Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya (pichani) ameeleza alivyoibiwa mtandao
wa miundombinu ya umwagiliaji na bomba za maji 80 katika shamba lake
lililopo katika Kijiji cha Chomvu Usangi, wilayani Mwanga, Kilimanjaro.
Hatua hiyo imekuja baada gazeti hili kuandika
habari za Polisi wilayani Mwanga kufanya operesheni ili kuwasaka
watuhumiwa wa wizi huo wa mabomba hayo yenye thamani ya Sh2.4 milioni.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo
walilalamikia operesheni hiyo kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakikamatwa
wakati hawahusiki.
Taarifa iliyotolewa na Msuya jijini Dar es Salaam,
jana ilisema, usiku wa Septemba 20, 2013, watu wasiojulikana waliingia
shambani kwake na kuharibu mtandao wa umwagiliaji maji zikiwemo bomba
80.
Msuya alisema licha ya mtandao huo wa bomba kufukiwa ardhini kwa zege bado wahalifu hao walifanikiwa kuzing’oa na kuondoka nazo.
“Uharibifu na wizi huu ni mkubwa na mahali pengine
walitumia misumemo ya chuma kukata mabomba na kuyaachanisha na zege,”
alisema.
Alisema Septemba 21, 2013 taarifa za uhalifu huo
zilifikishwa kwa watendaji wa Kijiji cha Chomvu, Kata ya Chomvu, Tarafa
ya Usangi na hatimaye uongozi wa Polisi wa Wilaya ya Mwanga na Mkoa wa
Kilimanjaro.
“Nilipokuwa nyumbani wilayani Mwanga, wakati wa
Krismasi, nilipata maelezo kutoka kwa maofisa wa polisi kuhusu maendeleo
ya upelelezi wa uhalifu huu,” alisema Msuya.
Aliwapongeza Polisi kwa kazi wanayoendeea kuifanya
licha ya kuwa katika mazingira magumu na kusema kwamba ana imani
wahalifu hao watakamatwa wakiwa na vidhibiti ili waweze kufikishwa
mahamani.
Alisema Tanzania inaongozwa na kutawaliwa na
sheria na kwamba viongozi wanashauriwa kuwatia moyo polisi kwa kazi ya
kupambana na uhalifu nchini.
Msuya alisema wasipofanya hivyo uhalifu wa aina hiyo unaweza kusambaa na kutokea sehemu nyingine kitendo ambacho hakikubaliki.
Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert
Boaz alikaririwa akithibitisha kutokea kwa tukio hilo nyumbani kwa
Msuya na kutahadharisha watu wasipotoshe uchunguzi huo.
MWANANCHI
MWANANCHI


Post a Comment