitaka daftari la wapiga kura liboreshwe kwanza, huku wale wa
Zanzibar wakitaka wasio na vitambulisho vya ukaazi waruhusiwe kupiga
kura kwa kutumia daftari la Nec.
MWANANCHI
Post a Comment