Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari
iliyotolewa na Ikulu kwa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na kupitia
kwake, kwa mkewe Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa
Afrika Kusini alisema ni msiba mkubwa kwa wote.
“Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa jumla
imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa karne ya 20 na 21.
Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika Kusini kwa kupoteza
kiongozi shupavu, jasiri, mwanamapinduzi, mvumilivu na mstahimilivu,”
alisema Rais Kikwete.
Rais amemwelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo
cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo
uliomwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika Kusini kuwa taifa moja
baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
“Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi
binadamu muungwana anavyopaswa kuwa. Ni wajibu wa wana-Afrika Kusini,
Afrika na dunia kwa jumla kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo,
kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake,” alisema.
Rais Kikwete pia ametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jana na bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemweleza Mandela kama mfano wa kuigwa
na viongozi wa Afrika.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, Profesa Lipumba alisema:
“Tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha
Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Tunamshukuru
Mungu kwa Madiba kwani ametoa mchango mkubwa si kwa Afrika tu bali kwa
dunia nzima katika mapambano ya ubaguzi wa rangi, ni mchango mkubwa
sana,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Hata alipotoka gerezani baada ya kufungwa kwa
miaka 27, Mandela hakuwa na kinyongo bali alisamehe na alianzisha
maridhiano yaliyoleta heshima na kujenga Serikali inayojali haki za
binadamu.” Amewataka viongozi wa Afrika kufuata nyayo zake ili kuleta
heshima ya Bara hilo:
“Afrika bado ina matatizo mengi lakini kama
viongozi watafuata mfano wa Mandela wa kutokuwa na kinyongo na kusamehe
hata baada ya kufungwa gerezani miaka 27, basi wataleta heshima ya
Afrika,” alisema Profesa Lipumba.
Naye mwanasiasa mkongwe nchini, Ibrahimu Kaduma
alisema, Mandela ameacha fundisho kuwa viongozi wanatakiwa na uthubutu
katika kuamua kufanya kile wanachokiamini hata kama itawalazimu kifo.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment