Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

WOTE TUNA CHA KUJIFUNZA KWA NELSON MANDELA

               


NIANZE kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunifikisha hapa nilipo leo, nikiwa na afya njema. Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara, wakati ukisoma habari hii, wapo mamilioni ya binadamu wenzetu kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao hawako sawa.
Hawawezi kusoma kama wewe unavyofanya hivi sasa kwa sababu hali zao haziwaruhusu, wengine wapo mahututi vitandani, wengine wana njaa kali na wengine wamepoteza maisha kwa namna moja ama nyingine.
 Utaona kwamba kwa afya tuliyonayo sasa, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kila jambo.

Dunia inaomboleza kifo cha mtu mkubwa, maarufu na mwenye mvuto, Nelson Mandela, ambaye alifariki dunia Alhamisi iliyopita, akiwa na umri wa miaka 95. Kwa umri wake, na hasa barani Afrika, watu hawalii, bali wanasherehekea.
Lakini kifo cha shujaa huyu, kinatuachia mambo mengi sana ya kujifunza.


Siyo tu kwa maisha yetu binafsi kama binadamu, bali pia kwa viongozi wa Afrika, ambao mara nyingi wamekuwa wakiendesha nchi kwa visasi, kujilimbikizia mali na kukosa uzalendo wa nchi zao.
Mandela amejipambanua kama binadamu wa aina yake. Pamoja na kukaa gerezani kwa miaka 27, akifanyishwa kazi ngumu, alipotolewa na hatimaye kuchaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini, kamwe hakuwa na kisasi. Aliunda tume maalum ya upatanishi, ili watu wote, weupe na weusi waliokoseana, kukaa pamoja na kusameheana, kazi ambayo ilifanywa vizuri na Askofu Desmond Tutu.
Aliwaamini na kuwapenda maadui zake. Wakati akitoka jela, nchi yake ilikuwa imegawanyika pande mbili, chama chake cha ANC na kile cha Inkhata Freedom Party, kilichokuwa kikiongozwa na Mangosuthu Buthelezi ambacho kilipendwa na wazungu na hivyo kumfanya kiongozi wake kuonekana kama msaliti kwa watu weusi.
Lakini Mandela aliposhinda uchaguzi, hakumtenga Mangosuthu, alimteua kuwa waziri na kumpa wizara muhimu kabisa ya mambo ya ndani. Na hata Fredrick De Clerk, yule rais aliyemtoa jela, hakumtupa, alimfanya kuwa makamu wa rais ili kumhakikishia kuwa hakuwa na kinyongo na wazungu.
Mandela alipenda Afrika Kusini iwe moja, yenye watu wa rangi tofauti, kila mmoja ajione yuko nyumbani. Alitumia nguvu kubwa kuhubiri upendo miongoni mwa wananchi wake. Alikuwa mkweli, tangu mwanzo, alisema mapambano yake hayakuwa kwa ajili ya kutawala, bali usawa kwa watu wake.

Ndiyo maana baada ya awamu yake ya kwanza, alikataa kuendelea, licha ya ukweli kwamba alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu bado alikuwa akikubalika.
Lazima tukubaliane, ni viongozi wachache wa Afrika wanaoweza kukubali kuachia madaraka kwa hiari, hasa kama wanaona wananchi wao bado wanawahitaji. Mandela anatufundisha kusamehe, kuridhika, kuheshimu na kuamini wengine.
Madaraka ya nchi kubwa kama Afrika Kusini hayakuweza kuyumbisha maisha ya Mandela kama binadamu. Hakujipa uungu mtu. Alibakia kuwa mtu wa kawaida kabisa, akijichanganya na watu wa kada zote, huku akiweka wazi mambo mengi.

Leo hii wakati kila mtu anaguswa na kifo cha kiongozi huyu, ni lazima tutambue kwamba haikutokea kwa bahati mbaya. Mandela alifanya kazi iliyoonekana na kukubalika. Viongozi wetu wa Afrika wanapaswa kujifunza kutoka kwake.
Nchi nyingi za Afrika zinashindwa kutekeleza mipango yake mingi ya maendeleo kwa sababu ya viongozi wake kukataa kwa makusudi kuwaamini wenzao.

Migogoro mingi inayotokea Afrika ni kwa sababu ya tamaa za viongozi kujilimbikizia mali, kukataa kwa makusudi kukaa mezani na wapinzani na kuzungumza kwa faida ya nchi zao.
 Viongozi hao wako tayari kuruhusu risasi na mabomu kwa raia wao, ili mradi tu kuwahakikishia wanaendelea kubaki madarakani.
Mungu ailaze pema peponi roho ya shujaa wetu Nelson Mandela.
Nimepasua jipu, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.


                GPL
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top