Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman akizungumza kwenye mkutano
na waaandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Msajili
wa Mahakama, Ignas Kitusi. Picha na Venance Nestory
*********
Jaji Mkuu Mohamed Othman Chande ameitaka Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania kuharakisha mchakato wake wa kuandaa ripoti inayohusu
migogoro ya ardhi nchini ili kutoa nafasi ya kufanyiwa marekebisho
Sheria ya Ardhi.
Jaji Chande ametoa kauli hiyo wakati ambao maeneo
mbalimbali nchini yamekumbwa na migogoro mikubwa ya ardhi na kusababisha
wananchi kupoteza mali,mifugo,makazi na wengine kuuawa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu
sherehe ya Siku ya Sheria Nchini itakayofanyika Februari 3, mwaka huu,
Jaji Chande amesema, “Ukiondoa idadi kubwa ya kesi za jinai, zinazofuata
wa wingi ni kesi za migogoro ya ardhi, hasa za madai, mfano Mahakama
Kuu ya Tanzania pekee kuna kesi za ardhi zaidi ya 6,000.”
Alisema asilimia 60 ya kesi hizo zinatoka kwenye
mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.“Mfumo wa kutatua kesi za ardhi
uko chini ya mamlaka tatu. Ngazi ya chini kabisa ni Baraza la Ardhi la
Kijiji ambalo lipo chini ya Serikali za Mitaa na Halmashauri. Pili, ni
Baraza la Kata,” alisema na kuongeza;
“Na tatu ni Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya
ambalo mamlaka yake ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Baada ya hapo ndiyo kinafuata Kitengo cha Ardhi cha Mahakama Kuu”
alisema.
Alisema tatizo lililopo sasa ni kwamba ili uweze
kutatua migogoro ya ardhi ni lazima uangalie kesi husika ipo katika
ngazi gani na kusisitiza kuwa migogoro mingi ipo katika ngazi za chini
ambazo zipo katika mamlaka nyingine.
“Hivi sasa mfumo wa migogoro ya ardhi na mashauri
ya ardhi unaangaliwa upya na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo
imetembelea mikoa yote nchini na kukutana na wadau wote ikiwamo,
mahakama, Wizara ya Ardhi, wananchi na wanasheria hivyo ripoti hiyo
ikitolewa itasaidia kuboresha sheria,” alisema.
Mahakama za mwanzo
Akizungumzia mahakama za mwanzo, Jaji Chande
alisema, “Tanzania tuna mahakama za mwanzo 960 lakini zinazofanya kazi
ni 803, kati ya hizo zinazofanya kazi mahakama 487 ndiyo zina mahakimu
wa kudumu na nyingine 316 hutoa huduma kwa kutembelewa na mahakimu mara
moja au mbili kwa wiki kutokana na mahakimu kutoishi maeneo hayo.”
Alisema kwa sasa kuna uhaba wa majengo zaidi ya
296 ya mahakama za mwanzo, kwamba kuna majengo 157 ya mahakama za mwanzo
ambayo hayafanyi kazi kwa sababu ya uchakavu.
Alisema mahakama hizo zinakabiliwa na changamoto
nyingi ikiwa ni pamoja na kuwapo katika majengo chakavu na nyingine
zikiwa ndani ya majengo yanayomilikiwa na taasisi mbalimbali na
Serikali, jambo ambalo alisema linazifanya mahakama hizo kuonekana
kutokuwa huru.
Alisema miundombinu ya mahakama nyingi ni mibovu
na kutolewa mfano mahakama za mwanzo zilizopo katika Wilaya za Bagamoyo,
Mkuranga na Kisarawe mkoani Pwani kuwa hazina umeme na kusisitiza kuwa
hali hiyo inachangia kuchelewa kutolewa kwa hukumu na haki kwa wananchi.
Hata hivyo, Jaji Chande aliipongeza Serikali kwa kuongeza Bajeti
ya Maendeleo ya Mahakama kutoka Sh17.8 bilioni mwaka 2012/13 mpaka
Sh42.7 bilioni.
“Tunafungua mwaka mpya wa mahakama na kati ya hiyo
bajeti tumepata Sh5.5 bilioni tu. Tutaendelea na malengo tuliyojiwekea
ya kujenga mahakama za mwanzo 25 na kukarabati nyingine 10. Lakini kwa
kiwango hiki cha fedha tulichopata ujenzi utakuwa mgumu,” alisema Jaji
Chande.
Mahakama kuchomwa moto
Akizungumzia tabia ya wananchi kuchoma moto
mahakama za mwanzo, alisema jambo hilo linawanyima haki watu wenye kesi
zao mahakamani na pia linachelewesha haki kutendeka.
“Tangu mwaka 2012 hadi sasa zimechomwa moto
mahakama za mwanzo nne, mbili za mkoani Mtwara, moja mkoani Lindi na
nyingine Njombe. Mahakama hizi zilikuwa na kesi nyingi na anayeathirika
ni wananchi wenyewe kwani ushahidi unapotea na walioko rumande
wataendelea kusota.”
Alisema mahakama za mwanzo zote nchini mwaka jana
zilipokea kesi 29,507 na kuamua kesi 27,747, “Tatizo la mahakama za
mwanzo ni zile kesi ambazo kila mwaka zinatakiwa kusogezwa mbele, mwaka
jana kulikuwa na kesi 15,533 na mwaka huu Januari kuna kesi 15,303,
idadi ya mrundikano wa kesi umebakia palepale.”
Operesheni Tokomeza
Akizungumzia kesi za watu waliokamatwa katika
Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanza Oktoba 4 mpaka Novemba Mosi mwaka
jana, ambayo ilisitishwa kwa muda kutokana na kukumbwa na kasoro katika
utekelezaji wake, alisema mahakimu waliotoa hukumu ya baadhi ya kesi
hizo hawakuwa miongozi wa vikosi vilivyokuwa vikiongoza operesheni hiyo.
“Watuhumiwa wengi walikamatwa na kufikishwa
mahakamani. Katika kipindi hicho mahakama ilipokea zaidi ya kesi 516
lakini zilizomalizika ni 188. Kesi hizi zimesikilizwa kwa mamlaka ambayo
imepewa mahakama na zilisikilizwa mahakamani siyo kwenye misitu”
alisema
Kesi za muda mrefu
Alisema mahakama imeandaa mipango ya kupunguza
wingi wa kesi zinazosikilizwa kwa muda mrefu, “Kesi kusikilizwa kwa muda
mrefu inategemea ipo katika mahakama ipi. Tumeanza kufanya tathmini ya
kesi zote, pia Mahakama Kuu kuna vikao maalum vimefanyika kuondoa kesi
hizo na tutahakikisha tunazipa kipaumbele kesi za muda mrefu kuliko kesi
mpya.”
MWANANCHI
Post a Comment