******
Makundi ya Urais wa 2015 yanaendelea kuivuruga CCM baada ya
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Singida, Mgana Msindai kuibuka na
kusema atamburuta mahakamani Mwenyekiti mwenzake wa Mkoa wa Geita,
Joseph Kasheku ‘Msukuma’ asipomwomba radhi kwa kumchafua kwa kumwita
mpuuzi.
Hata hivyo, Kasheku amesema Msindai anaweza kwenda
mahakamani huku akisisitiza kwamba hawezi kumwomba radhi kwa kuwa
anaamini kwamba alichofanya ni kinyume cha taratibu za chama na vikao.
Juzi, Kasheku alimponda Msindai mbele ya waandishi
wa habari kwa kitendo chake cha kusema kuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa
yote ya Tanzania wanamuunga mkono, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
katika safari yake ya urais wa 2015 wakati wa sherehe ya mwaka mpya
huko Monduli, Arusha.
Msindai alisema jana kuwa amemtaka Kasheku aitishe
mkutano wa waandishi wa habari na kumwomba radhi. “Asipofanya hivyo
ndani ya siku saba nitampeleka mahakamani,” alisema Msindai.
Msindai pia alikanusha kuwa aliwekwa kitimoto katika mkutano wa wenyeviti wa CCM wa mikoa uliofanyika Zanzibar.
Msindai aliyekuwa Mbunge wa Iramba Mashariki kwa
miaka 15, alikiri kuwa alialikwa pamoja na wenyeviti wenzake sita katika
sherehe ya mwaka mpya iliyoandaliwa na Lowassa huko Monduli.
Katika sherehe hizo, Lowassa alitangaza kuwa
ameanza safari ya matumaini, kauli ambayo wachambuzi wa masuala ya
kisiasa waliitafsiri kama tangazo la kuwania urais mwaka 2015.
Msindai alikanusha kutangaza kuwa wenyeviti wote
wa CCM wa mikoa wanamuunga mkono Lowassa wakati wa sherehe hiyo... “Mimi
ni Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, lakini sikuwahi kuzungumza kuwa
wenyeviti wote wanamuunga mkono Lowassa katika Uchaguzi Mkuu 2015...
kikubwa tulichozungumza ni kumuunga mkono katika safari yake ya
mafanikio katika kuendeleza elimu, maji, ujenzi wa zahanati.”
Msindai alisema wanamwangalia Lowassa kutokana na
uwezo wake katika kusimamia mipango yake ya maendeleo na zaidi katika
kupigania elimu pana kwa Watanzania.
“Alipokuwa Wizara ya Maji alichangia maji
kupatikana Dar es Salaam na mikoani na maendeleo mengi, uwajibikaji
kwenye jimbo lake na aendelee hivyo...hayo ndiyo tuliyomsifia.
Nilizungumza haya na sitabadilika,” alisema Msindai, ambaye alisema
haogopi kufukuzwa.
“Mimi si mpya ndani ya CCM kama ‘Msukuma’. Nina
miaka zaidi ya 40, ninaelewa taratibu zote za chama za udiwani, ubunge
na urais. Kama ni kampeni ni baada ya chama kumpitisha mtu na sisi
tutamuunga mkono... hata mimi ninaweza kuwania urais,” alisema.
Siombi radhi
MWANANCHI
Post a Comment