********
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kumhoji Mwakilishi wa Uzini, Mohamed Raza, kwa tuhuma za kugombanisha viongozi na wananchi na kushindwa kutetea misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Raza anatuhumiwa kufanya hayo katika matamshi anayodaiwa kuyatoa kwa waandishi wa habari kupitia mkutano wake wa Oktoba mwaka jana na mkanda wa video umetumika kama ushahidi katika kikao cha Kamati ya Siasa ngazi ya jimbo na wilaya.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Malindi jana, Raza alisema ametakiwa kujibu hoja 16 na Kamati ya Siasa ya Jimbo la Uzini na kwamba tayari kamati imetoa mapendekezo kwa ngazi ya wilaya.
Alisema kikao cha kwanza kilikutana Oktoba 27 mwaka jana na kumtaka ahudhurie kwa madai kuwa kulikuwa na mambo muhimu aliyopaswa kuyatolea ufafanuzi kutokana na matamshi yake katika mkutano wake na waandishi wa habari.
“Niliwasilisha ombi la udhuru kutokana na kukabiliwa na safari nchini Dubai, nikaomba wanitajie maeneo ambayo hawajayafamu ili niwajibu kwa maandishi, wenzangu walikuwa wagumu na waliendelea kunijadili bila kunipa nafasi ya kujitetea,” alisema Raza.
Alisema wakati akitafakari hayo, alipokea barua nyingine ya wito kutoka Wilaya ya Kati akitakiwa ahudhurie kikao cha Desemba 13 huko Dunga na kujibu tuhuma 16. Raza aliwataja baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho kuwa ni, Hassan Mrisho Vuai, Shukuru Adam Ali, Ame Abdallah Ame, Shaaban Jabu Kitwana, Mju Silima Makame na Arada Ali Abdallah.
Wengine ni Vuai Ali Mohamed, Usi Ali Mtumwa, Salama Mussa Bilal, Khalfan Salum Suleiman, Ali Makame Usi, Mussa Ali Hassan na Haji Mkema Haji.
Raza alizitaja tuhuma zinazomkabili kuwa ni pamoja na kuzungumzia hadharani, masuala mazito na yenye utata akiwa mwakilishi wa CCM, kuhoji uhalali wa marais Dk Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohamed Shein kuhusu kuunda Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba na kuitisha Bunge la Katiba.
Nyingine ni kutetea muundo wa Serikali tatu, kuwahasimisha wananchi wa Bara na Zanzibar kuchukiana na viongozi wa Muungano.
Nyingine ni kutamka kuwa Watanganyika hawawezi kutawala Zanzibar na kwamba wakijaribu watatawala miembe na minazi.
Pia kutoa kuponda ilani ya uchaguzi inayotaka Serikali mbili akisema mwisho wake ni Kisiwa cha Chumbe.
MWANANCHI
Post a Comment