Siku moja baada ya watu 25 kuripotiwa kufa kwa ajali tofauti
nchini ikiwamo iliyoua familia mkoani Singida, familia nyingine ya watu
wanne imeteketea kwa moto ndani ya nyumba katika Kijiji cha Iputi
wilayani Ulanga mkoani Morogoro.
Pamoja na tukio hilo, imeripotiwa kuwa watu
wengine 10 wamefariki dunia katika matukio tofauti ya ajali zilizotokea
katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Singida.
Matukio hayo ni mwendelezo kwa mwaka 2014 kuanza
vibaya baada ya vyombo vya habari jana kuripoti vifo vya watu 15 katika
ajali tofauti zilizotokea Same mkoani Kilimanjaro, Singida na Lindi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine
Shilogile alisema kuwa familia ya watu wanne ya baba na watoto watatu,
iliteketea kwa moto uliotokea saa 7 usiku juzi katika Kijiji cha Iputi
wilayani Ulanga.
Shilogile aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Kasmu Maleo (42), Kumbukeni Maleo (5), Mwanaisha Maleo (4) na Alfa Maleo (2).
Alisema kuwa katika ajali hiyo mama wa watoto hao,
Kisia Kihina (35), alijeruhiwa vibaya na moto na amelazwa katika Kituo
cha Afya cha Mwaya akipatiwa matibabu.
Kamanda Shilogile alisema kuwa chanzo cha ajali
hiyo ni moto ulioachwa na familia hiyo baada ya kupika chakula cha
jioni, hivyo ukateketeza nyumba hiyo.
Wafukiwa na kifusi Karatu
Katika tukio jingine, watu sita walifariki dunia
baada ya kufunikwa na kifusi wakati walipokuwa wakichimba changarawe
wilayani Karatu mkoani Arusha.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Japhet
Lusingu alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 10:00 juzi jioni katika
Kitongoji cha Sumawe Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Aliwataja waliokufa kuwa ni John Oswald (22),
Tumaini George (23), Benjamini George (16), Rafael Robet (23), John
Jumanne (28) na Emmanuel Oswald (33) wote wakazi wa Sumawe wilayani
Karatu.
MWANANCHI
Post a Comment