IDADI
ya mifugo inayokufa kwa kula mifuko ya nailoni inazidi kuongezeka
katika Kata ya Hombolo. Diwani wa Kata ya Hombolo Manispaa ya Dodoma,
Mussa Kawea katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi alisema katika
kipindi cha wiki mbili mifugo inayokufa imefikia 500 huku wafugaji
wengine wakiingia katika umasikini kwa kupoteza ng'ombe zaidi ya 20.
Alisema
mifuko hiyo ambayo imezagaa sana eneo la Hombolo kutokana na kuongezeka
kwa shughuli za kibinadamu zilizochangiwa na uwepo wa Chuo cha Serikali
za Mitaa Hombolo imekuwa chanzo kikubwa cha kuwatia katika umasikini.
Kawea
alisema licha ya mvua kuanza kunyesha na majani kuongezeka lakini
ng’ombe wamekuwa wakila mifuko hiyo inayozagaa ovyo kutokana na kuwa na
ladha ya chumvi chumvi.
Alisema
pamoja na wafugaji kulifikisha suala hilo kwenye kikao cha Baraza la
Madiwani lakini hakuna kitu chochote kilichofanyika mpaka sasa.
Alisema
ni muhimu kwa Serikali ikapiga marufuku utengenezaji wa mifuko hiyo
kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa mifugo huku akiwataka wananchi
wenye mazoea kuhakikisha kwamba hawaitupi hovyo na wanaichoma.
“Hali hii inatishia umasikini kwa wafugaji tunaomba Serikali kuangalia suala hili kwa makini. Alisema, kutokana na vifo vya ng’ombe vinavyotokea kila mara wafugaji wa maeneo hayo wameitaka Serikali kutimiza maagizo wanayoyatoa ikiwemo lile la kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo.
“Serikali
ilipiga marufuku utengenezaji wa mifuko ya rambo na kuagiza viwanda
vitengeneze mifuko ya karatasi ambayo ni rahisi kuharibiwa baada ya
matumizi lakini agizo hilo linaonekana halijazingatiwa,” alisema.
Alipohojiwa
hivi karibuni juu ya athari anazopata ng’ombe anapokula mfuko wa
plastiki Daktari wa Mifugo mkoani hapa, Goodluck Ndaweka alisema ng’ombe
anapokula mfuko wa plastiki husababisha mfuko ule kwenda kufunga utumbo
mwembamba jambo ambalo husababisha chakula anachokula kishindwe kupita.
Alisema kutokana na hali hiyo ng’ombe hukonda na hali hiyo hupelekea kifo chake.
HABARI LEO
Post a Comment