Algeria imeanza siku tatu za
maombolezi ya kitaifa kufuatia kuuawa kwa watu sabini na saba kwenye
ajali iliyohusiha ndege moja ya Kijeshi Kaskazini Mashariki mwa nchi
hiyo.
Abiria mmoja alinusurika ajali hiyo
iliyohusisha ndege aina ya Hercules C-130 iliyoanguka katika eneo la
milima ya Oum al-Bouaghi, ikiwa njiani kuelekea mji wa Constantine.
Ripoti zinasema hali mbaya ya anga ilisababisha ajali hiyo ya ndege.
Rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika amewasifu wanajeshi waliopoteza maisha yao na kuwataja kama wafia dini wa taifa hilo.
Wengi wa abiria sabini na nane waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni maafisa wa kijeshi na familia zao.
Mabaki ya ndege ya jeshi la Algeria iliyoanguka
Mwanajeshi aliyenusurika, anaripotiwa
kuendelea kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Constantine
kufuatia majeraha ya kichwa.
Wizara ya Ulinzi imesema kuwa imeunda
tume maalum kuchunguza ajali hiyo na kuwa Ahmed Gaid Salah, ambaye ni
mkuu wa majeshi nba naibu waziri wa Ulinzi atazuru eneo la ajali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa
vyombo vya habari, wizara ya ulinzi imesema kuwa hali mbaya ya anga
iliyohusisha kimbunga na mvua kubwa ya barafu ilisababisha ajali hiyo.
Runinga ya taifa ilionyesha picha za ajali hiyo.
Awali maafisa wa Ulinzi na shirika
hilo la habari liliripoti kuwa watu 103 walikuwa ndani ya ndege hiyo
lakini idadi hiyo ilipunguzwa hadi watu sabini na nane.
Post a Comment