RC MANYANYA |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali
Mkoani Rukwa inapenda kukanusha taarifa iliyotolewa na gazeti la Jambo
Leo toleo namba 1546 la tarehe 3, Disemba 2013 iliyoandikwa na Mwandishi
Gurian Adolf katika ukurasa wa 10 iliyokuwa na kichwa cha habari “TCCIA
Rukwa yaomba mbolea ya DAP”.
Sehemu
ya taarifa hiyo ilieleza kuwa; Nanukuu “Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Rukwa, Shadrack
Malila ameiomba Serikali kuwashauri wakulima wa Mkoa huo kutumia mbolea
nyingine ya kupandia mahindi badala ya mbolea ya minjingu ambayo
haijafanyiwa utafiti katika Mkoa huo.”
Kwa
mujibu wa gazeti hilo taarifa hiyo aliitoa mbele ya waandishi wa habari
Ofisini kwake mjini Sumbawanga ambapo aliongeza kuwa “Tangu awali
wakulima hao walikataa mbolea hiyo, baada ya kuitumia kupandia na
kushindwa kustawisha vizuri mazao yao ya mahindi, tofauti na mbolea ya
DAP ambayo husaidia kupatikana kwa mazao mengi”. Mwisho wa kunukuu.
Serikali
Mkoani Rukwa inapenda kukanusha kuwa sio kweli kwamba mbolea ya
minjingu haijafanyiwa utafiti kufaa kutumika katika Mkoa huu na kwamba
haijapokea malalamiko yeyote yaliyo rasmi kutoka kwa wananchi (wakulima)
juu ya ubora na ufanisi wa mbolea hiyo. Matokeo yake yameonekana kuwa
ni mazuri hususani baada ya mbolea hiyo kuboreshwa zaidi na sasa inaitwa
“Minjingu Mazao”.
Napenda
ifahamike wazi kuwa tafiti mbalimbali za udongo zimefanyika Mkoani
Rukwa mfano, taarifa ya BRALUP, 1977, Tafiti za udongo zilizofanywa na
Kituo cha Utafiti cha Uyole na Sampuli mbalimbali zilizopelekwa Chuo
Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kutoka Halmashauri ya wilaya ya Nkasi
miaka ya 2008-2010 na kuonesha sehemu kubwa ya udongo wa maeneo ya
Uwanda wa juu wa Ufipa (Ufipa Plateau) kuna upungufu mkubwa wa
kirutubisho cha aina ya Naitrojeni kulingana na mahitaji yake kwa mimea
jamii ya nafaka, hasa mahindi chotara.
Aidha,
majaribio ya kutumia aina na viwango mbalimbali vya mbolea kwa zao la
mahindi ikiwemo Minjingu yamefanywa kupitia Kituo Kidogo cha Utafiti cha
Uyole kilichokuwa wataalam huko Nkundi na mashamba ya majaribio sehemu
mbalimbali na kutoa matokeo yaliyofanyiwakazi. Kufuatia majaribio hayo,
Mkoa wa Rukwa ulitoa mapendekezo kwa kampuni ya Minjingu Mines &
Fertilizer ya kubadilishwa kwa umbile la mbolea ya Minjingu kutoka
katika umbile la unga (powder form) na kuwa katika umbile la sasa
la chengachenga ili kuwa rahisi wakati wa kuweka mbolea shambani. Pia
Mkoa ulipendekeza mbolea hiyo iwekewe kirutubisho aina ya Nitrojeni ili
kukidhi mahitaji ya udongo wa sehemu kubwa ya Ukanda wa juu wa Ufipa,
mapendekezo ambayo yamezingatiwa zimefanywa na matokeo yake kuonekanika.
Mashamba
Darasa yanayohusisha mbolea ya Minjingu Mazao yameanzishwa na
kuendeshwa sehemu mbalimbali za Mkoa katika msimu uliopita wa 2012/2013
na kukaguliwa na Viongozi kuona ufanisi wake. Yapo mashamba yaliyofanya
vizuri na yapo ambayo hayakufanya vizuri. Hali ya tofauti kama hiyo
hutokea kwa aina zote za mbolea zinapotumika katika maeneo tofauti. Ikumbukwe kuwa ardhi ipo hai na hutofautiana kutoka sehemu moja na nyingine!
Tafiti
nyingi zimeonesha kuwa wakulima wengi wameshindwa kupata matokeo mazuri
katika kilimo kwa kushindwa kufuata masharti ya wataalam wa kilimo hata
kama wakitumia mbolea ya aina yeyote. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa
na Profesa Kauzeni na wenzake katika vijiji vya Ntendo na Mtimbwa mwaka
1998, pamoja na mambo mengine ilibainika kuwa wakulima wachache
waliomudu kutumia mbolea au mbegu bora hawakuzingatia viwango
vilivyopendekezwa na wataalam. Walitumia karibu nusu tu ya mapendekezo,
Mfano Hekta moja iliyopandwa mahindi zilitakiwa kutumia kilo 125 za TSP Triple Super Phosphate ( P2O5 )18% na kilo 250 za UREA (N) 46%,
ili kuvuna tani sita za mahindi sawa na kilo 6,000 au wastani wa
magunia 60 kwa hekta. Waliofanya vizuri kidogo walitumia kilo 100 tu za
TSP na kilo 100 za UREA.
Kufuatia
taarifa hiyo, Uongozi wa Mkoa wa Rukwa haupendi kuingilia uhuru wa mtu
wa kupata na kutoa habari kama Mtanzania mwingine yeyote. Ni vema mtu
akatoa taarifa anazozifahamu vizuri/zilizofanyiwa utafiti, zisizoleta
mtafaruku au kuipotosha jamii na zisizolenga kuvutia maslahi binafsi kwa
namna yeyote ile.
Serikali
ya Mkoa imesikitishwa na taarifa aliyoitoa Bwana Malila. Ni dhahiri
kuwa ametumia vibaya nafasi yake ya uenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Rukwa
kuwashawishi wakulima wa Mkoa huu kuwa mbolea ya Minjingu haifai na
haitowapa mavuno mazuri. Ikumbukwe kuwa Bwana Malila ambae ni msambazaji
wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali katika Manispaa ya Sumbawanga kwa
mwaka huu 2013/14 pia ni mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo ikiwemo
mbolea anayoipigia chapuo ya Diammonium Phosphate maarufu kama DAP.
Ifahamike
pia kuwa Bwana Malila aliwahi kuwa na Mkataba na Kampuni ya Minjungu
Mines & Fertilizer Ltd katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/2010.
Kama kweli mbolea hiyo haifai mbona aliwahi kuwa wakala na akaisambaza
kwa wakulima bila kutoa matamko kama haya? Ni dhahiri kuwa taarifa yake
hiyo ina mgongano wa kimaslahi na hailengi katika kuboresha kilimo kwa
wananchi wa Mkoa wa Rukwa.
Imetolewa na
Albinus Mugonya,
Kaimu Katibu Tawala Mkoa,
RUKWA.
10 Disemba, 2013
Post a Comment