“Zimetolewa sifa nyingi zikimwelezea Waziri Mgimwa juu ya uaminifu wake.
Mimi nimesimamahapa kuthibitisha hilo, kwa muda mfupi alioteuliwa
amefanya kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa na sisi katika Serikali
tukasema sasa wizara imempata waziri anayestahili,”
Mizengo Pinda.PICHA|MAKTABA
****
Wakati Rais Jakaya Kikwete jana akiongoza mamia ya wakazi wa
Mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri wa
Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameahidi kuwa
Serikali itatekeleza ahadi alizotoa jimboni kwake.
Dk Mgimwa, ambaye alikuwa Mbunge wa Kalenga,
alizikwa jana saa 10 jioni katika kijiji cha Magunga kilichoko Kata ya
Maboga mkoani Iringa.
Dk Mgimwa aliyefariki Januari mosi mwaka huu
nchini Afrika Kusini, kutokana na tatizo la figo, alizikwa katika shamba
la makaburi lililopo karibu na nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji
hicho.
Akitoa ujumbe wa Serikali katika mazishi hayo,
Pinda alisema wataziangalia ahadi alizotoa marehemu na kuzifanyia kazi
zile ambazo hazijakamilika.
“Katika kumuenzi marehemu Mgimwa, sisi Serikali tunamuenzi kwa kutekeleza mema yote aliyotuachia,” aliongeza Pinda.
Pinda alisema Serikali imepoteza waziri aliyetegemewa katia wizara husika na taifa kwa jumla.
“Zimetolewa sifa nyingi zikimwelezea Waziri Mgimwa
juu ya uaminifu wake. Mimi nimesimama hapa kuthibitisha hilo, kwa muda
mfupi alioteuliwa amefanya kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa na sisi
katika Serikali tukasema sasa wizara imempata waziri anayestahili,”
alisema Pinda.
“Kati ya Oktoba 4-15 sisi serikalini tulimtuma
Mgimwa aende Marekani akafanye kazi moja na ndipo ilipogundulika kuwa
alikuwa na tatizo lakini yeye alivumilia hadi kazi ilipoishi ndipo
akarudi na alipofika akasema ngoja aende Afrika Kusini akaangalie afya
yake,” alisema Pinda.
Kwa upande wake, mtoto wa marehemu Godfrey Mgimwa
ambaye alisimama kutoa shukrani kwa Serikali na wananchi waliofurika
katika mazishi hayo, aliiomba Serikali kutekeleza ahadi kadhaa
alizoziacha baba yake kama njia pekee ya kuwafariji wanafamilia na
wananchi wa Jimbo la Kalenga.
“Siku 10 kabla ya kufariki dunia, baba aliniambia
kuwa wakazi wa Jimbo la Kalenga ninawapenda sana katika kipindi hiki
ambacho hali yangu si ya kuridhisha ningependa niwapelekee mabati 1,200.
Ametutoka bila ya kutekeleza ahadi hiyo, watoto na wanafamilia tunaomba
Serikali kutekeleza ahadi hizo kama njia pekee ya kutufariji,” alisema
Godfrey.
Godfrey alitaja miradi minne ambayo baba yake
alimweleza kuwa alikuwa anataka kuwatekelezea wakazi wa jimbo hilo kuwa
ni pamoja na umeme, minara ya simu, uanzishaji wa ushirika wa kuweka na
kukopa na barabara.
Akitoa mahubiri yake katika ibada ya misa ya
mazishi ya marehemu Mgimwa, Msaidizi wa Makamu wa Askofu wa Kanisa
Katoliki, Jimbo la Iringa, Padri Julius Kingalawe, alisema taifa
limefikia hatua mbaya ya watu kutokuaminiana.
Post a Comment