Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari (Hawapo pichani) noti
bandia zenye thamani ya Tsh 6,140,000 ambazo zilikamatwa maeneo ya Kituo
kikuu cha Mabasi cha jijini hapa ambapo mtuhumiwa alikuwa anataka
kuzisafirisha kwenda Dar es salaam. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha)
………………………………………………………………………….
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa
limemkamata mwanamke mmoja aitwaye Imelda Juma (20) Mkazi wa Sokoni One
jiji hapa akiwa na noti bandia zenye thamani ya Tsh 6,140,000 (Milioni
sita laki moja na elfu orobaini).
Akiongea
na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema
kwamba tukio hilo lilitokea tarehe 13.12.2013 muda wa saa 10:00 Alasiri
katika maeneo ya Kituo kikuu cha Mabasi mara baada ya jeshi hilo kupata
taarifa toka kwa raia wema.
Kamanda
Sabas alifafanua kwa kusema kwamba, siku ya tukio mtuhumiwa ambaye ni
Imelda Juma alimtuma dereva wa pikipiki maarufu kama “boda boda” aitwaye
Jamal Abdul ili aende maeneo ya Sakina Darajani kwenda kuchukua mzigo.
Mara baada ya dereva huyo kufika katika eneo hilo aliukuta mzigo huo
ukiwa pembeni ya pikipiki nyingine ambayo haikuwa na mtu.
Dereva
huyo wa pikipiki aliuchukua mzigo huo na kuupeleka katika kituo cha
mabasi cha Dar Express kama alivyoelekezwa na mtuhumiwa ambaye ndio
mmiliki wa mzigo huo ili autume kwa mtu aliyefahamika kwa jina moja la
Emmanuel ambaye inadaiwa yupo Dar es salaam.
Wafanyakazi
wa kampuni ya mabasi ya Dar Express waliokuwa ofisini hapo hawakuwa
tayari kuupokea na kuusafirisha mzigo huo bila kuufungua ili
wajiridhishe japokuwa dereva wa boda boda alikataa kufungua mzigo huo
kwa madai kwamba mwenye mzigo alimwambia hasikubali mzigo huo
ufunguliwe.
“Ndipo
wafanyakakazi hao wakamshauri dereva huyo wa boda boda kama hataki
ufunguliwe basi naye pia akate tiketi ili asafiri pamoja na mzigo wake
mpaka Dar es salaam”. Alisema Kamanda Sabas.
Mara
baada ya taarifa hiyo kufika katika kituo kikuu cha Polisi, askari
waliweka mtego na kumkamata mtuhumiwa huyo Imelda Juma ambaye
inasemekana alikuwa maeneo ya karibu na hapo.
Mpaka
hivi sasa Jeshi hilo linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo ili kuweza
kubaini mtambo unaotengeneza fedha hizo bandia huku pia likiendelea
kumtafuta mtumiwa mwingine aitwaye Emmanuel.
Kufuatia
tukio hilo Kamanda Sabas ameendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu
kwa jinsi wanavyoshirikiana na jeshi hilo juu ya utoaji wa taarifa kwani
fedha hizo kama zingesambaa mtaani kwa ajili ya matumizi zingedhoofisha
uchumi wa nchi kwa kiasi fulani.
Aidha
amewatahadhalisha wananchi wa Mkoa huu hasa wafanyabiashara kuwa makini
na noti mbalimbali wanazozipokea toka kwa wateja wao, kwani wengine
hutumia mwanya wa wingi wa noti kupenyeza fedha bandia.
Post a Comment